Wanamichezo mnaweza kuchepuka kidogo mashindano ya Bandari

Muktasari:

Timu shiriki ni Bandari Dar es Salaam, Bandari Tanga, Bandari Mtwara na timu iliyoundwa na Bandari za maziwa likiwemo la Vitoria, Tanganyika na Nyasa huku timu moja moja ikihusisha Bandari Zanzibar na Ticts Football Team.

Morogoro. Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya bandari Tanzania (TPA), Jayne Nyimbo amewaacha midomo wazi wanamichezo zaidi ya 480 baada ya kusema wanaweza kufanya mchepuka kidogo wakati wa mashindano ya Bandari (Inter-Ports Games 2019) yatakayofanyika kwa siku tano kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Bandari, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa mamlaka ya bandari Tanzania (TPA), Nyimbo alisema uwepo wa wanamichezo zaidi ya 480 Manispaa ya Morogoro ni fursa kwa wafanyabiashara kutengeneza fedha ndani ya siku tano za mashindano hayo.

“Mkuu wa mkoa wa Morogoro, hao unaowaona mbele yako ni zaidi ya wanamichezo 480 watakuwa hapa Manispaa ya Morogoro kwa siku tano za mashindano, hii ni fursa kwa wafanyabiashara katika kutoa kuwahudumia kwenye nyumba za kulala wageni, usafiri wa bodaboda, mamalishe, lakini na sisi tutafanya mchepuko kidogo.” alisema Jayne.

Kauli hiyo ilifanya kundi la wanamichezo hao kuangua vicheko ikiashiria jambo hilo limekaa kiutani zaidi.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare akawataka wanamichezo kudumisha ushirikiano na kujenga undugu na kuacha kucheza michezo isiyo ya kiungwana.

“Najua kila timu imejiandaa vizuri kushiriki, kushindana na mshindane kwa nidhamu na mdumishe ushirikiano baina yetu lakini ni vizuri pia kuepuka tabia ambazo zinaweza kuathiri afya zetu pamoja na kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.’alisema Ole Sanare.

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema michezo hiyo inasaidia kumfanya mfanyakazi kuwa na utimamu wa akili na kumtengenezea afya ya mwili baada ya kushiriki.

Mhandisi Kakoko alisema kuwa mashindano hayo yanafanyika mkoani Morogoro kwa mara ya pili mfululizo kutokana na utamu walioupata kwa urafiki wa kijiografia.

“Mwaka jana mashindano haya alifanyika hapa Jamhuri na kwa sababu Rais Magufuli amewahi kusema kuwa Morogoro katikati ya nchi na sisi tumepapenda na tulipata utamu,”alisema Mhandisi Kakoko.

Mashindano hayo yanashirikisha wanamichezo katika michezo ya soka, netiboli, bao, kuvuta kamba na riadha ikishirikisha timu za Bandari Dar es Salaam, Bandari Tanga, Bandari Mtwara na timu iliyoundwa na Bandari za maziwa likiwemo la Vitoria, Tanganyika na Nyasa huku timu moja moja ikihusisha Bandari Zanzibar na Ticts Football Team.