Wambura afikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka 17

Muktasari:

  • Kumekuwa na sintofahamu kati ya Michael Wambura na mabosi wa TFF wakiongozwa na raisWallace Karia. Viongozi wa TFF wanadai Wambura si kiongozi wa Shirikisho hilo lakini kiongozi huyo alipinga na kufungua kesi mahakamani.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Makamu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na akikabiliwa na mashtaka 17, yakiwemo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na uhujumu uchumi.

Wakili kutoka Takukuru, George Baraza akisaidia na Iman Mitume, amedai mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa, mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 10/ 2019, kesi inaendelea sasa mahakamani.

Wambura amefikishwa mahakamani ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoa taarifa kuamua kuachana na masuala ya mpira wa miguu.

Kwa mujibu wa taarifa kwa waandishi wa habari iliyotolewa na Wakili Emmanue Muga anayemsimamia kazi zake.

Katika taarifa hiyo, Wambura ameamua pia kuondoa kesi iliyokuwa mahakamani. Kesi hiyo alifungua kwa ajili ya kukazia hukumu ya Mahakama juu ya uamuzi wa kufungiwa kwake na TFF hapo awali.

Hata hivyo katika taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Wambura hajabainisha sababu hasa ya kuchukua uamuzi huo.

Taarifa za hivi karibuni zilidaiwa kuwa Wambura alishikiliwa na Takukuru kutoka na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha alipokuwa madarakani.