Warembo wa Zanzibar wanavyodatisha Cecafa

Muktasari:

Sasa gazeti hili linakuletea mpango mzima safari ya kikosi cha Zanzibar hadi wanashiriki mashindano hayo.

IJUMAA iliyopita walikutana Uwanja wa Amaan Karume, Kisiwani Zanzibar, wakapanga mikakati yao kisha wakaenda bandarini kupanda boti hadi Dar es Salaam wakaanza michuano ya Cecafa ya wanawake.

Hicho ni kikosi cha Zanzibar ambacho mbali na burudani ya soka, kimekuwa gumzo na mvuto wa aina yake kwa mashabiki wa soka wanaoshuhudia michuano ya Cecafa wanawake inayoendelea kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Cecafa Tanzania 2019 ni michuano inayoshirikisha timu za mataifa manane wanachama kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ambapo Kundi A wapo Zanzibar, wenyeji Tanzania Bara, Burundi na Sudan Kusini. Kundi B, lina Ethiopia, Kenya, Uganda na Djibouti.

Zanzibar bwana inaelezwa kuwa na wachezaji warembo na wanaovutiwa kwelikweli, jambo lililosababisha kupata mashabiki wengi ambao wengi wao sio tu wanafurahia soka lao tu, bali pia ni pale wanapowaona wanapambana uwanjani.

Achana na uwanjani, kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za wadau wa soka gumzo ni wanawake hao warembo wa Zanzibar. Uzuri wao unaelezwa ni maumbo ya kuvutia yaliyojazia vizuri, rangi za miili yao wakiwamo weupe na weusi.

Msimamizi wa timu, Rachael Palangyo anathibitisha kupokea simu za wadau mbalimbali wakimshawishi japo wapate mawasiliano ya wachezaji hao wapate kuzungumza yao, lakini hajathubutu kufanya hivyo, akisema huwa anabaki anacheka tu.

Wachezaji wanaowapagawisha zaidi mashabiki kutokana na mvuto wao ni kiungo, Hafidha Juma Ally ambaye anavaa jezi namba saba na mshambuliaji, Riziki Abbakar Islah anayevaa jezi namba 10.

Sasa gazeti hili linakuletea mpango mzima safari ya kikosi cha Zanzibar hadi wanashiriki mashindano hayo.

JAMANI KUNA WAKE ZA WATU

Kocha mlezi wa timu hiyo, Hatma Mwalim Hamis pamoja na Kocha Mkuu, Mohammed Salah ‘Rishard’ kwa pamoja wanaweka sawa kuwa kikosi chao kina wachezaji walioolewa na wengine hawajaolewa.

“Kitu kikubwa ambacho tunakifurahia kwa walio na waume, wamewaruhusu kwa moyo mmoja kwa sababu wanajua hiyo ni kazi kama zilivyo nyingine na wanatupa ushirikiano,” anasema Mwalimu.

Mwalimu anawataja wachezaji anaojua wameolewa ni pamoja na Riziki, Sabahi Hashim Yusuf, Neema Machano Othman, Hajra Abdallah Ali, Zena Yunus Mohammed na Ipsamu Salum Yusuf.

Anasema, sehemu kubwa ya wachezaji hao ni wafanyabiashara ndogo ndogo: “Wanajishughulisha na kazi tofauti lakini wengi wao ni wafanyabiashara ndogo ndogo kama nguo, chakula na juisi.

HAWAKUKAA KAMBINI KISA UKATA

Salah anasema, alipata wachezaji hao kutokana na mechi za kirafiki kwa sababu hakuna ligi inayochezwa kwao.

“Wana klabu zao, Zanzibar kuna timu kama tano ambazo zinafanya mazoezi na kucheza mechi za kirafiki tu na ndipo nilipowapata wachezaji hawa,” anasema Salah na kuzitaja klabu hizo ni New Generation, Women Fighters, Jumbi, Green Queens na Bungi Sisters.

Anasema, alichagua wachezaji 45 na wakafanya mazoezi kwa wiki mbili, wanakutana Uwanja wa Aman asubuhi wanafanya mazoezi na kurudi nyumbani kwao hadi ilipofika siku ya safari ya kuja Dar es Salaam kwa ajili ya mashindano ya Cecafa.

