Wanarudi kuwashika

Friday September 14 2018

 

L0NDON ENGLAND. LIGI ya Mabingwa Ulaya imerudi tena na droo ya hatua ya makundi imeleta mechi nyingi za kusimulia ndani ya mwezi huu.

Liverpool iliyofika fainali msimu uliopita, imepangiwa vigogo, ikipewa timu za Paris-Saint Germain na Napoli, sambamba na Red Star Belgrade kwenye Kundi C.

Inter Milan imerejea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini miamba inayoikabili si mchezo, imepangwa na Barcelona, Tottenham Hotspur na PSV Eindhoven, wakati Juventus, Manchester United, Valencia na BSC Young Boys zimepangwa kwenye kundi moja.

Kutokana na makundi ya msimu huu yalivyopangwa, yatawashuhudia wachezaji kibao wakirudi kucheza dhidi ya timu zao za zamani, hapo ndipo utamu unapozidi kunoga!

Cristiano Ronaldo

v Man United

Si mara ya kwanza kwa Cristiano Ronaldo kumenyana na Manchester United kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, aliwahi kufanya hivyo wakati akiwa na Real Madrid. Lakini, msimu huu atakuwa na Juventus akiwakabili waajiri wake wa zamani, Man United. Ronaldo aliichezea Man United mechi 292 kabla hajahama na sasa yupo Juventus, mahali ambako ameshacheza mechi tatu kwenye Serie A. Ukiweka kando Ronaldo kuwakabili Man United, supasta huyo wa Ureno, atakutana pia na kocha wake wa zamani, Jose Mourinho, ambaye aliwahi kufanya naye kazi huko Bernabeu.

Paul Pogba

v Juventus

Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, moja ya mechi za hatua ya makundi itazikutanisha Manchester United na Juventus. Mechi hiyo itamfanya kiungo Paul Pogba kukutana na timu yake ya zamani, Juventus.

Akiwa kwenye kikosi cha Juventus, Pogba alicheza mechi 178, hivyo msimu huu atarudi Turin kumenyana na waajiri wake wa zamani na kwa sasa wanajadili ishu ya kumrudisha kwenye kikosi chao.

Jambo hilo ndilo linalozidisha mvuto wa mechi hiyo kwa sababu itakuwa Pogba dhidi ya Juventus.

Edinson Cavani

v Napoli

Napoli hadi sasa bado inaikumbuka huduma ya mshambuliaji wake matata, Edinson Cavani, aliyetumikia timu hiyo katika mechi 138. Lakini, kwa sasa staa huyo wa Uruguay anakipiga Paris Saint-Germain na kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, atawakabili waajiri wake wa zamani kwenye mechi za hatua ya makundi. Napoli imebadilika tangu Cavani aondoke, lakini bado atakwenda kukutana na Marek Hamsik.

Hii ni mara ya kwanza kwa Cavani kuivaa Napoli tangu atue PSG, lakini alifanya hivyo mara tano alipokuwa Palermo.

Thomas Lemar

v AS Monaco

Monaco imeachana na winga wake matata kabisa, Thomas Lemar kwenye dirisha lililopita la usajili akienda kujiunga na Atletico Madrid.

Kwenye kikosi cha Monaco, Lemar alicheza mechi 127, lakini sasa akiwa na Atletico ameshacheza mechi tatu. Kitendo cha Atletico Madrid kupangwa kundi moja na AS Monaco kwenye Ligi ya Mabingwa hiyo ina maana Lemar anarudi kumenyana na timu yake ya zamani kwenye michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu Ulaya.

Ni mechi ambayo itampa changamoto Lemar kutokana na jinsi anavyokubalika na mashabiki wa AS Monaco.

Radamel Falcao

v Atletico Madrid

Straika wa AS Monaco, Falcao atarudi kuwawinda waajiri wake wa zamani, Atletico Madrid atakapomenyana nao kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Falcao alishawahi kuwa Atletico Madrid na amecheza mechi 91, hivyo mechi hiyo ya makundi itamshuhudia Mcolombia huyo akirudi kucheza dhidi ya timu yake ya zamani.

Falcao alikaa kwenye timu hiyo kwa miaka miwili, akifunga mabao 70 katika mechi hizo 91, hivyo Atletico itakuwa na ufahamu inakwenda kukutana na mshambuliaji wa aina gani katika mechi hiyo ya hatua ya makundi itakapoanza na AS Monaco.

Philippe Coutinho

v Inter Milan

Kiungo wa Kibrazili, Coutinho kwa sasa anakipiga Barcelona. Lakini, kabla ya hapo aliwahi kuwa Inter Milan, ambako alicheza mechi 47 kabla ya kwenda Liverpool ambayo ilimuuza Barcelona Januari mwaka huu.

Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, mechi zake za makundi, Barcelona imepangwa na Inter Milan, hivyo jambo hilo litamfanya Coutinho kwenda kuvaana na timu yake ya zamani. Inter ndiyo ilikuwa klabu ya kwanza ya Ulaya kwa Coutinho baada ya kumsajili wakati huo akiwa na umri wa miaka 16 mwaka 2008.

Joao Cancelo

v Valencia

Concelo kwa sasa yupo kwenye kikosi cha Juventus, ambacho kimeshacheza mechi tatu kwenye Serie A msimu huu. Aliwahi kuwapo Valencia na ameichezea mechi 91.

Concelo amejiunga na Juve kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa wachezaji akitokea Valencia, lakini haikuwa moja kwa moja kwa sababu msimu uliopita alikuwa kwa mkopo Inter Milan. Beki huyo Mreno aliichezea Valencia kwa msimu mitatu na kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya atarudi kuikabili timu yake ya zamani.

Carlo Ancelotti

v PSG

Kocha Carlo Ancelotti kwa sasa yupo Napoli, amecheza mechi tatu, ameshinda mbili, amepoteza moja, lakini alipokuwa Paris Saint-Germain alicheza mechi 77, ameshinda 49, sare 17 na kupoteza mara 11. Kwenye mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, Ancelotti atarudi kumenyana na timu yake ya zamani, PSG. Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Ancelotti kukutana na timu za zamani, amefanya hilo mara nane ikiwamo kwenye fainali ya michuano hiyo ya Ulaya wakati alipoichapa Juventus akiwa na AC Milan miaka miwili tu baada ya kuachana nayo.

Wachezaji wengine

Mastaa wengine watakaorudi kucheza na timu zao za zamani kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu ni pamoja na Andreas Pereira (Man United) akichuana na Valencia, Jason Denayer (Lyon) dhidi ya Man City, Renato Sanches (Bayern Munich) dhidi ya Benfica, Rafinha (Barcelona) dhidi ya Inter Milan, Benedikt Howedes (Lokomotiv Moscow) atacheza na Schalke na Olarenwaju Kayode (Shahktar Donetsk) ataikabili Manchester City.

Advertisement