Watatu wapigwe bei Pogba atue Real Madrid

Muktasari:

Ugumu mwingine unaowakabili Real Madrid kwenye usajili huo wa Pogba ni pesa wanayotaka Pogba, ambapo mabosi wa Los Blancos kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na wenzao hao kujadili mpango huo.

MADRID, HISPANIA. Hakuna namna. Real Madrid sasa inasubiri kuwapiga bei mastaa wake watatu kabla ya kurudi tena Manchester United kumfukuzia kiungo Paul Pogba.

Kiungo huyo Mfaransa mwenye medali ya ubingwa ya Kombe la Dunia bado matamanio yake ni kuachana na Man United kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, licha ya kwenda kujiunga na timu yake huko kwenye maandalizi ya msimu mpya katika kambi ya Australia.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane bado anahitaji huduma ya kiungo Pogba akimweka kwenye orodha ya wakali wake anaowataka katika dirisha hili la majira ya kiangazi, lakini sasa huduma yake haiwezi kupatikana hadi hapo watakapofungulia mlango wa kutokea Bernabeu mastaa wake wengine.

Ripoti zinadai kwamba mastaa Gareth Bale, James Rodriguez na Isco wote wapo kwenye orodha ya kufunguliwa mlango wa kutoka ili kumpisha kiungo huyo wa Kifaransa kutua Santiago Bernabeu.

Ugumu mwingine unaowakabili Real Madrid kwenye usajili huo wa Pogba ni pesa wanayotaka Pogba, ambapo mabosi wa Los Blancos kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na wenzao hao kujadili mpango huo.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Perth, Austrailia, kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer alizungumza kitu kuhusu Pogba na kusema kwamba Manchester United haina kawaida ya kuwauza wachezaji wake nyota.

"Kumekuwa na maneno mengi kuhusu wachezaji, wale wanakuja na wanaoondoka. Kwangu mimi, hii naone kama kawaida tu. Hadi hapa tulipo, hakuna ofa yoyote tuliyopokea kuhusu wachezaji wetu. Kuanzia Paul na wachezaji wengine tulionao wamekuwa na mikataba mirefu hapa," alisema.