Wanaogelea kwa staili tano

Muktasari:

Shebe alisema kuwa klabu ya kuogelea ya Morogoro itakuwa na waogeleaji 27 wakati klabu mpya ambayo inakuja kwa kasi, FK Blue Marlins itakuwa na waogeleaji 25, UWCEA (13), Wahoo (6) na waogeleaji tisa wataibeba klabu ya Braeburn.

JUMLA ya waogeleaji 228 kutoka klabu tisa za Tanzania Bara na Zanzibar watashiriki katika mashindano ya kuogelea ya Taliss-IST yaliyopangwa kufanyika Jumamosi na Jumapili kwenye bwawa la kuogelea la IST lililopo Masaki, Dar es Salaam.

Meneja wa klabu ya Taliss-IST, Hadija Shebe alisema kuwa waogeleaji 78 wataiwakilisha klabu ya Taliss ambapo klabu ya Bluefins itawakilishwa na waogeleaji 39 na ile ya Dar es Salaam Swimming Club (DSC) itakuwa na waogeleaji 31.

Shebe alisema kuwa klabu ya kuogelea ya Morogoro itakuwa na waogeleaji 27 wakati klabu mpya ambayo inakuja kwa kasi, FK Blue Marlins itakuwa na waogeleaji 25, UWCEA (13), Wahoo (6) na waogeleaji tisa wataibeba klabu ya Braeburn.

Alisema kuwa ujumla staili tano zitashindaniwa na waogeleaji katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Jubilee Insurance na Nissan ambao ni wadhamini wakuu, Burger 53, Subway, FLM Catering na Azam.

Staili hizo ni free, butterfly, backstroke, breaststroke na Individual Medley. Waogeleaji watashindana katika umri tofauti ambao ni chini ya miaka minane, tisa na 10, miaka 11 na 12, 13 na 14 na kuanzia miaka 15 na kuendelea.

“Kutakuwa na jumla ya mashindano 105 ambapo siku ya kwanza waogeleaji watashindana katika mashindano 71 na siku ya pili watamalizia. Washindi katika kila umri watazawadiwa vikombe na washindi katika kila tukio watazawadiwa medali mbalimbali,” alisema.