Watanaswa kwa pesa nene

Muktasari:

Hii hapa orodha ya masupastaa watano ambao dili zao mwishoni mwa msimu huu kama watanaswa basi zitakuwa za pesa ndefu.

LONDON, ENGLAND.MIEZI miwili imepita tangu dirisha la uhamisho wa Januari lilipofungwa na si muda mrefu dirisha jingine litafunguliwa kuona wachezaji wakihama kutoka timu moja kwenda nyingine.

Dirisha lijalo la majira ya kiangazi linatarajiwa kuwa na mvuto mkubwa sana kutokana na kudaiwa litahusisha masupastaa wa maana ambao bila ya shaka ada zao za uhamisho zitakuwa zimechangamka si chini ya Pauni 100 milioni. Orodha ya mastaa wa maana wanaotajwa watahama mwishoni mwa msimu huu ni ndefu na baadhi yao ni Toni Kroos, Kalidou Koulibaly na Gareth Bale.

Hii hapa orodha ya masupastaa watano ambao dili zao mwishoni mwa msimu huu kama watanaswa basi zitakuwa za pesa ndefu.

Eden Hazard (Chelsea kwenda Real Madrid)

Kurudi kwa Zinedine Zidane huko Real Madrid kumechochea kwa kiasi kikubwa usajili wa Eden Hazard kwenda kwenye kikosi hicho cha Bernabeu. Hazard shujaa wake ni Zidane na ndio maana anataka kwenda kucheza chini yake huko Bernabeu.

Hali ilivyo Hazard haonekani kuwa na mpango wa kuendelea kubaki Stamford Bridge baada ya msimu huu kufika mwishoni kwa sababu kuna kila dalili timu hiyo ikashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Licha ya kwamba mkataba wa staa huyo utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao, haiwezekani kunaswa kwa pesa ndogo.

Christian Eriksen (Spurs kwenda Madrid)

Si kitu cha kificho kuwa Real Madrid imeanza kujisuka upya kwenye dirisha lijalo la usajili na ndio maana inahusishwa na mastaa watupu. Msimu huu hadi sasa imeachwa nyuma kwa pointi 12 na vinara Barcelona huko La Liga na imetupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ajax.

Kwenye mipango yake, Real Madrid inamsaka pia kiungo Christian Eriksen, ambaye mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao. Kama asipokubali kusaini dili jipya, basi Spurs itamuuza lakini haitakuwa kwa pesa kiduchu.

Antoine Griezmann (Atletico kwenda Man United)

Manchester United kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa na mpango wa kutaka kumsajili staa wa Ufaransa na Atletico Madrid, Antoine Griezmann. Ilitaka kumnasa mwaka 2017, lakini dili liliharibika kwa sababu Atletico ilifungiwa kusajili, hivyo ilikuwa vigumu Griezmann kuondoka kwa sababu isingekuwa rahisi kupata mtu wa kuziba pengo lake.

Lakini, dili hilo linaweza kutokea dirisha lijalo la usajili baada ya staa huyo kuwa tayari kuondoka Atletico huku Barcelona na PSG zikimtaka. Pia anaweza kwenda Old Trafford, lakini si kwa dau la kitoto.

Paulo Dybala (Juventus kwenda Liverpool)

Staa wa Kiargentina, Paulo Dybala mambo yake si mazuri huko Juventus na ndio maana kumekuwa na mpango wa kuachana na timu hiyo kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ameshtukia jambo hilo na ameonyesha dhamira ya dhati ya kumtaka Dybala. Juventus inataka kumtikisa Klopp kwa kumwambia kwamba wabadilishane na Mohamed Salah. Vyovyote inavyokuwa Klopp mpango wake ni kumnasa Dybala, lakini dili hilo haliwezi kuwa la kitoto.

Philippe Coutinho (Barca kwenda PSG)

Hana muda mrefu sana kwenye kikosi cha Bercalona, lakini kwa sasa linapotajwa jina lake, basi linamhusishwa na mpango wa kuondoka kwenye kikosi hicho. Manchester United inatajwa sana kwenye mpango wa kumsajili kiungo huyo wa Kibrazili, ambaye Januari mwaka jana tu hapo Barcelona ililipa Pauni 142 milioni kupata huduma yake.

Coutinho maisha yake si mazuri Barca na ndio maana timu nyingi zinamhitaji. Kama dili la Man United likishindwa, basi mabingwa wa Ufaransa, PSG wameonyesha dhamira ya dhati kuinasa saini yake na huenda akanaswa dirisha hili lijalo la majira ya kiangazi.