Wameuzwa tofauti na bei zao sokoni

Saturday December 8 2018

 

By LONDON, ENGLAND

JANUARI haipo mbali wakati mashabiki wa soka watakaposhuhudia kwa  mara nyingine dirisha la usajili wa wachezaji likifunguliwa. Wakati wa usajili unapofika kuna timu zimekuwa zikiuziwa wachezaji kwa pesa nyingi bila ya kuzingatia thamani zao halisi sokoni.
Hawa hapa mastaa waliouzwa kwa pesa nyingi kuliko thamani zao zilivyokuwa sokoni kwa kipindi hicho wanapigwa bei na kununuliwa na timu nyingine.

6.Gareth Bale- Real Madrid
Amenunuliwa: Pauni 90.90 milioni
Thamani yake sokoni: Pauni 58.50 milioni
Mwaka 2013, Real Madrid ilitaka kuwajibu Barcelona baada ya kumsajili Barcelona. Wao walikwenda kumsajili winga wa Tottenham Hotspur, Gareth Bale. Kwenye usajili huo, Los Blancos walilipa Pauni 90.90 milioni kumnasa Bale, wakati thamani yake halisi sokoni kwa wakati huo ilikuwa Pauni 58.50 milioni. Akiwa na kikosi cha Madrid, Bale ameshinda mataji mengi, lakini ukweli ni kwamba alitua Bernabeu kwa pesa kubwa sana kuliko thamani yake halisi ya bei yake sokoni.

5.Paul Pogba- Man United
Amenunuliwa: Pauni 94.50 milioni
Thamani yake sokoni: Pauni  63 milioni
Manchester United wanaona kama wameibiwa hivi wakati Juventus ilipowataka walipe Pauni 94.50 milioni kwa ujumla wake ada na bonasi nyingi ili kunasa saini ya kiungo Paul Pogba mwaka 2016. Mfaransa huyo ameshindwa kucheza kwa kufikia matarajio kwenye kikosi hicho. Kocha wake amekuwa akimshutumu kwamba haweki jitihada anapokuwa ndani ya uwanja. Lakini, wakati anasajili, Pogba thamani yake sokoni ilikuwa Pauni 63 milioni, hivyo hapo Man United ililipa Pauni 31.50 milioni zaidi kupata huduma ya staa huyo.

4.Cristiano Ronaldo- Juventus
Amenunuliwa: Pauni 105.30 milioni
Thamani yake sokoni: Pauni 90 milioni
Juventus walilipa Pauni 105.30 milioni kupata huduma ya supastaa Cristiano Ronaldo kutoka Real Madrid kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Hata hivyo, kwa wakati huo wakati Juve inamsajili CR7, thamani yake sokoni ilikuwa Pauni 90 milioni. Kwa maana hiyo, Juve wamelipa zaidi ya Pauni 15.30 milioni zaidi kupata huduma ya staa huyo ambaye ni mshindi mara tano wa tuzo za Ballon d’Or. Bado ameonyesha kuwa na uwezo mkubwa akifunga mabao 10 kwenye Serie A msimu huu.

3.Philippe Coutinho- Barcelona
Amenunuliwa: Pauni 117 milioni
Thamani yake sokoni: Pauni 81 milioni
Thamani ya Philippe Coutinho sokoni kwenye dirisha la Januari wakati Barcelona inamsajili ilikuwa Pauni 81 milioni. Hata hivyo, wababe hao wa Nou Camp walitoa mkwanja mrefu zaidi kupata huduma ya Mbrazili huyo kutoka Liverpool ili kwenda kuziba pengo lililoachwa wazi na Neymar. Kwenye mchakato huo, Barcelona ililipa Pauni 117 milioni huko Liverpool kumnasa fundi huyo wa mpira. Kwa maana hiyo, Barcelona wamelipa Pauni 36 milioni zaidi kwenye usajili wa mchezaji huyo kwa kulinganisha thamani yake ilivyokuwa sokoni.

2.Kylian Mbappe- PSG
Amenunuliwa: Pauni 121.50 milioni
Thamani yake sokoni: Pauni 108 milioni
Waandaaji wa Ballon d’Or, France Football walianzisha tuzo mpya kuhakikisha kinda wa Kifaransa, Kylian Mbappe anashinda kitu kutokana na kile alichokifanya mwaka huu. Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 19 alishinda tuzo inayoitwa Kopa ikiwa na maana ya makinda wanaochipukia. Mwaka huu, Mbappe ameshinda mataji manne akiwa na PSG na alifunga mabao manne kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 kuisaidia Ufaransa kushinda taji hilo. PSG ilimnasa kwa Pauni 121.50 milioni wakati thamani yake halisi sokoni ilikuwa Pauni 108 milioni. Kwa maana hiyo, alinunuliwa kwa Pauni 13.5 milioni zaidi.

1.Neymar- PSG
Amenunuliwa: Pauni 199.80milioni
Thamani yake sokoni: Pauni 90 milioni
Kwa mwaka 2017, thamani ya supastaa Neymar sokoni ilikuwa Pauni 90 milioni. Lakini, PSG wakafanya kufuru kulipa Pauni 199.80 milioni kumnunua Mbrazili huyo. Kwa maana hiyo wamelipa zaidi ya Pauni 109 milioni kuliko thamani yake halisi. Shida kubwa ilitokana na kipengele kilichokuwa kimewekwa kwenye mkataba wake huko Barcelona.Advertisement