Wambura akosa dhamana kesi kuendelea Feb 14

Muktasari:

 

  • Katika mashtaka hayo 17, yanayomkabili Wambura; shtaka moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo, mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha kiasi zaidi ya Sh100milioni.

Wambura hakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Katika mashtaka hayo 17, yanayomkabili Wambura; shtaka moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo, mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa Serikali, George Barasa akisaidiana na Moza Kasubi na Imani Mitumezizi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Kelvin Mhina imedaiwa kuwa Wambura alikabiliwa na kesi ya Uhujumu uchumi namba 10/2019.

Barasa alidai katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004, sehemu isiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Barasa amedia siku hiyo ya tukio mshtakiwa Wambura kwa nia ya kutapeli alitengeneza barua ya kughushi ambayo haina kumbukumbu namba akionyesha imeandikwa na E Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Jeck system anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka la kutoa Nyaraka ya uongo imedaiwa, mshtakiwa alitoa barua iliyokuwa haina kumbukumbu namba ya tarehe 6/7/2004 akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck system ltd.

Akidai kuwa anadai mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, kuanzia shtaka la 3 hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia kiasi cha zaidi Sh95 milioni kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbalimbali na riba kutoka kwa kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa siyo kweli.

Moja mashtaka hayo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu imedaiwa, Juni 17.2015 huko katika ofisi za TFF kwa njia ya udanganyifu, Wambura alijipayia Sh 10Milioni kutoka TFF kwa kuonyesha kuwa ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ha Jeck jambo ambalo siyo kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Moza amedai kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014 huko katika ofisi za TFF mshtakiwa alijipatia Sh 25milioni kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Vile vile, katika shtaka jingine la utakatishaji fedha haramu, Mshtakiwa anadaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21 2015, alijipatia Sh 75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali na zimetokana na shtaka la kughushi.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa kesi hiyo imefunguliwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi na kwamba mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza.

Barasa alidai kuwa upelelezi katika kesi bado haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya upande wa mashtaka kumaliza kumsomea Wambura mashtaka yake, wakili wa utetezi Majura Magafu aliiomba mahakama kuitupilia mbali kesi hiyo kwa sababu mashtaka yote 17 hakuna shtaka hata moja lilolofunguliwa chini ya sheria ya uhujumi uchumi hivyo yalitakiwa yafunguliwe kama mashtaka ya kesi ya kawaida ya jinai ambayo yanamruhusu mshtakiwa kujibu.

Kufuatia hoja hiyo, Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 14 kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutolewa uamuzi.