Wamefunga mara nyingi robo fainali Mabingwa Ulaya

Muktasari:

  • Wakati michuano hiyo ikifika kwenye hatua hiyo ya nane bora kuna mastaa hao wameweka rekodi zao tamu kabisa kwa kufunga mabao mara nyingi katika mechi za hatua hiyo ya robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

BARCELONA,HISPANIA.KIPUTE cha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kinaendelea, usiku wa leo Jumanne kasheshe litakuwa huko Nou Camp wakati Barcelona na Lionel Messi wake watakapowakaribisha Manchester United wakati huko Turin, Juventus watakuwa nyumbani kucheza dhidi ya Ajax.

Kufumba na kufumbua, kesho Jumatano kutakuwa na mechi nyingine matata ambapo Liverpool watakuwa ugenini dhidi ya FC Porto huko Ureno, wakati kwenye nyasi za Etihad, wenyeji Manchester City watamaliza ubishi dhidi ya Tottenham Hotspur.

Wakati michuano hiyo ikifika kwenye hatua hiyo ya nane bora kuna mastaa hao wameweka rekodi zao tamu kabisa kwa kufunga mabao mara nyingi katika mechi za hatua hiyo ya robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

5. Andriy Shevchenko- mabao 9

Andriy Shevchenko ni moja ya washambuliaji bora kabisa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hasa kwa kipindi ambacho alikuwa kwenye kikosi cha AC Milan. Fowadi huyo wa zamani wa Ukraine, amefunga mabao tisa kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa mechi zake zote alizocheza akiwa Dynamo Kyiv na AC Milan. Shevchenko amefika fainali mbili za michuano hiyo akiwa na Milan na kushinda ubingwa mara moja.

4. Filippo Inzaghi- mabao 9

Straika Filippo Inzaghi alicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na vikosi bora kabisa Italia, Juventus na AC Milan. Hata hivyo, hakuwa na mafanikio wakati alipokuwa na Juventus, huku ubingwa wake wa Ligi ya Mabingwa Ulaya alibeba mara mbili akiwa na AC Milan. Inzaghi alizisaidia timu zote hizo mbili katika mechi zake za robo fainali, akiwa amefunga mabao tisa katika mechi za hatua hiyo ikiwa ni mabao yake aliyofunga katika mechi zote alizocheza.

3. Raul Gonzalez- mabao 10

Anashika namba mbili kwa kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya timu hiyo huku akiwa na rekodi ya kucheza mechi nyingi kwenye kikosi cha wababe hao wa Bernabeu. Staa huyo Mhispaniola alifunga mabao 10 katika mechi za robo fainali alizocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa timu zake alizochezea katika michuano hiyo, Real Madrid na Schalke. Amebeba ubingwa mara tatu akiwa na Madrid.

2. Lionel Messi- mabao 10

Messi ameisaidia Barcelona kushinda mara nne ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na rekodi zake kwenye mechi za robo fainali zinamwonyesha kwamba amefunga mabao 10. Hakufunga kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Manchester United hivyo anasubiri leo kuona kama ataongeza jingine.

1. C. Ronaldo- mabao 24

Cristiano Ronaldo ameonyesha kuwa ni tishio zaidi baada ya kufunga mabao 24 katika mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Staa huyo wa Ureno amefunga mabao hayo akiwa kwenye kikosi cha Manchester United, Real Madrid na Juventus huku akiwa amebeba ubingwa mara tano. Matarajio ya Juventus ni kwamba Ronaldo atawasaidia kuondoa gundu la kushindwa kubeba ubingwa huo.