Wameliamsha kinoma

TAMASHA la Simba ni moja kati ya matukio makubwa nchini kwani ni sehemu ya maadhimisho ya klabu hiyo kutimiza miaka takribani 82 tangu ilipoanzishwa mwaka 1936. Hutumika kutambulisha kikosi, vifaa na jezi ambazo Simba itatumia kwenye msimu wa mashindano unaofuata lakini pia huambatana na matukio kadhaa yenye lengo la kuwakutanisha pamoja, mashabiki, wapenzi, wanachama, viongozi na wachezaji wa klabu hiyo.

Hufanyika kila ifikapo Agosti 8 na tamasha la mwaka huu litakuwa la kumi (10) mfululizo katika historia yake tangu lilipoanzishwa mwaka 2009.

Katika kipindi hicho cha miaka tisa ya tamasha la Simba Day, wapo wachezaji ambao wamekuwa na bahati ya kushiriki mara nyingi kwenye tukio hilo la kihistoria.

Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya wachezaji wa Simba walioshiriki mara nyingi tamasha hilo.

JONAS MKUDE - 7

Kiungo wa Simba, Jonas Mkude licha ya umri wake wa miaka 26, anaongoza chati ya wachezaji walioshiriki mara nyingi Simba Day akiwa amefanya hivyo mara saba na tamasha la mwaka huu litakuwa la nane kwake. Miaka ambayo Mkude ameshiriki Simba Day ni 2011,2012, 2013, 2014, 2015, 2016 na 2017.

SAID NASSORO ‘CHOLLO’ - 7

Mkude yupo sawa na beki huyo kwani Chollo naye ameshiriki Simba Day mara saba ambapo ni mwaka 2009, 2010, 2011, 2012, 2013, 2014 na 2015. Chollo aliondoka Simba aliichezea Stand United, Mwadui FC na Dodoma FC.

SAID NDEMLA -5

Hili litakuwa tamasha la sita kwa Said Ndemla, kiungo mshambuliaji huyo ameshiriki matamasha matano ya Simba Day ambapo ni mwaka 2013, 2014, 2015, 2016 na 2017, hili litakuwa tamasha lake la sita.

MWINYI KAZIMOTO -5

Kazimoto anayecheza nafasi ya kiungo, angefikia rekodi ya Ndemla iwapo angekuwepo kwenye kikosi cha Simba msimu ujao. Kazimoto hayupo kwenye usajili mpya baada ya mkataba wake kumalizika jambo. Hata hivyo, ameshiriki mara nyingi tamasha hilo ambapo mwaka 2011, 2012, 2015, 2016 na 2017, Kazimoto alikuwa miongoni mwa nyota wa kikosi cha Simba.

AMRI KIEMBA -5

Ni miongoni mwa nyota walioshiriki tamasha la Kwanza la Simba Day mwaka 2009 akiwa ni mmoja wa nyota wa kikosi cha kwanza cha Simba. Kiemba mbali ya tamasha la mwaka 2009, pia ameshiriki miaka ya 2010, 2011, 2012 na 2014. Kiemba kwasasa amestaafu kucheza soka.