Wamachinga: Haijawahi kutokea jezi Stars kuuzika hivi

Muktasari:

Mmoja wa wanunuzi wa jezi hiyo, Anna John alisema ameamua kununua jezi ya timu ya Taifa kwani anaamini kwa mechi ya leo ni zamu ya Tanzania na Stars hawatowaangusha. 

Dar es Salaam. Saa chache kabla ya mchezo wa kihistoria wa Taifa Stars na Uganda, mashabiki wa soka nchini wamechangamkia jezi za timu hiyo.
Wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga) walitumia fursa hiyo kuuza jezi za Taifa Stars kwenye eneo linalozunguka Uwanja wa Taifa huku wauzaji hao wakibainisha kuwa haijawahi kutokea jezi hizo kuuzika kwa kiwango kikubwa kama leo.
"Siwezi kusema nimeuza bei gani mpaka sasa, lakini leo hesabu inanifurahisha," alisema muuzaji wa jezi hizo aliyejitambulisha kwa jina la Athuman Rashid.
Alisema katika miaka miwili iliyopita kwenye mechi za Stars, hajawahi kufanya biashara kama alivyofanya leo.
Muuzaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Denis alisema kwa namna alivyopiga pesa kwa kuuza jezi hizo, anasubiri muda wa mechi ufike afunge biashara ili naye akaisapoti Stars ndani ya uwanja.
"Stars wamenipa mkwanja wa maana tu leo, hivyo na mimi lazima nikawasapoti," alisema.
Alisema fulana ya Stars moja anauza kati ya Sh 10,000, 15,000 na 20,000 kulingana na ubora wa jezi na hakuna anayeomba kupunguziwa bei.
Mmoja wa wanunuzi wa jezi hiyo, Anna John alisema ameamua kununua jezi ya timu ya Taifa kwani anaamini kwa mechi ya Leo ni zamu ya Tanzania na Stars hawatowaangusha.