Watanzania wampa mzuka Banda Taifa Stars

Muktasari:

  • Kitendo cha Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais John Magufuli na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe kuelekeza nguvu kwa Taifa Stars, kimemfanya beki, Abdi Banda akiri morali yao kwa sasa iko juu.

Dar es Salaam. Beki wa Baroka FC ya Afrika Kusini na Taifa Stars, Abdi Banda anasema morali yake kwa timu ya taifa imeongezeka zaidi kutokana na namna Serikali ya Tanzania na Watanzania kwa ujumla walivyorudisha imani kwao hivyo wanakwenda Cape Verde na nguvu mpya.

Banda amejiunga katika kikosi cha Taifa Stars jana Jumapili akitokea Afrika Kusini katika klabu yake hiyo.

Kinachofanywa sasa na taifa chini Rais John Magufuli na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe kimewafanya wachezaji watambue umuhimu na majukumu yao Tanzania na kusababisha kazi yao kuwa nyepesi.

"Sisi tumejiandaa vizuri na kikubwa kilichozidisha morali ni jinsi ambavyo Serikali yetu ikiongozwa na Rais John Magufuli na Waziri Mwakyembe pamoja na Watanzania kwa ujumla walivyorudisha imani kwetu na sasa ni kazi kwetu kuwapa raha,"alisema Banda ambaye hivi karibuni alifunga ndoa na mkewe, Zabibu Kiba anayeishi naye Afrika Kusini.

Amekizungumzia kikosi cha Cape Verde watakayocheza nayo wiki hii, Banda amesema, wanaiheshimu timu hiyo lakini watapambana na kushinda.

"Mchezo utakuwa mgumu, lakini tutapambana kwa nguvu zote kuleta furaha kwa Watanzania. Tutakuwa ugenini hivyo tutacheza kwa tahadhari kubwa ili tuweze kupata matokeo mazuri,"alifafanua Banda.