Washambuliaji 10 wazawa waliotikisa Ligi Kuu

Muktasari:

  • Hata hivyo ni nyota wa nje ndio waliotawala zaidi kuzifumania nyavu msimu huu

Dar es Salaam.Kwa msimu wa pili mfululizo washambuliaji wa kigeni wameendelea kutikisa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya Meddie Kagere kutwaa tuzo ya mfungaji bora.

Kagere, raia wa Rwanda amefuata nyayo za Mganda Emmanuel Okwi ambaye alitwaa tuzo hiyo msimu uliopita.

Kabla ya Okwi, msimu wa 2016/2017 washambuliaji wazawa walitikisa baada ya Saimon Msuva aliyekuwa Yanga na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting waliibuka wafungaji bora kwa pamoja baada ya kufunga mabao 14 kila mmoja.

Pamoja na Kagere kuibuka mfungaji bora msimu huu, baada ya kufunga mabao 23 akifuatiwa na Heritier Makambo raia wa DR Congo wa Yanga aliyefunga 17.

Hata hivyo, wapo washambuliaji wazawa ambao wamempa ushindani mkubwa Kagere na hapana shaka kasi ya nyota hao ilikuwa chachu kwake ya kufunga idadi hiyo ya mabao na kuibuka mfungaji bora.

Nyota 10 wazawa waliotikisa msimu uliomalizika wa ligi ingawa hawakumpiku Kagere.

1.  John Bocco-Simba

Inawezekana ni majeraha ambayo alikuwa akiyapata nyakati fulani ndio yalimgharimu hadi akashindwa kuibuka mfungaji bora, lakini pamoja na hilo, amepambana kusaka zawadi ya kuwa mchezaji aliyefumania nyavu mara nyingi. Msimu huu ameifungia Simba mabao 16.

2. Salum Aiyee - Mwadui FC

Wakati msimu unaanza, wengi walimtegemea mshambuliaji Charles Ilanfya angekuwa kinara wa mabao ndani ya kikosi cha Mwadui, lakini aliamua kutimkia KMC. Ghafla akaibuka Salum Aiyee ambaye amefanya kazi kubwa ya kuibeba Mwadui msimu huu na amempa Kagere ushindani mkali katika vita ya ufungaji bora na ameshika nafasi ya pili akiwa na mabao 17.

3. Said Dilunga  - Ruvu Shooting

Ameonyesha uwezo mkubwa msimu huu na kugeuka mwiba mkali kwa mabeki wa timu pinzani ambao wamekuwa wakipata taabu wanapotaka kumdhibiti kwa kuwa anajua kukaa katika naafsi sahihi ndani ya eneo la hatari ukiongeza na uwezo wake wa kufunga mabao na haikushangaza kumaliza Ligi Kuu akiwa na mabao 10.

4.Adam Adam - Prisons

Hakuwa akipata nafasi katika kikosi cha African Lyon, hivyo akaamua kutimkia Prisons ambako walimpa fursa ya kucheza na kwa kiasi kikubwa wamenufaika naye, kwani tangu aliposajiliwa wakati wa dirisha dogo hadi sasa amefunga mabao 10.

5.Dickson Ambundo - Alliance

Ana kasi, akili, uwezo wa kumiliki mpira, kupiga pasi na kufunga mabao ambayo yamekuwa msaada kwa Alliance iliyoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu msimu huu na kwa kudhihirisha hilo, amefunga mabao 12.

6.Habib Kiyombo-Singida United

Ni mmoja wa nyota waliotabiriwa kufanya vizuri msimu huu baada ya kutamba msimu uliopita akiwa na Mbao FC, lakini majeraha ya hapa na pale pamoja na changamoto za kiuchumi katika kikosi cha Singida United zimemyumbisha lakini hata hivyo amepambana na kupachika mabao 11.

7. Eliud Ambokile - Mbeya City

Hajacheza katika mzunguko wa pili kwani aliachana na Mbeya City na kujiunga na timu ya Black Leopards ya Afrika Kusini, lakini katika mzunguko wa kwanza alifunga mabao 10.

8.Ayoub Lyanga-Coastal Union

Ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kumiliki mpira na akili ya kukaa katika nafasi inayochagizwa na utulivu alionao anapokaribia lango la timu pinzani.

Lyanga amekuwa tegemeo la Coastal Union ambayo ameifungia mabao 11 katika Ligi Kuu msimu huu.

9. Idd Selemani ‘Nado’  - Mbeya City

Mbeya City ilimnasa baada ya kumuona katika mashindano ya soka kwa timu za mitaani ya Sports Extra Ndondo Cup,Dar es Salaam na tangu aliposajiliwa amekuwa tegemeo la timu hiyo ambayo amefunga mabao 10 msimu huu.

10. Said Khamis  - Mbao

Mabadiliko ya benchi la ufundi ambayo Mbao iliyafanya katikati mwa msimu yalimrudisha nyuma katika mbio za kuwania ufungaji bora baada ya kujikuta akibadilishwa kutoka kucheza kama mshambuliaji wa kati na kuchezeshwa pembeni lakini hata hivyo amepachika mabao tisa msimu huu.