Wanasimba wasifanye makosa, wawe makini na uchaguzi wao

Thursday September 13 2018

 

KLABU ya Simba inatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu wake, Novemba 3 na kwa sasa zoezi la urudishaji wa fomu kwa wagombea linaendelea kabla ya kufanyika kwa usaili wa kupitisha watakaoenda kuchuana kwenye uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi wa Simba, jumla ya wagombea 21 wamejitokeza, wakiwamo wawili wanaowania Uenyekiti ambayo ni Mtemi Ramadhani na Swedi Nkwabi, huku kwenye Ujumbe kukiwa na wagombea 19 akiwamo aliyewahi kuwa Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda ‘Simba wa Yuda’.

Baadhi ya Wajumbe ni; Patrick Rweyemamu, Asha Baraka, Jasmine Badou, Ally Suru, Iss Kajuna, Said Tulliy, Hamis Ramadhan, Christopher, Abdallah Migomba, Hussein Mlinga, Mohammed Wendi, Juma Pinto, Abubakar Zebo, Seleman Haroub, Zawadi Kadunda na Alfred Eliya.

Uchaguzi huo utafanyika ikiwa ni mwanzo wa safari ya kuundwa kwa Simba mpya itakayofuata mfumo wa kisasa wa hisa unaofanya timu hiyo iwe chini ya mwekezaji na kuondoka na ule mfumo uliozoeleka wa klabu kumilikiwa na wanachama.

Ingawa zoezi la uchukuaji na urudishwaji wa fomu za wagombea umeendeshwa kwa usiri mkubwa, kama uchaguzi huo utafanyika sirini, lakini Wanasimba wenye dhima ya kuifanya Simba izaliwe upya sasa ni zamu yao. Zamu ya kuhakikisha klabu inaingia kwenye mfumo huo mpya kwa kishindo na kuwa mfano kwa kuchagua watu wanaoamini wataisaidia klabu yao kwenda na falsafa ya mfumo huo chini ya mwekezaji mkuu, Mohammed ‘Mo’ Dewji.

Japo ni mapema kwa sasa kuanza kuwajadili wagombea waliojitokeza kwa nafasi zinazowaniwa kwa maana ya Uenyekiti na Wajumbe watano wa Bodi ya Wakurugenzi, lakini kwa kuitakia Simba yenye afya ni nafasi ya watakaoshiriki uchaguzi huo kuanza kuwasoma na kuwaelewa wagombea hao. Ni lazima wahakikishe wanawajua kwa undani wagombea hao ili kujiridhisha kuwapa nafasi za kuwawakilisha kwenye Bodi ya Wakurugenzi kwa mustakabali wa Simba mpya.

Wajumbe hao wa kuchaguliwa wakiungana na wawili wa kuteuliwa na mwenyekiti utaifanya klabu kuwa na timu ya watu makini ambao wataenda kushirikiana na wale wa wajumbe wa upande wa mwekezaji kuweza kufanya kazi ya kuitoa Simba mahali ilipo hadi kwenye kilele cha mafanikio na maendeleo ya Simba SC Co. Ltd.

Kama wanachama wa Simba wataendelea kuishi katika zama zile za mfumo wa kizamani wa kuchagua watu kwa sababu tu ya kuongeza kwake kwa ufasaha, rangi ama ubabe wake wa kupinga kila jambo lililopo mbele yake, haitasaidia kitu.

Licha ya vigezo vya elimu vilivyowekwa, pia wagombea waliojitokeza katika uchaguzi huo wanapaswa kupimwa na rekodi zao za nyuma katika kupigania maendeleo ya klabu hiyo na namna wanavyoweza kusaidia kuipeleka mbele.

Kufanya kosa sio kosa, ila kurudia kosa ndio kosa...wanachama wote wa Simba ni wazi wanawajua nje ndani ya wagombea waliojitokeza katika kinyang’anyiro hicho na wakati wakisubiri kujua watakaopitishwa kwenda kuchuana mwishoni, lazima wapitie kwa ufasaha wasifu wa wagombea wote ili kuwajua kwa undani.

Pia watumie nafasi za kampeni za wagombea hao kusikiliza kwa makini hoja zao na kuwaelewa kama ni wenzao katika safari ya matumaini.

Kusikiliza kampeni jinsi watakavyojinadi itawarahisishia kazi pia kuwajua kwa undani wagombea kama kweli ni wenzao ama la katika kuifanya Simba mpya iwe ya kuigwa ndani na nje ya nchi. Kitu cha muhimu ni kila mwanasimba kushiriki kwa namna moja ama nyingine katika kufanikisha safari ya mafanikio ya Simba mpya, ili hata mambo yakiwa mazuri ama mabaya kusiwe wa kumnyooshea kidole kwani ni wao waliofanya uamuzi.

Ndoto ya kila mwanasimba ni kutaka kuiona Simba ikiingia kwenye anga za klabu za TP Mazembe ya DR Congo, Al Ahly na Zamalek za Misri na nyingine zinazotamba katika Afrika kuanzia kisoka hadi kiuchumi.

Ndio maana tunawakumbusha wanasimba, huu ni wakati wao wa kuisaidia klabu yao kuianza safari ya kuzivifuata vigogo wa soka Afrika ambazo baadhi zina umri mchache tangu kuasisiwa kwao kulinganisha na wababe hao wa soka nchini.

Kosa lolote ambalo watalifanya sasa, linaweza kuwa majuto kwao kwa miaka minne ya kipindi cha uongozi kwa watakaochaguliwa Novemba 3 ambao watashirikiana na mwekezaji kuifanya Simba ipae ama la. Wanasimba kazi kwenu!

Advertisement