Wamefunika kwa mabao 2018

Saturday December 8 2018

LONDON, ENGLAND
LIGI Kuu mbalimbali za Ulaya zinaendelea kupamba moto hasa kwa kipindi hiki kigumu cha baridi katika bara hilo. Ligi nyingi zitasimama kupisha baridi hiyo na mapumziko ya Krismasi, lakini ligi moja tu, Ligi Kuu England, yenyewe mechi zake zitaendelea kupigwa bila kusimama.
Kwa maana hiyo, ligi hizo zitakazosimama zikirudi itakuwa mwaka huu wa 2018 umeshakwisha na kuanza kwa Mwaka Mpya 2019.
Kutokana na hilo, makala haya yanaangazia wachezaji waliofunga mabao  mengi kwenye mechi za ligi kwa mwaka wote wa 2018 kwa mechi zilizochezwa hadi sasa huku supastaa wa Kireno, Cristiano Ronaldo akiongoza kwenye idadi hiyo.
Hii hapa orodha ya mastaa sita wanaoongoza kwa kufunga mabao kwenye mechi za ligi zilizochezwa kwa mwaka huu pekee, 2018.

6.Cristhian Stuani- mabao 23, mechi 30
Straika wa Girona, Cristhian Stuani anashika namba sita kwa vinara wa mabao kwenye mechi za ligi kwa mwaka wote wa 2018. Fowadi huyo wa kimataifa wa Uruguay amefunga mabao 23 katika mechi 30 alizocheza kwenye La Liga hadi kufika sasa, ambapo zimebaki siku chache kwa mwaka huu kufika mwisho. Kwa rekodi zake za La Liga kwa msimu huu wa 2018/19, straika huyo mwenye umri wa miaka 32, amefunga mabao 11 na hivyo kuwa kinara wa mabao kwenye ligi hiyo akiwaburuza wakali kama Lionel Messi na Luis Suarez kwenye kupasia mipira nyavuni. Stuani ni mmoja wa wachezaji hodari kwa kufunga kutokana na kufunga mara nyingi kwenye mwaka huu wa 2018.

5.Luis Suarez- mabao 24, mechi 32
Mashabiki wa Barcelona walikuwa kwenye mashaka makubwa wakati Lionel Messi alipotakiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu baada ya kuumia bega. Lakini, fowadi wao mwingine Luis Suarez alijivisha majukumu na kuifanya Barcelona kuzidi kutamba na kushinda mechi zake muhimu katika La Liga na hata akafunga 'hat-trick' kwenye El Clasico, wakati wakali hao wa Nou Camp walipoishushia kipigo cha mabao 5-1 Real Madrid. Kuonyesha kwamba Suarez si mshambuliaji wa mchezo mchezo, kwa mwaka huu wa 2018 pekee amefunga mabao 24 katika mechi 32 alizocheza kwenye La Liga. Kwa msimu huu mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31 amefunga mabao tisa na kuasisti manne kwenye mikikimikiki hiyo ya La Liga.

4.Florian Thauvin- mabao 25, mechi 31
Winga wa Olympique Marseille, Florian Thauvin si mtu anayepamba sana vichwa vya habari vya magazeti, lakini huduma ya staa huyo wa Ufaransa ni moto kwelikweli anapokuwa dimbani. Kwa mwaka huu, Thauvin amefunga mabao mengi na amekuwa tishio sana mbele ya goli kuliko washambuliaji watatu wa PSG kwa pamoja, Kylian Mbappe, Neymar na Edinson Cavani. Kwa ujumla wake, Thauvin, ambaye alichemsha sana alipokuwa kwenye kikosi cha Newcastle United, kwa mwaka huu peke yake amefunga mabao 25 katika mechi 31 alizocheza kwenye Ligi Kuu Ufaransa. Huduma yake ni muhimu kweli kweli katika kikosi hicho cha Marseille, licha ya kwamba mara nyingi amekuwa akianzia benchi.

3.Mbaye Diagne- mabao 28, mechi 31
Kasimpasa si jina maarufu sana kwa mashabiki wa soka waliopo nje ya Uturuki, lakini kama unamfahamu Rais Recep Tayyip Erdogan, basi bila ya shaka utakuwa umesikia kitu kuhusu timu hiyo kwa sababu uwanja wao wanaoutumia kwa mechi za nyumbani unaitwa jina la rais huyo. Lakini, sababu moja kubwa ya kuizungumzia timu hiyo kwa sababu straika wao Mbaye Diagne amekuwa mmoja wa wachezaji waliofunga mabao mengi kwa mechi za ligi zilizochezwa ndani ya mwaka huu wa 2018 pekee. Fowadi huyo amefunga mabao 28 katika mechi 31 alizoitumikia timu hiyo ndani ya mwaka huu.

2.Lionel Messi- mabao 28, mechi 31
Kinara wa mabao wa La Liga kwa msimu wa 2017/18, Lionel Messi anashika namba mbili kwa mastaa waliofunga mabao mengi kwa  mwaka 2018 pekee, akiwa ameweka kwenye kamba mara 28 katika mechi 31 alizocheza hadi sasa. Kwa msimu huu, Messi amefunga mara tisa kwenye La Liga na hivyo kufanya idadi yake ya mabao aliyofunga tangu mwaka ulipoanza Januari kufikia 28. Kwenye Ballon d'Or kwa mwaka huu aliishia kushika nafasi ya tano, huku kiungo Luka Modric akiibuka mshindi. Messi alikosa mechi kadhaa mwaka huu kutokana na kuwa majeruhi.

1.Cristiano Ronaldo- mabao 32, mechi 29
Supastaa wa Juventus, Cristiano Ronaldo haonekani kuchoka kufunga kwa siku za karibuni. Fowadi huyo amejiunga na Juventus kwenye dirisha lililopita akitokea Real Madrid. Tangu alipotua kwa Vibibi Vizee, Ronaldo ameendeleza moto wake wa kufunga, ambapo ndani ya msimu huu ameshafunga mabao 11 katika mechi 18. Mabao hayo yamemfanya Ronaldo kufikisha mabao 32 katika mechi 29 za ligi alizocheza tangu mwaka huu uanze akiwa na kikosi cha Real Madrid na Juventus.Advertisement