Wameanza kutetea majina yao

SIMBA, Yanga na Azam FC ndizo zinazoongoza kusajili wachezaji wa kigeni, tofauti na timu nyingine zinashiriki Ligi Kuu Bara, na kati ya mastaa waliojiunga na klabu hizo msimu huu, wapo walioanza kuonyesha makali.

Ni mastaa wa Simba na Yanga walioingia kwa kishindo nchini, wakazi wa jiji la Dar es Salaam walijua kuna ugeni kutokana na mapokezi waliyoyapata kwa mashabiki wa soka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere mpaka kwenye makao makuu ya klabu za Kariakoo, Jangwani na Msimbazi.

Japokuwa sio mastaa wote ambao waliteka mitandao ya kijamii wamefanikiwa kutikisa kwenye mechi tano ambazo klabu hizo zimecheza, wapo baadhi ambao wamewaaminisha mashabiki kwamba hawajaja kutembea.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya mastaa ambao wamewateka mashabiki kutokana na kile ambacho wamekionyesha katika mechi ambazo wamecheza.

MUKOKO TONOMBE-YANGA

Yanga ilimsajili kiungo Mukoko Tonombe akitokea As Vita ya DR Congo, wakati anatua ardhi ya Tanzania alikutana na mapokezi makubwa ya mashabiki wa Yanga waliojitokeza uwanja wa ndege.

Mukoko aliwahi kukiri kwamba mapokezi hayo ni kama deni ili kuhakikisha anaonyesha kile walichokitarajia kutoka kwake na amefanikiwa katika hilo, kwani tayari mashabiki wanafurahia undabwindabwi wake.

Katika mechi ambazo Mukoko amecheza Yanga za ligi na kirafiki dhidi ya KMKM na Mwadui, ameonekana kuwakosha mashabiki wa Jangwani na kupata hamu ya kuendelea kuona makuu kutoka kwake.

CARLOS FERNANDES ‘CARLINHO-YANGA

Japokuwa winga wa Yanga, Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ anaonekana sio mchezaji anayetumia nguvu, mashabiki wa timu hiyo wanafurahia jinsi ambavyo anatumia akili kucheza.

Katika mechi alizocheza za ligi na kirafiki, Carlinhos ameonekana anaaminiwa zaidi kupiga faulo na kona, huku akiwa anamiliki mpira mguuni - tageti yake kubwa ikiwa ni kupeleka mipira mbele.

Ni kati ya mastaa waliopata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki, mpaka alifikia hatua ya kutoa machozi. Hilo aliwahi kulizungumzia kwamba, alilia kwa sababu hajawahi kupata ukarimu kama ule katika maisha yake.

BENARD MORRISON-SIMBA

Kutikisa kwa usajili wa Benard Morrison ambaye si mpya kwenye macho ya mashabiki wa Tanzania, kulitokana na kuhama Yanga kwenda Simba, jambo ambalo bado linatikisa mpaka sasa kutokana na utata wa hapa na pale unaoelezwa juu ya uhamisho wake.

Katika mechi za Simba ambazo amecheza, mashabiki wamekuwa wakifurahia kumuona, wakimpigia miluzi na shangwe. Na hii ni pengine kutokana na uwezo wake ama kuhama kutoka kwa watani zao wa jadi.

CHRIS MUGALU-SIMBA

Simba ilimsajili Cris Mugalu kutoka Lusaka Dynamos na anaonekana ni mtaalamu wa kuzifumania nyavu za wapinzani wao, kwani mpaka sasa ana mabao matatu katika ligi, ilhali mechi za kirafiki anayo mawili.

Pamoja na kwamba mashabiki wa Simba hawakujitokeza kwa wingi kwenye mapokezi yake, ila usajili wake ulivuma na kutawala kwenye mitandao ya kijamii na kumfanya ajitume ili kulinda hadhi ya jina lake.

PRINCE DUBE- AZAM FC

Uwezo wake ndio umemtambulisha kwa Watanzania, kujua kuna straika hatari ndani ya kikosi cha Azam FC. Dube ndiye anaongoza kwa kufunga mabao matano kwenye Ligi Kuu Bara, akimuacha nyuma staa wa Simba, Meddie Kagere kwa bao moja.

Licha ya kwamba usajili wake haukuwa na mvumo mkubwa kama ilivyokuwa kwa mastaa wa Simba na Yanga - klabu ambazo zina utajiri wa mashabiki, Dube ameamua kuonyesha kishindo chake uwanjani.

JOASH ONYANGO- SIMBA

Ni beki mzoefu ambaye tangu alipojiunga na Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya ameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Onyango aliondokanchini Kenya akiwa mchezaji bora na ameonyesha kuwa ni bora kwenye michezo mitano ya Ligi Kuu Bara ambayo ameiongoza timu hiyo kwenye idara ya ulinzi wa kati ambayo kwa sasa anacheza pamoja na Pascal Wawa.