Wametengenezewa nafasi, wameshindwa kutupia!

Tuesday February 12 2019

LONDON, ENGLAND.KWENYE soka kitu cha kwanza kikubwa inachofanya timu ni kujaribu kutengeneza nafasi za kufunga, ili mabao yafungwe na ushindi upatikane.

Lakini, katika hilo kuna baadhi ya mastaa wamezigharimu sana timu zao kutokana na kupoteza nafasi nyingi za kufunga walizotengenezewa na wenzao mchezoni.

Hawa hapa mastaa watano waliopoteza nafasi nyingi za kufunga kwenye Ligi Kuu England msimu na kama wangefunga basi habari ingekuwa nyingine.

Lakini, data hizo hazihusishi nafasi walizopoteza kwenye mechi zilizopigwa wikiendi iliyopita, ambayo ilishuhudia Chelsea wakipigwa Sita Bila na Manchester City.

5. Jamie Vardy

– nafasi 12

Advertisement

Fowadi wa Leicester City, Jamie Vardy, ni moja ya washambuliaji matata kabisa waliopo kwenye Ligi Kuu England. Vardy amekuwa tishio kubwa kwa mabeki wa timu pinzani, lakini kuna shida moja kubwa inayomkabili ni kwamba amekosa umakini mkubwa katika kuweka mipira kwenye nyavu. Anafunga, lakini kama angekuwa makini angeweza kufunga mabao mengi zaidi. Kwa sasa Vardy amefunga mabao manane, lakini amepoteza nafasi 12 za kufunga, ambazo zingemfanya awe mbali kwa mabao.

4. Mohamed Salah

– nafasi 12

Staa wa Liverpool, Mohamed Salah amefunga mabao 17 kwenye Ligi Kuu England hadi sasa msimu huu. Mabao hayo yanamfanya aongoze kwenye kufunga, akifungana kwa mabao na Sergio Aguero wa Manchester City. Lakini, Mo Salah angekuwa na mabao mengi sana kama angekuwa makini na kutumia nafasi alizopata uwanjani kwani kabla ya mechi ya wikiendi, ambayo alitupia wavuni, fowadi huyo amepoteza nafasi 12 za kufunga kwenye ligi hiyo kwa msimu huu. Mo Salah anafunga, lakini kushindwa kuwa makini zaidi, kutamgharimu msimu huu kwenye mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu huko England na Ulaya.

3. Gabriel Jesus

– nafasi 12

Licha ya kutambua kwamba analazimika kugombea nafasi na straika matata Sergio Aguero, Mbrazili Gabriel Jesus bado anashindwa kupandisha kiwango chake cha mpira na hasa kwenye kufunga mabao kwa maana ya kuhakikisha anatumia vyema kila nafasi anayopata kama anavyofanya mpinzani wake. Staa huyo wa Kibrazili amefunga mabao sita katika mechi 20 alizocheza katika kikosi cha Manchester City, lakini angeweza kufunga mara nyingi zaidi kama angekuwa makini, kwani amepoteza nafasi za kufunga mara 12 na kuigharimu timu yake.

2. Callum Wilson

– nafasi 13

Ikinyakua pointi 33 katika mechi 25, ni kitu rahisi kusema kwamba Bournemouth hawapo vibaya sana kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Mechi yao iliyopita walichapwa na Liverpool. Lakini, kwa mabao yao waliyofunga msimu huu, theluthi moja, yamewekwa wavuni na mshambuliaji Callum Wilson, aliyeweka nyavuni mara 10 katika mechi 21. Lakini, Wilson angeweza kufunga mabao mengi zaidi kama asingepoteza nafasi nyingi za kufunga alizozipata, amepoteza nafasi 13 za kufunga.

1. Pierre-Emerick Aubameyang

– nafasi 17

Arsenal ya Unai Emery imekuwa haina viungo wengi wabunifu kwenye ligi msimu huu na hilo linawafanya washambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette kuwa katika presha kubwa ya kupata nafasi za kufunga.

Hata hivyo, wamejitahidi kwa uwezo wao kutengeneza nafasi nyingi za kutosha kiasi cha kumfanya Aubameyang kufunga 15 na nyingine 17 akikosa.

Kwa rekodi zisizohusisha mechi za wikiendi iliyopita, Aubameyang ndiye aliyekuwa akiongoza kwa kukosa nafasi nyingi kwenye ligi hiyo.

Advertisement