Waziri kutegua kitendawili Yanga

Muktasari:

  • Kikao hicho kilichifanyika Jumatatu iliyopita Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kilitakiwa kuendelea siku inayofuata, lakini hakikufanyika kufuatia Dk. Mwakyembe kupata udhuru.


WAKATI kampeni za Uchaguzi wa Yanga zilizotarajiwa kuanza leo Alhamisi zikisogezwa mbele kutokana na wagombea kuhofia usalama wao, Serikali kwa mara nyingine inatarajiwa kutengua hatma ya uchaguzi huo baada ya kufanyika kikao kizito.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alikutana na pande zote zinazohusika kwenye uchaguzi huo na kuna baadhi ya mambo yamemshtua, lakini mbivu na mbichi atazitangaza kesho Ijumaa.

Taarifa zinasema Serikali kupitia Waziri Mwakyembe ilikutana na pande tatu kwa maana Baraza la Michezo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Yanga kujadiliana ishu ya uchaguzi huo.

Kikao hicho kilichifanyika Jumatatu iliyopita Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kilitakiwa kuendelea siku inayofuata, lakini hakikufanyika kufuatia Dk. Mwakyembe kupata udhuru.

Habari zaidi zinasema kikao hicho sasa kinaweza kumalizwa kesho Ijumaa ambapo maamuzi ya kikao hicho yanaweza kubadilisha zoezi zima linaloendelea sasa.

“Tutaendelea na hicho kikao Ijumaa tulishakutana Jumatatu na ilikuwa tuendelee Jumanne lakini Waziri akapata dharura nafikiri wataendelea Ijumaa (kesho) serikali inataka kuona busara zinatumika katika hili,” alisema mmoja wa viongozi wa TFF.

Shirikisho hilo kupitia Kamati ya Uchaguzi imekuwa ikiendesha mchakato wa uchaguzi huo wa Yanga, huku Kamati ya Uchaguzi ya Yanga ikiwekwa kando kwa kilichoelezwa mapendekezo yao kwa manufaa ya uchaguzi huo yanapuuzwa.

Lakini wanachama na wadau wa klabu hiyo wanakataa kinachoendelezwa na TFF kwa madai wenye jukumu la kuusimamia uchaguzi huo ni Yanga wenyewe na TFF wanapaswa kuwa waangalizi tu.