Wamechezea vichapo England hadi aibu!

Muktasari:

Makocha hao pamoja na kupata mafanikio katika timu mbalimbali England bado wanashikiria rekodi ya kuona timu zao zimefungwa mechi nyingi katika Ligi Kuu England.

 LONDON, ENGLAND. Jose Mourinho amekumbana na vichapo vitatu kwenye Ligi Kuu England kwa msimu huu huko Manchester United katika mechi nane alizocheza. Hata hivyo, jambo hilo bado halimwingizi kwenye rekodi za makocha waliofungwa mechi nyingi kwenye Ligi Kuu England tangu ilipoanza. Hii ndio orodha ya makocha sita ambao wamechapwa mechi nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu England.

6 .Arsene Wenger- mechi 153

Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger amekuwa kwenye kiti cha ukocha kwenye mechi 828 za Ligi Kuu England katika miaka yake 22 aliyodumu kwenye kikosi hicho chenye maskani yake Emirates. Ameshinda mechi 476 kati ya hizo, ametoka sare mara 199 na kuchapwa 153. Amebeba mataji matatu tu ya Ligi Kuu England na mengi zaidi ya Kombe la FA. Atabaki kuwa gwiji wa aina yake kwenye kikosi hicho cha washika bunduki.

5. David Moyes- mechi 178

Kocha wa zamani wa West Ham United na Everton, David Moyes mambo yake bado si mazuri, akiwa hana kazi kwa sasa. Aliwasaidia West Ham wasishuke daraja, lakini uongozi wa timu hiyo hawakuona hiyo ni sababu ya kumpa mkataba wa muda mrefu zaidi hivyo wakaachana naye. Lakini, matatizo ya Moyes yalianzia pale alipokwenda kurithi mikoba ya Sir Alex Ferguson huko Manchester United. Rekodi zake kwenye Ligi Kuu England amenoa kwenye timu 526, ameshinda 204, sare 144 na amepoteza mara 178.

4. Mark Hughes- mechi 179

Tangu Mark Hughes aliposimamia mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England akiwa kocha wa Southampton, Machi mwaka huu, kikosi hicho chenye maskani yake St Mary's kimechapwa mara tisa kwenye ligi hiyo. Kwenye rekodi zake, kocha huyo aliwahi kuinoa pia Manchester City amechapwa mara 179 kwenye mechi za Ligi Kuu England kati ya 460 alizoziongoza timu yake. Mechi alizoshinda ni 158 na sare ni 123. Kazi yake kubwa ya msimu huu ni kuwaokoa Saints wasishuke. Aliwahi kuzinoa pia QPR, Fulham na Blackburn Rovers.

3. Sam Allardyce- mechi 199

Big Sam hana kazi kwa sasa ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka kibao kupita. Lakini, hilo lineonyesha wazi ni jinsi gani makocha wazawa wanavyochemsha kwenye Ligi Kuu England katika miaka ya karibuni. Kazi yake ya mwisho ilikuwa Everton, lakini baada ya kuwaokoa wasishuke daraja, alifutwa kazi na nafasi yake imechukuliwa na kocha Marco Silva. Kocha huyo maarufu kama Big Sam, amepoteza mechi 199 kwenye Ligi Kuu England. Baadhi ya timu alizowahi kuzinoa kwenye ligi hiyo ni pamoja na Crystal Palace, West Ham, Bolton, Sunderland na Newcastle.

 

2. Steve Bruce- mechi 207

Gwiji wa Manchester United, Steve Bruce amekuwa na rekodi ya hovyo kwenye Ligi Kuu England kwenye ukocha. Kocha huyo amefungwa mechi 207 kwenye Ligi Kuu England huku akiwahi kupita kwenye vikosi vya Hull City, Crystal Palace, Birmingham City, Sunderland na Wigan Athletics kwa uchache wake. Mechi alizoshinda kwenye ligi ni 132 na sare 137, hivyo kuwa na rekodi ya kufungwa mechi nyingi kuliko alizoshinda.

1.Harry Redknapp- mechi 239

Kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Harry Redknapp ndiye mwenye rekodi ya kupoteza mechi nyingi zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu England. Mwingereza huyo alishawahi kuzinoa Portsmouth, Southampton, West Ham, QPR na Bournemouth kwa kuzitaja kwa uchache tu. Alipokuwa Spurs aliisaidia timu hiyo kufika hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ndiye aliyembadili pia Gareth Bale kutoka kuwa beki wa kushoto hadi kuwa winga matata. Amefungwa mechi 239 kati ya 642 alicheza kwenye Ligi Kuu England huku mechi 167 zikiwa sare.