Wanga alia bodi ya ligi kuchomea picha

Wednesday June 5 2019

 

By Thomas Matiko

Nairobi.STRAIKA wa Kakamega Homeboyz, Allan Wanga kaimwagia machungu yake yote bodi inayoendesha Ligi Kuu nchini KPL, akiishutumu kwa kumsababishia kupoteza kiatu cha dhahabu kilichotwaliwa na Enos Ochieng juzi Jumapili.

Mechi zote za kumaliza msimu ziliratibiwa kuchezwa Jumatano ya wiki iliyopita na baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa kwenye mchuano waliolimwa Kakamega Homeboyz 2-0 na Sofapaka, Wanga aliyeshindwa kupata bao alikuwa mwepesi wa kuwapongeza wapinzani wenzake wakali wa magoli msimu huu Enos Ochieng wa Ulinzi na Umaru Kasumba wa Sofapaka.

Kile hakujua ni mechi ya Ulinzi dhidi ya Mt Kenya ilikuwa imeahirishwa na KPL baada ya timu hizo kuingia uwanjani zikiwa zimevalia jezi za kufanana za rangi nyekundu.  Kutokana na hilo mechi haingeweza kuendelea na hivyo kusukumwa hadi Jumapili.

Hatua hiyo ndiyo imemuumbua Wanga baada ya Ochieng aliyekuwa akimfukuzia kwa karibu sana akiwa na upungufu wa goli moja  kuishia kufunga hat-triki iliyomsaidia kutwaa kiatu cha dhahabu kwa kupachika mabao 20.

Wanga anasisitiza kama mechi hiyo ingechezwa siku moja kwa mujibu wa sheria basi kwa asilimia kubwa yeye ndiye angeishia kumaliza kama mfungaji bora.

“KPL walikosea, hii sio sawa kabisa kwangu sababu Ochieng alijua alichotakiwa kukifanya ili kunizidi magoli. Sina tatizo naye ila hizi sheria za KPL. Kama mechi ingechezwa wakati mmoja na zile zingine jinsi ilivyo utaratibu kote duniani chochote kingeweza kutokea ila hiii hapa ni wazi jamaa alijua atahitaji kujituma kupata bao za kuzidi. Ina uma,” akasema.

Advertisement

Hata hivyo, kocha wa Ulinzi, Benjamin Nyangweso kamtetea Ochieng kwa kusema hakukuwa na uhakika angepachika bao au la hata kama mechi hiyo ingekosa kuahirishwa.

Kulikuwepo pia na malalamishi kwamba, kwa mujibu wa sheria KPL walistahili kuwapa ushindi kwani kando na kuvalia jezi sawia na wenyeji, Mt Kenya walifika uwanjani kuchelewa.

 Hata hivyo wadau wengine wakahoji kuwa hatua hiyo ingemnyima fursa Ochieng huku wengine wakipinga na kusisitiza sheria ingefuatwa.

Advertisement