Wawa ahamishia mazoezi yake ufukwe wa Coco

Sunday April 5 2020

Mwanaspoti, Tanzania, Wawa ahamishia, Simba SC mazoezi yake, ufukwe wa Coco

 

By Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Beki wa kati wa Simba, Paschal Wawa, ameamua kuhamishia mazoezi anayofanya katika ufukwe wa Coco jijini hapa kujifua katika kipindi hiki cha mapumziko ya kupisha juhudi za Serikali kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa corona.
Wawa ameamua kuweka kambi binafsi kwenye fukwe za bahari wa Coco akipiga mazoezi na akageuza sebule yake kuwa ukumbi wa gym kwa muda.
Hii ni kutokana na kusimama kwa mechi za ligi katika kipindi hiki cha kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona ambao umekuwa tishio dunia nzima.
"Kwangu muda wote ni kazi na hata sasa napambana mwanzo mwisho Mungu abariki,  tutakaporudi kwenye ligi niwe katika kiwango changu au zaidi,"alisema Wawa.
"Nafanya mazoezi yangu binafsi nyumbani wakati mwingine naenda Coco Beach. Coco kwa sababu ya mazingira tulivu na mchanga mwingi."
Alisema,  hana wasiwasi na kiwango chake hâta kama kipindi hiki ligi imesimama kwa sababu anajitambua na anapambana na mazoezi.
Alisema,  kutokana na maagizo ya kujikinga na ugonjwa wa corona, amekuwa mwangalifu na anachukua tahadhari kuona anajilinda na kuwalinda wengine.
Wawa aliyewahi kukipiga Azam FC, amekuwa tegemeo ndani ya kikosi cha Simba kutokana na kufanya kwake vizuri.

Advertisement