Watu 12 washikiliwa sakata la kutekwa Mo Dewji

Muktasari:

Mo ametekwa leo asubuhi akiwa anaelekea kwenye mazoezi katika hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema idadi ya watu wanaoshikiliwa kwa mahojiano kuhusu tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohamme Dewji ‘MO Dewji’, imefikia 12.

Mapema leo asubuhi Mambosasa alitaja idadi ya wafanyakazi watatu wa hoteli hiyo ndiyo wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

MO ametekwa alfajiri ya leo Oktoba 11, katika hoteli ya Colosseum iliyopo Masaki, jijini Dar es salaam.

"Kwa sasa wako 12 wakiwamo walinzi wote watano waliopo Kampuni ya G1 inayosimamia ulinzi wa hoteli hiyo, pia kuna security Manager wa hoteli,"amesema Mambosasa.

Mambosasa ametoa taarifa hiyo baada ya kupigiwa simu na Mwandishi wa gazeti hili akitaka kufahamu ukweli wa kushikiliwa kwa idadi.

Vyanzo kutoka eneo la tukio hotelini hapo zinaeleza idadi hiyo iliongezeka mapema leo baada kuchukuliwa walinzi hao kwa mahojiano zaidi.

Aidha, Mambosasa amesema watu hao wataendelea kushikiliwa na Polisi. "Wewe mbona unakimbilia kujua wataachiwa lini?, wapo tunavyoongea hivi wako ndani,"amesema Mambosasa alipoulizwa ni lini wataachiwa.

Aidha, Mambosasa amesema hadi sasa hakuna taarifa zozote za awali walinazo kuhusu kupatikana kwa mfanyabiashara huyo.