Waondoke tu

Monday February 11 2019

 

LONDON, ENGLAND.KUNA wanasoka hao wamekuwa maarufu kwelikweli kwenye klabu zao na wamekuwa ghali kutokana na vipaji walivyonavyo na viwango vyao wanavyovionyesha katika mechi za kila siku.

Lakini, baadhi ya mastaa hao wamejikuta wakiwa kwenye uhusiano mbaya na makocha wao na wengine wakishuka viwango vyao kiasi cha kuwafanya kutofurahia sana maisha kwenye timu zao wanazocheza kwa sasa.

Kitu kinachovutia ni kwamba wachezaji hao si kama wamekwisha kabisa viwango vyao, isipokuwa pengine ni upepo tu hauendi sawa kwenye timu walizopo kwa sasa na kwamba wanaweza kutoboa na kurudi kwenye makali yao kama wataamua kubadili timu kwa kuondoka katika klabu walizopo kwa sasa na kwenda kusaka maisha kwingineko.

Hawa hapa masupastaa watano ambao wakiondoka kwenye timu zao za sasa na kwenda kwingineko hakuna atakayeshangazwa na jambo hilo. Waondoke tu.

5.Philippe Coutinho

Philippe Coutinho amejiunga na Barcelona Januari ya mwaka jana tu hapo, lakini mambo yake hayaonekani kwenda sawa katika kikosi hicho cha Nou Camp.

Licha ya kwamba wachezaji wenzake wamekuwa wakimsapoti na kocha akiamini anaweza kubadilika, lakini Mbrazili huyo amejikuta nje ya kikosi mara kadhaa na sasa anapata nafasi kwa sababu tu Ousmane Dembele ni majeruhi.

Mabosi wa klabu hiyo wamekuwa wakipiga hesabu za kumpiga bei kama atashindwa kupandisha kiwango chake na bila ya shaka jambo hilo linamfanya Coutinho kucheza kwa presha kubwa huko Nou Camp. Kama mambo yataendelea kuwa hivyo, Coutinho ni vyema tu akitafuta timu nyingine ya kwenda.

4.Romelu Lukaku

Romelu Lukaku alianza maisha yake Manchester United msimu uliopita vizuri sana ambapo alifunga mabao 27 katika michuano yote akisaidia timu yake kupata hadhi yake licha ya kwamba ilishindwa kubeba mataji.

Lakini, baada ya Kombe la Dunia 2018, Lukaku ameshuka kiwango chake, hayupo tena kwenye ule ubora wake na hafungi tena mambo kama ilivyokuwa misimu iliyopita.

Kutokana na timu hiyo kukabiliwa na majanga mengi msimu huu, mashabiki wameanza kumtolea macho Lukaku na kumwaona kwamba si mchezaji wa kumtegemea kutokana na kushindwa kufunga mabao wakati yeye ni mshambuliaji wa kati na hiyo ndiyo kazi yake.

Jambo hilo limemfanya hata kocha wa muda kwenye kikosi hicho, Ole Gunnar Solskjaer kumwaamini zaidi straika Marcus Rashford na kumpa nafasi ya kuanza mara nyingi mbele ya Mbelgiji huyo. Akiondoka, hakuna shabiki wa Man United atakayeteseka.

3.Jerome Boateng

Jerome Boateng amekuwa akisumbuliwa sana na matatizo ya majeruhi ya mara kwa mara kwa misimu ya karibuni, lakini hilo halijawahi kuwa tatizo katika msimu huu.

Hata hivyo, Boateng amejikuta kwenye wakati mgumu kutokana na kushindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza ambapo kocha wa sasa wa Bayern Munich, Niko Kovac anapendelea zaidi kuitumia kombinesheni ya Mats Hummels na Niklas Sule kwenye safu ya mabeki wa kati. Jambo hilo linamsukuma Boateng kufikiria kubadilisha timu mwishoni mwa msimu ili kwenda kupata nafasi ya kucheza na si kama maisha yake yalivyo kwa sasa huko kwenye kikosi cha Allianz Arena.

Shida nyingine ni kwamba Bayern Munich mpango wao ni kufanya usajili mwishoni mwa msimu na jambo hilo linamfanya Boateng kutokuwa na chaguo jingine zaidi ya kwenda kutafuta maisha kwingineko tu.

2.Alexis Sanchez

Staa mwingine wa Manchester United mwenye shida ya kiwango chake ni Alexis Sanchez. Fowadi huyo wa kimataifa wa Chile alijiunga na Man United akitokea Arsenal Januari mwaka jana, lakini tangu atue Old Trafford ubora wa kiwango chake umekuwa si kama vile zamani.

Baada ya kupambana na hali yake kuhusu ufiti wa uwanjani, staa huyo alijikuta akiwa nje ya uwanja wakati timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Jose Mourinho. Kwa sasa Sanchez anajaribu kufurukuta kutafuta nafasi chini ya kocha mpya Ole Gunnar Solskjaer.

Lakini, shida inakuja sehemu moja tu, Anthony Martial yupo kwenye ubora mkubwa sana kwa sasa na jambo hilo linamfanya Sanchez asiwe na chaguo jingine zaidi ya kusubiri tu kwenye benchi kwa sababu anapopata nafasi bado ameshindwa kuonyesha ule ubora wake.

Mpango wa Man United ni kusajili winga mwingine mwisho wa msimu, wakimsaka Douglas Costa na kama dili hilo likifanyika basi hadi Sanchez hatakuwa na namna nyingine zaidi ya kutafuta mlango wa kutokea tu.

1.Mesut Ozil

Chini ya kocha Arsene Wenger, Mesut Ozil alikuwa mchezaji mwenye uhakika wa kupata nafasi katika kikosi cha Arsenal. Piga ua, asingekosekana kwenye kikosi cha wababe hao wa Emirates.

Lakini, chini ya kocha wa sasa, Unai Emery, Mjerumani huyo amekuwa akisugua benchi na kuweka benchi katika mechi zote kubwa.

Ozil wa sasa anapangwa kwenye zile mechi ambazo timu ina uhakika wa kushinda, lakini zile zenye utata, Emery hampangi kabisa kikosini na amekuwa akiona bora Aaron Ramsey au Alex Iwobi.

Ukweli upo wazi kwamba Emery ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho hadi msimu ujao na kwa jambo hilo ina maana suala la Ozil kukaa kwenye benchi kitakuwa ni kitu kitakachoendelea. Kuepusha kupoteza kipaji chake pamoja na kuwaingiza hasara Arsenal kutokana na kumlipa Pauni 350,000 kwa wiki, basi ni vyema tu akatafuta mlango wa kutokea na kwenda kutafuta maisha kwingineko ambako atapewa nafasi ya kucheza kuliko kusugua tu benchi huko Emirates.

Advertisement