Wanausikia ubingwa wa ligi kwa wenzao tu

Tuesday February 19 2019

 

LONDON, ENGLAND . MATAJI ndicho kitu kinachoelezwa kuwa ni moja ya sababu za msingi zinazowafanya wachezaji kuhama timu moja kwenda nyingine.

Lakini, unaambiwa hivi, kuwa mchezaji bora hakuna maana ya kwamba utakuwa na uhakika wa kushinda kila kitu na ndio maana supastaa kama Ronaldo wa Brazil, ameshindwa kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hadi anastaafu licha ya kucheza kwenye klabu matata huku akiwa kwenye kiuwango bora.

Hivyo hivyo, kuna orodha ya wachezaji hao unaweza kuwa kwenye wakati mgumu kuamini kwamba, umahiri wao wote hawajawahi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu kwenye maisha yake ya kisoka hadi sasa.

5.Antoine Griezmann

Umri: Miaka 27

Mechi za ligi: 346

Katika msimu wake wa kwanza mzima, Antoine Griezmann alifunga mabao sita katika mechi 39 alizocheza wakati Real Sociedad iliposhinda ubingwa wa Segunda Division na misimu minne baada ya hapo amekuwa akicheza kwenye La Liga. Staa huyo Mfaransa alinaswa na Atletico Madrid baada ya Diego Costa kwenda Chelsea baada ya ubingwa wa La Liga 2013/14. Lakini, tangu Griezmann atue Atletico timu hiyo imemaliza nafasi ya tatu kwenye La Liga mara tatu na msimu uliopita walimaliza nafasi ya pili.

4.Marco Reus

Umri: Miaka 29

Mechi za ligi: 301

Baada ya kushindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza akitokea kwenye timu ya watoto ya Borussia Dortmund, Marco Reus alirudi tena kwenye timu hiyo mwaka 2012 baada ya kwenda huko kuichezea Monchengladbach. Dortmund walitoka kubeba ubingwa wa Bunndesliga kwa misimu miwili mfululizo wakati Reus anarudi kwenye timu hiyo na baada ya hapo, Bayern Munich wanachukua utawala wakibeba tu ubingwa wa ligi kumfanya staa huyo aendelea kusubiri hadi sasa akiwa na matumiani kuna siku anaweza kunyanyua kwapa kushangilia ubingwa.

3.Pierre-Emerick Aubameyang

Umri: Miaka 29

Mechi za ligi: 336

Pierre-Emerick Aubameyang alitumikia misimu yake ya kwanza minne ya soka la kulipwa akiwa kwenye kikosi cha AC Milan, kipindi hicho wababe hao wa Italia wakiwa bado washindani kwenye ligi. Lakini, kwa kipindi hicho alishindwa kucheza mechi hata moja kwenye kikosi cha kwanza na kuamua kutimkia zake Saint-Etienne mwaka 2011. Baada ya hapo akatimkia zake Borussia Dortmund mwaka 2013, hakubeba taji la Bundesliga.

Sasa ametua kwenye kikosi cha Arsenal na haonekani kama atabeba ubingwa wa ligi msimu huu, licha ya kuwa msaada mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji akifunga mabao muhimu kwa Arsenal.

2.Fernando Torres

Umri: Miaka 34

Mechi za ligi: 560

Fernando Torres utashangaa kumwona kwenye orodha hii. Staa huyo kwa umahiri wake wa kufunga kiasi cha kupachikwa jina la El Nino, anaelekea kwenye mwisho wa maisha yake ya soka akiwa hana medali hata moja ya ubingwa wa ligi, licha ya kubeba mataji mengine makubwa kama Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ubingwa wa Ulaya na Kombe la Dunia.

Kwenye klabu, Torres amecheza kwenye vikosi vya Atletico Madrid, Liverpool, Chelsea na hata AC Milan, lakini mambo hayajawahi kuwa mazuri na kubeba ubingwa wa ligi. Aaamini hilo linaweza kwisha huko Japan kwenye kikosi cha Sagan Tosu.

1.Juan Mata

Umri: Miaka 30

Mechi za ligi: 406

Juan Mata alitokea kwenye akademia ya Real Madrid. Baada ya kushindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza, alitimkia zake Valencia ambako alishinda ubingwa wa Copa del Rey katika msimu wake wa kwanza tu huku akiwa bora.

Baada ya kutamba huko Mestalla, Mata akanaswa na Chelsea mwaka 2011 na kwenda kucheza hapo, lakini hakubeba ubingwa wowote wa ligi kabla ya kutimkia Manchester United, ambako pia amepishana tu na mataji hayo ya ligi kwa sababu amekuja Old Trafford wakati Man United ikitokea kubeba ubingwa, kisha alikotoka Chelsea nao walibeba ubingwa.

Advertisement