Washindi wa Mchongo wa Mwanaspoti wapewa chao

Muktasari:

Mmoja wa washindi hao, Anyimike alisema yeye ni msomaji mzuri wa gazeti la Mwanaspoti na amekuwa akifuatilia mashindano mbalimbali yanayochezeshwa na gazeti hilo hata hivyo hakuamini kama angeshinda kiasi hicho cha fedha.

MOROGORO. MTUMISHI wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Japhet Anyimike na mfanyabishara ndogondogo ‘machinga' Samwel Petro wamekabidhiwa kitita chao cha Sh 100,000 kila mmoja baada ya kuibuka washindi wa shindano la Mchongo na Mwanaspoti wiki iliyopita.

Shindano hilo ambalo litachezeshwa kwa miezi mitatu washindi watatu kutoka mkoa wa Morogoro akiwemo muuza genge huko Kihonda Manispaa ya Morogoro, Ursula Mohamed naye alijinyakulia kiasi hicho cha fedha.

Mmoja wa washindi hao, Anyimike alisema yeye ni msomaji mzuri wa gazeti la Mwanaspoti na amekuwa akifuatilia mashindano mbalimbali yanayochezeshwa na gazeti hilo hata hivyo hakuamini kama angeshinda kiasi hicho cha fedha.

Alisema kushinda huko kumempa chachu na hamasa ya kuendelea kucheza huku akiamini kwamba ipo siku ataibuka mshindi na kujinyakulia bodaboda ambayo nayo inatolewa kupitia shindano hilo.

Naye Samweli Petro alisema kiasi hicho cha fedha alichoshinda kitamsaidia kuongeza mtaji katika shughuli zake za ujasiliamali na pia aliahidi kuendelea kucheza shindano hilo.

Akieleza namna ya kucheza shindano hilo Meneja Mauzo wa Kampuni ya magazeti ya Mwananchi mkoa wa Morogoro, Aziz Msuya alisema kushiriki ni rahisi kwani msomaji  wa gazeti la Mwanaspoti anatakiwa kujaza kuponi iliyopo kwenye gazeti hilo na kuikata kisha kuipeleka ofisi ya Mwananchi au kumkabidhi muuzaji wa magazeti ya Kampuni hiyo.

Wakati umebaki mwezi mmoja shindano hilo kumalizika Msuya aliwahamasisha wasomaji wa gazeti la Mwanaspoti kushiriki kucheza shindano hilo ili kujinyakulia zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu, simu janja pamoja na bodaboda.