Wachezaji 45, alifanya mchujo kwa kuwatoa watano kila baada ya muda hadi wakafikia 20, ambao amesafiri nao kuja Dar es Salaam.

“Mchujo huo mbali na mazoezi yetu ya kawaida, tulicheza mechi za kirafiki na timu za wanaume kuona tunapata mazoezi na wachezaji tunaowataka,“ anasema Salah na kuzitaja timu tatu walizocheza nazo ni ZPEC ambayo ni U-20 ya Zanzibar, Jang’ombe Boys na Black Fela.

“Hatukuwa na kambi kama mastaa sisi, tulikutana tukitokea nyumbani na kufanya mazoezi kisha nyumbani lakini si kama tulikuwa tunapenda ni ukata tu,” anasema Salah ambaye Zanzibar anafundisha Klabu ya Jang’ombe Boys.

“Tulitaka kujiandaa vizuri kama ambavyo timu nyingine zinafanya lakini hatukuwa na pesa lakini kwa sababu wote tulikuwa na malengo, hatukujali hilo,” anaeleza Salah.

WACHEKELEA KAMBI YA DAR ES SALAAM, UROJO KAMA KAWAIDA

Salah anasema, tangu wafike wamepata mapokezi mazuri na wanaishi katika hoteli nzuri na kupata kila kitu.

“Kweli maisha yetu hapa Dar es Salaam ni mazuri kweli kweli, tunalala pazuri, chakula kizuri na huduma zote tunapata,” anasema Salah.

Akafafanua chakula cha urojo ambacho ni maarufu sana Kisiwani Zanzibar hakipikwi ndani ya hoteli, lakini nje ya hoteli kama hatua tano za miguu kuna jamaa anauza, wanapohitaji ni kiasi cha kwenda hapo na kujihudumia kwa kiasi wanachotaka.

MAVAZI KWENYE MECHI

Kama inavyozoeleka mavazi wanayotumia wachezaji wote ni bukta na tisheti jambo ambalo kwa wanawake wa Zanzibar huwezi kumkuta amevaa hivyo, huwa wanafunika vichwa kwa vitambaa, hijabu na shungi na magauni makubwa kama baibui, dela na juba.

“Kweli kwetu ni changamoto kutokana na mazingira, imekuwa hivyo kwa sababu hatukuwa na maandalizi lakini tumejifunza na tunafanyia kazi,” anasema Salah.

Amefafanua, pamoja na wachezaji wao kuvaa bukta na kutofunika vichwa vyao, wenyeji wa Zanzibar wamekuwa waelewa kwa sababu wanajua vijana wao wako kwenye michezo na kazi.

SHEPU YAZUA UTATA

Kiungo wa Zanzibar, Hafidja Juma Ali, hakucheza mechi ya jana Jumatatu dhidi ya Sudan Kusini kwa sababu jezi ambazo timu hiyo imezivaa, zilikuwa zinambana na kumwonyesha maumbile yake kama alivyo.

Hafidja ni Yule mchezaji ambaye amekuwa akiwarusha roho sehemu kubwa ya mashabiki kutokana na namna alivyoumbwa.

Aliyeweka wazi jambo hilo ni Kocha Mkuu wa Zanzibar, Salah lakini akasisitiza mchezo ujao dhidi ya Tanzania atakuwepo uwanjani.

“Jezi zijazo ni kubwa kidogo tofauti na tilizotumia leo, zimekuwa hazimpi uhuru wa kucheza kwa sababu zinambana na kumwonyesha maumbile yake, “ alisema Salah.

Alisema, hiyo imesababisha mashabiki wapige kelele kumshangilia na kumpigia kelele nyingi kutokana na namna alivuoumbika.

MASHINDANO MAGUMU

“Timu zimejiandaa kweli kweli ingawa ujio wetu ni kushindana na kujifunza zaidi ili wakati mwingine tufanye kitu kizuri zaidi,” anasema Salah.

Zanzibar ni mabingwa mara moja wa mashindano hayo wakichukua taji mwaka 1986 kabla ya mashindano hayo kusimama kwa takriban miaka 30.

Kwenye michuano ya 2016 iliyofanyika Uganda, waliondolewa hatua ya makundi wakiwa wamechapwa idadi kubwa ya mabao ambayo ni 30 wao wakipata moja. Katika michuano ya mwaka huu kama wameimarika kidogo.