Waziri Mwakyembe aonya wanaobeza taasisi ya sanaa

Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe

Muktasari:

Kauli hiyo ya Mwakyembe imetolewa ikiwa ni siku chache tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwa katika hafla ya msanii Diamond ya kukutana na wakazi wa Tandale kudai kwamba chuo hicho hajawahi kusikia kimetoa msanii maarufu.

Pwani. Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema Taasisi ya Sanaa Bagamoyo (TaSUba) ni kiwanda cha wasanii na kushauri watu kuacha kukibeza.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo  alipokuwa akifungua Tamasha la 37 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, linalotarajia kufika kilele Oktoba 27 mwaka huu.

Mwakyembe amesema historia ya chuo hicho inaonyesha wasanii wengi waliopikwa katika chuo hicho wanafanya vizuri ikiwemo nje ya nchi ambapo wamesaidia katika kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia.

"Wanaofikiri chuo hiki hakina umuhimu watakuwa wanajidanganya sana, kwani hata hao maofisa Sanaa na utamaduni mnaowaona nchi nzima asilimia 95 wametoka hapa na wamekuwa wakiisaidia serikali kwa kiasi kikubwa.

" Pia watendaji akiwemo Katibu wa Bodi ya Filamu,Joyce Fisoo, ambaye amewahi kushindwa tuzo mbalimbali za filamu kimataifa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa(Basata),Godfrey Mngereza ambaye ni mpigaji mzuri wa vyombo vya muziki.

"Bado tuna wahadhiri wengi katika vyuo vyetu vikuu ambao wamewapika wasanii wengine, sijui hao supastaa mnaowataka nyie ni wapi?"alihoji Mwakyembe.

Katika ushauri wake amewataka watu kwenda kupata historia ya chuo hicho kabla ya kukinyooshea kidole na utendaji wake na viongozi wa chuo nao kujitahidi kukitangaza ili kuepuka kuwapa watu nafasi kukizungumzia ndivyo sivyo.

Akizungumza kuhusu tamasha hilo la utamaduni lolilokutanisha nchi kumi zikwemo za Ulaya, Waziri Mwakyembe amewasihi watanzania kuhudhuria kwa wingi ili kujifunza tamaduni za watu mbalimbali.

Wakati kwa upande wa wasanii amewataka kutumia fursa za warsha zinazotolewa katika kipindi chote kama njia ya kuwasaidia kuboresha kazi zao.