Wawa aiwahi Mtibwa Sugar

Thursday May 16 2019

 

By Thobias Sebastian

WATETEZI wa Ligi Kuu Bara, Simba leo watashuka uwanjani kuvaana na Mtibwa Sugar, huku beki wao kisiki, Pascal Wawa ikielezwa amepona na kama Kocha Patrick Aussems anataamua kumpanga, atakinukisha kama kawaida tu.

Wawa amekosa michezo kadhaa tangu alipoumia kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe, ila kwa sasa amepona na Daktari wa timu hiyo, Dk. Yassin Gembe akisema imekabaki kwa Aussems tu.

Beki huyo wa kati aliyeumia nyonga dakika ya sita tu ya mchezo huo ulioisha kwa suluhu, jana alikuwa sehemu ya kikosi kilichopiga tizi asubuhi kwenye Uwanja wa ndani wa Sea Scape ilipo kambi ya Simba.

Meneja wa Simba alisema kurejea kwake kutaongeza nguvu kwenye eneo la ulinzi lililokuwa likitegemea wachezaji wawili tu, huku Kocha Aussems alisema amefurahi Wawa kupona, lakini bado hajaamua kumtumia leo.

“Ndio kwanza ametoka katika majeraha kumtumia kwa haraka yanaweza kutokea mawili akafanya vizuri na kuingia moja kwa moja kwenye timu, ila kutokumtumia kwa haraka anapata pia muda wa kutosha kufanya mazoezi huku akipona zaidi,” alisema Aussems.

Naye Dk Gembe alisema; “Wawa amepona na ameanza kufanya mazoezi na wenzake na uwezo wa kucheza endapo kocha ataamua kumtumia, ila yupo fiti kabisa kwa sasa.”

Advertisement