Wanasoka washkaji wanaotikisa dunia

Muktasari:

Hata hivyo, viungo hao wawili si kundi la kwanza la wanasoka walioamua kuwa marafiki wakubwa kweye mchezo wa soka. Ni hawa ndio baadhi ya wanasoka waliamua kuwa washkaji kwenye soka la dunia.

LONDON,ENGLAND.WOTE ni wanasoka na wameamua kuwa maswahiba. Mason Mount na Declan Rice ni sura mpya ya wanasoka waliamua kuwa marafiki wakubwa, wakati huu wakikutana kwenye timu ya taifa ya England, huku wote wote wakiwa walianzia urafiki wao walipokuwa wadogo huko klabuni Chelsea.

Hata hivyo, viungo hao wawili si kundi la kwanza la wanasoka walioamua kuwa marafiki wakubwa kweye mchezo wa soka. Ni hawa ndio baadhi ya wanasoka waliamua kuwa washkaji kwenye soka la dunia.

Lingard na Rashford

Wameanzisha hadi staili yao tofauti ya kusalimiana, wakishikana mikono kwa kasi sana. Mastaa hao, Jesse Lingard na Marcus Rashford wamekuwa wakiichezea Manchester United na ndiko hasa ulikoanzia urafiki wao kabla ya kukutana pia katika timu ya taifa ya England. Lingard amemzidi Rashford miaka mitano, hivyo anamchukulia kama mdogo wake huko kwenye kikosi cha Man United. Lingard amedai kwamba ndani ya uwanja, anahakikisha kwamba hakuna mtu anayemwonea Rashford, kama alivyomtetea katika mechi ya Manchester derby mwaka 2016.

Lovren na Salah

Beki wa kati Dejan Lovren na mshambuliaji Mohamed Salah, wamekuwa na maelewano mazuri sana ndani na nje ya uwanja. Kwa kifupi, wawili hao ni marafiki wakubwa baada ya kukutana huko Liverpool. Wakati Salah alipotua Liverpool mwaka 2017, wawili hao walizungumza kuhusu ugumu wa mambo na tangu hapo wamekuwa hawaachani. Beki, Lovren alisema kwamba aliona kuna uelewano mzuri baina yake na Mo Salah tangu walipokutana kwa mara ya kwanza huko Anfield na hivyo wamekuwa ni moja ya wanasoka walioamua kuwa marafiki wa kusaidiana mambo ndani na nje ya uwanja.

Alli na Dier

Wakati Dele Alli aliposainishwa na Tottenham Hotspur kutoka MK Dons mwaka 2015, haraka sana alianzisha urafiki na Eric Dier, ambaye pia ndio kwanza alikuwa ametua kwenye kikosi hicho. Eric Dier alikuwa amesajiliwa kutoka Sporting Lisbon ya Ureno na wawili hao kwa haraka walianzisha urafiki na tangu hapo, huwa hawaachani katika mambo yao. Dele Alli amekuwa akisema wazi kwamba amekuwa na urafiki mzuri sana na Dier kitu ambacho wamekuwa wakikionyesha ndani na nje ya uwanja na mambo yanakuwa mazuri zaidi wanapoanzishwa pamoja na kocha Mauricio Pochettino kwenye mechi za Spurs.

Pogba na Lukaku

Kama kusingekuwapo na nguvu ya Paul Pogba, basi kulikuwa na nafasi ndogo sana ya Romelu Lukaku kunaswa na Manchester United. Katika majira ya kiangazi ya mwaka 2017, wakati straika wa Kibelgiji, Lukaku alipokuwa kwenye mtihani wa kuchagua moja, Man United au Chelsea, lakini Pogba, alitumia urafiki wake kumshawishi swahiba wake walipokutana mapumziko huko Los Angeles, Marekani kuja kutua Old Trafford. Wawili hao, Lukaku na Pogba mara kadhaa wamekuwa wakionekana pamoja, wakicheza mpira wa kikapu, hata kutumia ndege moja binafsi kwenye mitoko yao. Ndani na nje ya uwanja wamekuwa na urafiki mkubwa, lakini kwa sasa itabidi wasubiri hadi mwisho wa msimu kuwa pamoja kutokana na Lukaku kuihama Man United na kutimkia huko Inter Milan.

Aubameyang na Lacazette

Pierre-Emerick Aubameyang alisajiliwa na Arsenal, Januari 2018 na kwa haraka sana akatengeneza urafiki na mshambuliaji mwenzake, Alexandre Lacazette. Staa Aubameyang alisema kwamba mara ya kwanza tu alipomwona Lacazette, aliona ni mtu wanayeendana na kuamua kuwa marafiki licha ya kwamba wote wamekuwa wakicheza nafasi ya ushambuliaji. Urafiki wao umeleta mambo matamu ndani ya uwanja, wakitengenezeana nafasi za kufunga kwenye mechi na hivyo kuifanya Arsenal kushinda mechi zake kirahisi. Urafiki wa washambuliaji hao hauishii uwanjani tu, bali wamekuwa wakifanya mambo yao mengine nje ya uwanja na mara nyingi wamekuwa kwenye mitoko ya pamoja.

