Waogeleaji kuiwakilisha mashindano ya Dunia China

Thursday December 6 2018

 

By Na Majuto Omary

Dar es Salaam. Waogeleaji wanne wa Tanzania watashindana katika mashindano ya dunia ya kuogelea yaliyopangwa kufanyika mjini , China kuanzia Desemba 11 mpaka 16 eneo la Hangzhou Olympic and International Expo Center.

Waogeleaji hao ni Kalya Temba na Celina Itatiro kwa upande wa wanawake huku, Collins Saliboko na Hilal Hilal watawakilisha upande wa wanaume.Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Kuogelea nchini (TSA) Asmah Hilal alisema jana kuwa waogeleaji hao watakuwa chini ya kocha, Alexander Mwaipasi na Mwenyekiti wa chama chao, Imani Dominick.

Asmah alisema kuwa waogeaji wa kike, Kayla na Celina wameondoka jana usiku wakati Collins ataungana na wenzake mjini Hangzhou akitokea Uingereza huku Hilal ambaye ndiye nahodha wa timu hiyo ataondokea Dubai.

Alisema kuwa waogeleaji hao wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano hayo ambayo pia yataambatana na mkutano mkuu wa Shirikisho la Mchezo wa kuogelea duniani (Fina) na kozi ya makocha, Mkutano Mkuu wa Fina na kozi ya makocha utaanza Jumamosi.“Tunawashukuru wazazi kwa kuingia gharama kwa waogeleaji wetu na kufanikisha ushiriki wao, ni matarajio yetu kuwa watafanya vizuri pamoja na changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo, mashindano yatakuwa magumu kwani waogeleaji nyota wa Dunia nao watakuwepo,” alisema Asmah.

Alisema kuwa TSA imeingia madarakani hivi karibuni na kwa muda wote wamekuwa wakiangaika hapa na kule kuhakikisha waogeleaji wetu wanashindana katika mashindano makubwa na muhimu kwa maendeleo ya mchezo.“Hakuna haja ya kutoa sababu ya muda kuwa hatushiriki kutokana na muda mfupi wa kukaa madarakani, tuliomba kazi ya kuiendeleza mchezo na tunatakiwa kufanya ili kutimiza wajibu wetu, tunaomba wadhamini watuunge mkono,” alisema.Katibu Mkuu wa TSA, Inviolata Itatiro alifafanua kuwa mashindano hayo ya 14 yatafanyika kwenye bwawa la kuogelea la mita 25 ambalo ni la kisasa zaidi limejengwa na kampuni ya Italia ya Myrtha Pools na linahamishika. Bwawa hilo la kuogelea limejengwa kwenye uwanja wa tenisi na litaondolewa na kuwekwa eneo la wazi ambalo litatumiwa na jamii.

Advertisement