Waziri Mkuu Majaliwa autaka ubingwa Afcon

Muktasari:

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kazi kubwa ya kushawishi FIFA kuyaleta mashindano haya hapa nchini pamoja na ujio wa Rais wa FIFA, pia TFF kwa uratibu wa mashindano hayo sasa.

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhakikisha Tanzania inatwaa ubingwa katika fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17.

Tanzania itawakilisha na timu ya Serengeti Boys, itakuwa mwenyeji wa fainali za Afrika (Afcon) zilizopangwa kuanza Aprili 14 hadi 28, Dar es Salaam.
Majaliwa alitoa agizo hilo leo Bungeni, Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto.

Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali imehusika vipi na mashindano hayo ya Afcon na mkakati wa kuendeleza utalii nchini, ambapo Waziri Mkuu alisema maandalizi yote yanaendelea kufanyika na Serikali imejiandaa  kupokea wageni hao.

Waziri Mkuu alisema TFF inaendelea na maandalizi ya mashindano hayo baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kuipa Tanzania uenyeji wa fainali hizo.

Amesema Watanzania wanatakiwa wawe wazalendo na kuipa ushirikiano timu yao ili kuhakikisha inaibuka mshindi kwenye fainali hizo.

Pia Waziri Mkuu amesema Wizara ya Maliasili na Utalii itatumia mashindano hayo kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. “Tutawapeleka Kilwa wakaone majengo ya zamani yaliyokaliwa na Waarabu na maeneo mengine.”

Waziri Mkuu amewasihi Watanzania kutumia fursa ya mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika nchini kwa kufanya shughuli mbalimbali zitakazowaongezea kipato. “Kwa kupitia mashindano hayo sisi kama Watanzania tumejipanga huduma zote zipo za chakula, hoteli na usafiri.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kazi kubwa ya kushawishi FIFA kuyaleta mashindano haya hapa nchini pamoja na ujio wa Rais wa FIFA, pia TFF kwa uratibu wa mashindano hayo sasa.