Wapinzani wa Simba robo fainali

Muktasari:

Droo ya hatua ya robo fainali ya mashindano hayo imepangwa kufanyika kesho Jumatano, Machi 20 jijini Cairo ambapo kiutaratibu timu nne zilizoongoza makundi zitapangwa kucheza dhidi ya timu zilizoshika nafasi ya pili.

 SIMBA imeweka rekodi mpya baada ya kuwa timu ya kwanza kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu utaratibu wa mashindano hayo ulivyobadilishwa mwaka 2017.

Ushindi wa mabao 2-1 ilioupata dhidi ya AS Vita Club kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwenye Uwanja wa Taifa juzi, umeifanya ifikishe pointi 9 ambazo zimeiweka kwenye nafasi ya pili nyuma ya Al Ahly yenye 10 na kupelekea zote mbili zifuzu robo fainali huku JS Saoura na Vita zikitupwa nje ya mashindano.

Ukiondoa Simba na Al Ahly ambazo zimefuzu hatua ya robo fainali kutokea Kundi D, timu nyingine sita ambazo zimepenya ni pamoja na Wydad Casablanca na Mamelodi Sundowns zilizokuwa kundi A, Esperance na Horoya za kundi B pamoja na TP Mazembe na CS Constantine ambazo zinatokea Kundi C.

 Droo ya hatua ya robo fainali ya mashindano hayo imepangwa kufanyika kesho Jumatano, Machi 20 jijini Cairo ambapo kiutaratibu timu nne zilizoongoza makundi zitapangwa kucheza dhidi ya timu zilizoshika nafasi ya pili.

 

Kwa maana hiyo timu za Wydad Casablanca, TP Mazembe, Al Ahly na Esperance zitawekwa katika chungu cha kwanza na Simba, Constantine, Mamelodi na Horoya zitakuwa chungu cha pili.

Hata hivyo hakuna uwezekano wa Simba kupangwa na Al Ahly kwenye robo fainali kwa sababu walikuwa kundi moja na hivyo wawakilishi hao wa Tanzania wanaweza kukutana na timu mojawapo kati ya Esperance, Wydad Casablanca au TP Mazembe. Timu hizo tatu kila moja ina uimara na udhaifu wake ambao kama Simba itafanyia kazi iwapo itapangwa na mojawapo, kuna uwezekano mkubwa ikapenya kuingia nusu fainali.

Esperance Ni mabingwa watetezi wa taji hilo ambalo walilitwaa msimu uliopita baada ya kuichapa Al Ahly kwa ushindi ushindi wa jumla wa mabao 4-3 ikipoteza kwa mabao 3-1 ugenini kabla ya kushinda mabao 3-0 nyumbani.

 Ni timu ambayo hucheza kwa kasi katika kipindi cha pili hasa katika dakika 10 za mwisho za mchezo muda ambao ndio wamekuwa wakifunga idadi kubwa ya mabao na kwa kulidhihirisha hilo, katika mabao tisa iliyofunga kwenye hatua ya makundi, matano wameyapata kipindi cha pili na kati ya hayo, manne walifunga katika dakika ya kuanzia 85 hadi zile za nyongeza baada ya dakika 90 kukamilika.

Wamekuwa hawatoi presha kubwa kwa wapinzani kipindi cha kwanza hivyo kama Simba watajipanga vyema na kukitumia kisha kuwa makini kipindi cha pili, wanaweza kuwatoa ikiwa watapangwa kukutana nao robo fainali.

Wydad Casablanca-Morocco Silaha kubwa ya Wydad Casablanca ni uwanja wao wa nyumbani ambao wamekuwa wakiutumia vyema kupata matokeo ambayo yamekuwa yakiwavusha kwenda hatua zinazofuata lakini wamekuwa hawatishi sana ugenini.

 Ni timu yenye washambuliaji wanaojua vyema kutumia nafasi pindi wanapokuwa jirani na lango la timu pinzani lakini udhaifu mkubwa unaoweza kuibeba Simba ikiwa watakutana ni ubovu wa safu yao ya ulinzi ambayo imekuwa ikiruhusu mabao pindi inapokutana na timu yenye washambuliaji wasumbufu.

 Na katika kulidhihirisha hilo, kwenye hatua ya makundi licha ya kufunga mabao manane, safu yake ya ulinzi imeruhusu mabao sita.

TP Mazembe Ikiwa watapangwa kukutana, haitokuwa mara ya kwanza kwani kabla ya hapo walishawahi kukutana mwaka 2011 kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na Simba ikatolewa kwa kipigo cha jumla cha mabao 6-3 lakini baadaye Mazembe waliadhibiwa na kutupwa nje kwa kumchezesha mchezaji ambaye hakuwa halali.

Uimara wa Mazembe ambao Simba watapaswa kuhakikisha hauwatesi iwapo watakutana ni miguu ya kiungo mshambuliaji, mkongwe Tresor Mputu ambaye ndiye mpishi wa mabao ya timu hiyo lakini ndiye ameiweka mgongoni kwa sasa.

Mputu katika mabao 13 ambayo Mazembe imefunga kwenye makundi, amehusika katika mabao nane akifunga manne na kupiga pasi nne za mabao. Pia wana mshambuliaji Elia Meschak ambaye ndiye amekuwa akitumia vyema pasi za Mputu kufunga mabao.

 Hata hivyo udhaifu wa TP Mazembe ni kutokuwa na kasi pindi wanapokuwa ugenini jambo linaloweza kuibeba Simba nyumbani iwapo watapangwa pamoja.