Mount na Rice

Ilikuwa kwenye akademia ya Chelsea, wakiwa na umri wa miaka kama saba hivi, ndipo Mason Mount na Declan Rice walipoanzisha urafiki wao. Familia zao zilikuwa zikisafiri pamoja na kwenda likizo pamoja, huku wakiwa pamoja kwenye mechi za Chelsea jambo lililowafanya kuwa na urafiki wa karibuni sana. Lakini, Chelsea iliamua kuachana na Rice akiwa na umri wa miaka 14, jambo lililomfanya mama yake Mount kulia sana. Lakini, marafiki hao wa siku nyingi, wamekutana tena wakiwa wakubwa, wakiichezea timu ya taifa ya England baada ya kocha Gareth Southgate kuwajumuisha kwenye kikosi chake. Mount aliweka video kwenye mtandao wa kijamii inayomwonyesha Rice akiwa amelala, wakati walipokuwa mapumzikoni pamoja katika mapumziko ya mwisho wa msimu.

Kolasinac na Ozil

Kwenye Ligi Kuu England kumeshuhudia wanasoka kadhaa waliokuwa maswahiba, wakiwamo pia Sead Kolasinac na Mesut Ozil huko kwenye kikosi cha Arsenal. Wawili hao wamekuwa na urafiki mkubwa wa kusaidiana katika kila hali. Hivi karibuni, Ozil alivamiwa na majambazi wenye visu wakitaka kumpora, lakini Kolasinac aliyekuwa pamoja kwenye gari alishuka na kupambana na majambazi hao kumwokoa swahiba wake. Mwaka 2017, wakati Kolasinac alipohamia Arsenal, Ozil alisema anamchukua na kwenda kuishi kwake na tangu hapo, wawili hao wamekuwa marafiki wakubwa kiasi cha kuwafanya wake zao pia kuwa marafiki.

Messi, Suarez na Fabregas

Hili ni kundi la marafiki ambalo mashabiki wa soka watapenda kuliona likiwa pamoja muda wote. Lionel Messi, Luis Suarez na Cesc Fabregas ni marafiki wakubwa, wakikutana huko Barcelona na tangu hapo wamekuwa wakikutana kwenye mambo mbalimbali, ikiwamo kwenye mitoko yao ya mwisho wa msimu. Mara nyingi, wanasoka hao kinapofika kipindi cha likizo, wamekuwa wakitoka pamoja na hata wake zao, Antonella Roccuzzo (Messi), Sofia Balbi (Suarez) na Daniella Semaan (Fabregas) nao wamekuwa marafiki wakubwa. Mwaka 2017 kwenye mtoko wao huko Ibiza, walipokuwa na familia zao, marafiki hao wamedaiwa kutumia Pauni 32,630 kwenye mlo wa usiku tu, walipokuwa wakila bata kujipongeza kumalizika kwa msimu katika visiwa vya starehe.

Firmino na Coutinho

Muda wao waliokuwa pamoja Anfield ulikuwa mfupi, lakini ulikuwa mtamu zaidi. Wawili hao, ambao ni marafiki wakubwa wote ni Wabrazili, ambapo Roberto Firmino na Philippe Coutinho ukiweka kando kutengeneza kombinesheni nzuri kwenye nafasi ya ushambuliaji, walikuwa na maswahiba wakubwa pia. Lilikuwa pigo kubwa sana kwa Firmino baada ya Coutinho kuhamia zake Barcelona mwaka jana katika dili la uhamisho wa Pauni 142 milioni. Wawili hao wamekuwa na uhusiano mkubwa hata kama hawachezi timu moja na mara nyingi wamekuwa wakiendelea na uhusiano mzuri wanapokutana kwenye timu ya taifa ya Brazil.

Nolan na Carroll

Wakati Andy Carroll alipokumbwa na kesi ya unyanyasaji mwaka 2010 alitegemea msaada mkubwa kutoka kwa swahiba wake, Kevin Nolan. Wawili hao walikuwa marafiki wakubwa walipokutana huko Newcastle United, ambapo Nolan alimwambia Carroll aende kuishi kwake jambo kwa masharti mawili, kwanza kuwasomea kitabu cha hadithi cha Peppa Pig watoto wake na kwenda kulala mapema. Wawili hao wamekuwa na urafiki mzuri sana na wamekuwa hawaachani, kiasi cha Carroll kumtaja Nolan kwenye kikosi chake cha wachezaji watano bora, sambamba na mastaa wengine aliocheza nao Liverpool, Steven Gerrard na Luis Suarez.

Owen na Shearer

Hivi karibuni, Michael Owen amefichua kuwa na bifu na Alan Shearer. Kamwe usimwaamini sana, kwani siku chache baadaye, alimtaja kwenye kikosi chake cha kwanza bora cha mastaa aliowahi kucheza nao timu moja. Owen na Shearer walicheza pamoja Newcastle United na kwenye timu ya taifa ya England, huku kinachodaiwa wawili hao kutibuana kwenye jambo moja tu, Shearer aliona Owen analipwa mshahara mkubwa wakati Owen alimwona Shearer anapendwa sana kwenye kikosi hicho cha St. James’ Park. Suala la kudai kwamba wamekuwa na bifu ni ndogo sana na ukilinganisha uhusiano wao ambao kipindi hicho walipokuwa Newcastle mmoja alipofunga bao, basi walikuwa wakishangilia pamoja, hawaachani.