KIJIWENI LIVE: Wema akisanuka pale WCB kuna pesa zake kibao

BONGO hakuna lockdown lakini haimaanishi corona haipo. Ugonjwa upo, unasambaa kwa kasi na unaua. Jilinde. Linda wenzako. Fuata ushauri wa wataalamu. Karibu Kijiweni; Luqman Maloto na Dk Levy ndio wenyeji wako.

LUQMAN: Kwa mara ya kwanza katika historia, kafa polisi anayeliliwa na kila mtu.

DK LEVY: Halafu anaongelewa na mpaka na masela wa hip hop yaani kubum kabam zile za kina Fid Q na Profesa Jay.

LUQMAN: Prof Jay ni Mbunge wa Chadema na kila siku wanawalalamikia polisi, ajabu polisi huyu amemgusa Jay na u-Chadema wake. Kweli yule jamaa alikuwa polisi wa wote.

DK LEVY: Hakuwa polisi wa wote. Alikuwa polisi wa ajabu. Nasikia vibaka waliokamatwa aliwapa daawa badala ya vipigo na pingu. Aliwapa mawaidha mpaka wanamwaga macho. Vibaka walikuwa wanaumizwa na maneno yake kuliko vipigo vya wananchi wenye hasira kali. Yule jamaa alikuwa Nabii kwenye umbile na jukumu la kipolisi. Zaidi alitosheka na mshahara.

LUQMAN: Umeanza uwendawazimu wako. Watu tupo ‘sirias’ wewe unaleta umajinuni. Yule jamaa anaitwa Masoud Mohamed. Begani alikuwa na nyota tatu, yaani Mrakibu Msaidizi. Weupe wanaita “assistant superintendent”. Kisha Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OCCID). Mwamba amewahi sana kuondoka. Na hilo ndilo linauma.

DK LEVY: Siku zote watu wa namna hii, huwa karibu sana na njia ya kwenda alikokwenda. Sina maana wengine waogope kuwa kama yeye kwa kuamini kuwa watawahi kwenda alikokwenda. Lakini pia yawezekana huko wanakowahi kwenda watu wenye hulka, tabia, moyo na matendo kama yeye kukawa kutamu zaidi kuliko kubaki duniani. Yawezekana kaondolewa ili kutengana na dunia hili lililojaa upuuzi mwingi na magonjwa kama yote.

LUQMAN: Tumuombee ASP Masoud Mohamed, safari iliyo njema. Tuhame mada. Naona wenzetu baada ya Karantini, wameshadhibiti corona, sasa hivi ligi za soka zinafunguliwa. Sisi hata karantini bado lakini Rais wetu amesema anafikiria kuruhusu ligi kuchezwa bila mashabiki. Je, hatupo vizuri?

DK LEVY: Hatupo vizuri kivipi? Unataka tufanyeje ili ujue tupo vizuri? Karantini ya nini Sasa? Rais ataruhusu ligi ichzwe soon. Halafu inakuaje ligi zinakuwa za kwanza kufikiriwa kuliko elimu? Au soka ndo kila kitu kwa sasa?

LUQMAN: Unashauri nini kifanyike? Hukawii kujiona mtaalamu wa afya.

DK LEVY: Nashauri tu kifanyike kitu kwa ajili ya kitu na watu. Unaomba ushauri wangu wakati umetoka kusifia matope hapa hapa?

LUQMAN: Huna nyimbo wewe. Ila ndugu yangu maisha yamebadilika sana. Aunty Ezekiel siku hizi anauza baa. Jacqueline Wolper fundi cherehani. Wema Sepetu kawa mama wa mapishi. Huoni dunia inaelekea ukingoni?

DK LEVY: Hizo ni hatua nzuri sana wamefikia kimaisha. Maana hapo kabla walikuwa watumishi tu wa kucheza ‘sini’ chache kwenye filamu za wasanii wenzao. Kama leo wana miradi yao ni suala la kuwapongeza sana. Sasa wewe unadhani bila hizo shughuli wanazofanya hapa mjini wangekuwa wageni wa nani? Ujue wale ni watu wazima sana hivi sasa, hebu fikiria kwamba 2006 walikuwa tayari watu wazima, vipi leo 2020 si watakuwa wazee?

LUQMAN: Umezeeka wewe, sio Wema. Yaani Aunty awe mzee leo? Tena Wema na Wolper bado wabichii, maana hata hawajazaa.

DK LEVY: Sawa kwa wewe tindinga sishangai ukiona wale ni wabichi. Maana nasikia watu mliokulia Kanda ya Ziwa mnachanganywa sana na mapouda a.k.a mekapu. Ndo maana vibibi mnaona kama vibinti. Mtaliwa hapa mjini mpaka mfe kwa corona.

LUQMAN: Unavyoponda utafikiri ukipewa ofa ya kumuoa Wolper au Wema utakataa.

DK LEVY: Kwamba dunia itakuwa imeishiwa wanawake au nitakuwa nimeshikiwa bunduki au kuwa nao itakuwa ni tiketi ya kwenda peponi? Hata kama nitaambiwa njia ya kwenda peponi ni kuwa nao hao, nitalazimika kutafuta mawakili 17 kutoka pande zote za dunia wanipe back up.

LUQMAN: Maneno tu. Sizitaki mbichi hizi. Aisee imebumbuluka kumbe Harmonize ana mkwanja mrefu kuliko Diamond. Aliona hawezi kuwa chini ya mtu anayemzidi pesa. Akasepa zake kuanzisha Konde Gang.

DK LEVY: Hata hili ulikuwa hujui blaza? Upo mjini kuhesabu maghorofa au kutakatisha pesa? Sasa tangu lini Mondi akamzidi Konde Boy? Mimi nawaangaliaga tu mnavyoneng’eneka kama sare za shule zilizoanikwa kwenye kamba. Yaani yule Sara Mzungu unadhani aliingia kichwa kichwa?

LUQMAN: Usimsifie sana. Ile hela ya Konde Boy sio ya muziki, ni tour ya ukweni. Diamond ni zake peke. Sio za ukweni

DK LEVY: Ndo maneno yenu. Zake peke yake wakati kuna wachangiaji hapo kama Konde Boy, Rayvanny, Lavalava, Mavoko, Darleen, Zuchu na Mbosso? Sijakutajia Wema, Zari, Tanasha, Hamisa na Penny. Wote hao walishiriki kumuingiza pesa direct and indirect. Lakini Konde Boy kakata mauno jukwaani na kitandani ili ku-make more money. Konde Boy ni noma na nusu Sheikh.

LUQMAN: Ila kweli, Wema angepata mawakili wazuri, ana pesa nyingi ndani ya Diamond lakini hapati kitu kwa unyonge wake. Wema alimpa Diamond bonge la lift. Bora Zari, Mobetto na Tanasha wamepata watoto, angalau watapata matumizi. Wema ana nini sasa?

DK LEVY: Wema aliumbwa kuwatumikia watu. Tatizo lake anatumia mtu badala ya watu. Angejiingiza kwenye siasa kitambo kileee angepiga pesa sana. Yeye akajiingiza kwenye mapenzi tatizo ndo lilipoanzia. Sasa hivi sasa mpaka Hamisa anafaidi matunda ya Wema aiseee. Waganda na Wakenya wanakula mema ya Wema kupitia Mondi Bin Laden. Akili kumkichwa, atafute mawakili wenye masivii yao wanaweza kumtengenezea kitu akapata pesa. Mondi kamtumia sana Wema aiseeee.