Wanamuziki 30 kuwasha moto Tamasha la Fiesta Dar

Thursday November 22 2018

 

By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Zaidi ya wanamuziki 30 wanatarajiwa kushiriki katika tamasha la fiesta linalotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu kwenye Viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kamati ya Maandalizi, Gardner G Habash, alipokuwa akizungumzia tamasha hilo.

Habash amesema mpaka kufika leo wasanii 30 tayari wamesajiliwa na wengine bado wataendelea kuwasajili hadi siku ya Jumamosi asubuhi.

Akielezea mafanikio ya tamasha hilo tangu lianze amesema anashukuru limekuwa la mafanikio ikiwemo kupokelewa vizuri katika kila mahali walipopita.

Pia, wasanii amesema wamekuwa wabunifu tofauti na huko nyuma na pia wamekuwa wakiishi kwa kushirikiana na kupendana.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Tigo wadhamini wakuu wa tamasha hilo, William Kapinga amesema kiingilio katika tamasha hilo ni Sh15,000 kwa watakaolipia getini na Sh10,000 kwa watakaolipa kwa tigopesa.

Wakati wale watakaotumia usafiri wa Uber kwenda katika tamasha hilo na wakati huohuo wakiwa wamelipa kwa tigopesa watapata punguzo la Sh5000.

Akizungumza kwa niaba ya wasanii, Joh Makini, amesema wakazi wa Dar es Salaam wategemee mambo makubwa katika shoo hiyo kwani kila walipopita wameacha alama hivyo hata katika Jiji hilo watarajie mambo mazuri pia.

Advertisement