Wataalam wafunguka hasira za Yanga

WAKATI vitendo vya vurugu vinavyofanywa na mashabiki wa Yanga dhidi ya wenzao wa Simba vikikemewa vikali, wanasaikolojia wametoa kauli juu ya matukio hayo.

Juzi Jumapili, Yanga ikicheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja Jamhuri mjini Morogoro, mashabiki wa Yanga walionekana wakimshambulia shabiki wa aliyevalia jezi ya Simba baada ya kupita kwenye jukwaa lao.

Kitendo hicho, kiliwafanya Polisi kuingilia ili kutuliza vurugu hizo huku uongozi wa Yanga jana Jumatatu ukitoa tamko la kukemea vikali vitendo hivyo vinavyofanywa na mashabiki wao.

Wanasaikolojia waliizungumzia video iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha mashabiki hao wakiwafanyia vurugu wenzao, walidai baadhi ya mashabiki wa Yanga wana matatizo ya kisaikolojia ambayo yanawasukuma kufanya vitendo hivyo ambavyo vinatakiwa kukemewa kwa haraka ili visije kuleta maafa makubwa.

Charles Nduku, ambaye ni mwanasaikolojia alisema, ameona vurugu hizo na kubaini kuwa inatokana na kuaminishwa vitu vikubwa tofauti na uhalisia.

Alisema Wanayanga wameaminishwa vitu vikubwa na wana matarajio makubwa juu ya timu yao tofauti na wanachokiona wanapokwenda uwanjani bado hakijakidhi haja zao kulinganisha na Simba wanachoaminishwa.

“Matumaini ya Wanayanga na kinachotokea ni vitu viwili tofauti na kilichopo katika akili zao na kinachotokea hakiendani, hivyo vitendo ni kutokana na wao kujiona wadogo na wanawaona Simba wakubwa basi na wao wanatamani kuwa kama Simba,” alisema mtaalam huyo.

Kwa upande wa Karoli Mabula alisema; “Mara nyingi mtu unapokuwa na matarajio makubwa yaliyopitiliza kiwango halafu yakawa hayaonekani inakuwa shida, sio katika mpira tu hata kwenye maisha ya kawaida.”

KAULI YA UONGOZI

Uongozi wa Yanga kupitia Kaim Katibu wake Wakili Patrick Simon umelaani na kukemea vikali kitendo hicho na kuviomba vyombo vya sheria kuwachukulia hatua endapo itawabaini waliofanya vitendo hivyo.