Wambura ngoma bado mbichi kabisa Kisutu

Thursday May 23 2019

 

By Fortune Francis

Dar es Salaam. Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha anaendelea kusota rumande kutokana na upelelezi kutokamilika.

Wakili wa serikali, Fatma Waziri amedai leo Mei 23, 2919 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mfawidhi Kelvin Mhina kuwa kesi hiyo imekuja kwaajili ya kutajwa upelelezi bado unaendelea.

Hakimu Mhina, aliahirisha kesi hiyo hadi, Juni 4, 2019 kesi hiyo itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Wambura alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza, Februari 11, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh 100 milioni, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2019.

Katika mashtaka hayo 17; shtaka moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Juni 6, 2004 sehemu isiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es salaam mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa la kughushi.

Advertisement

Siku hiyo, Wambura kwa nia ya kutapeli  alitengeneza barua ya  kughushi ambayo haina kumbu kumbu namba akionyesha  imeandikwa na E Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa  kampuni ya Jeck system anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka lingine Wambura anadaiwa kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, iliyokuwa haina kumbu kumbu namba ya Julai 6, 2004, akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, kuanzia shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia kiasi cha zaidi Sh 95 milioni, kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbali mbali na riba kutoka kwa kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa siyo kweli.

Katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadiawa kutenda kosa hilo, Juni 17, 2015 huko katika ofisi za TFF, ambapo kwa njia ya udanganyifu, mshtakiwa alijipayia Sh 10milioni kutoka TFF kwa kuonesha kuwa ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ha Jeck jambo ambalo siyo kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadai, kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, makao makuu ya Shirikisho hilo, alijipatia Sh 25milioni kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia, shtaka jingine utakatishaji fedha haramu, Mshtakiwa anadaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21 2015, alijipatia Sh 75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali na zimetokana na shtaka la kughushi.

Advertisement