Waziri Mwakyembe kuiaga timu ya Afrika

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe

Muktasari:

  • Tanzania itashiriki michezo hiyo ya 12 ikiwa na rekodi ya kuvuna medali 24 tangu ilipoanza kushiriki mwaka 1965, ambazo ni dhahabu sita, fedha tisa na shaba tisa zilizotwaliwa na timu za riadha, ngumi na netiboli ambayo ndiyo ilikuwa ya mwisho kushinda kwenye michezo ya 2011 mjini Maputo Msumbiji.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ataikabidhi bendera ya Taifa timu ya Tanzania itakayoagwa Kesho Jumanne kuelekea Morocco kwenye michezo ya Afrika
Hafla ya kuiaga timu hiyo itakayoondoka keshokutwa Jumatano itafanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 7 Mchana
Timu ya judo na riadha ndizo zitaiwakilisha nchi kichezo ya Afrika itakayofunguliwa Agosti 19 kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat.
Msafara wa Tanzania utakuwa na wanariadha, Gabriel Geay, Natalia Elisante, Sarah Ramadhan, Regina Mpigachai, Ally Gulam, Benjamini Kurwa na kocha Mwinga Mwanjala wakati judo itawakilishwa na Anangisye Kwele, Abdulrabi Alawi, Ally Hamisi Husein na kocha Innocent Malya.
Mfalme wa Morocco, Mohammed VI ndiye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi itakayoshirikisha wanamichezo kutoka mataifa 54 ya Afrika watakaochuana katika michezo 23 tofauti.
Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha mesema hafla ya kuiaga timu ya Tanzania itaongozwa na waziri Mwakyembe na maandalizi yote yamekamilika.
"Timu zote zimeingia kambini Leo Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kuagwa Jumanne na Judo wataondoka Jumatano kuelekea Morocco wakati riadha wenyewe wataondoka Agosti 20 kutokana na mashindano yao Morocco kuanza Agosti 23 hadi 26," alisema.