Wambura arudi rumande hadi Machi 28

Thursday March 14 2019

 

By Fortune Francis

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura umedai upelelezi haujakamilika na uko hatua nzuri.

Wakili wa serikali Wankyo Saimon alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina, wakati kesi hiyo ilipotajwa.

"Mheshimiwa kesi hii imekuja kwaajili ya kutajwa, upelekezi haujakamilika, lakini umeshafikia hatua nzuri tunaomba tarehe nyingine kwaajili ya kutajwa," alidai Wakili Wankyo.

Baada ya Hakimu Mhina, kusikiliza maelezo hayo aliahirisha kesi hiyo hadi, Machi 28 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.

Mshtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Wambura alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza, Februari 11, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh 100milioni, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2019.

Katika mashtaka hayo 17; shtaka moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004, sehemu isiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Siku hiyo, Wambura kwa nia ya kutapeli alitengeneza barua ya kughushi ambayo haina kumbu kumbu namba akionyesha imeandikwa na E Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa  kampuni ya Jeck system anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka la kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, mshtakiwa  alitoa barua iliyokuwa haina kumbu kumbu namba  ya Julai 6, 2004, akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, kuanzia shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia kiasi cha zaidi Sh 95 milioni, kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbali mbali na riba kutoka kwa kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa siyo kweli.

Pia, katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadiawa kutenda kosa hilo, Juni 17, 2015 huko katika ofisi za TFF, ambapo kwa njia ya udanganyifu, mshtakiwa alijipayia Sh 10milioni kutoka TFF kwa kuonesha kuwa ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ha Jeck jambo ambalo siyo kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadai, kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, makao makuu ya Shirikisho hilo, alijipatia Sh 25 milioni kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia, shtaka jingine utakatishaji fedha haramu, Mshtakiwa anadaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21 2015, alijipatia Sh 75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali.

Advertisement