Waliopita Azam wapania ushindi

Saturday August 17 2019

 

By Thobias Sebastian

ZIMESALIA saa chache tu kabla ya Simba na Azam kushuka Uwanja wa Taifa katika mechi ya Ngao ya Jamii, lakini mzuka walionao nyota wa Simba waliopita Chamazi ni kama wote wakitangaza wangependa kuibeba chama lao kupanda usiku wa leo.

Simba ina nyota sita waliowahi kuichezea Azam misimu ya nyuma akiwamo kipa Aishi Manula aliyetwaa ngao hiyo mara tatu, mbili akiwa na Simba ambapo alisema anatabiri mchezo mgumu kwa upande wao kwa vile Azam ni timu bora yenye uwezo wa kupata matokeo mazuri kama wao.

Mbali na Manula, Simba inao pia Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Pascal Wawa na nahodha John Bocco.

“Bado naendeleo na matibabu yangu kuwepo katika mchezo si rahisi, ila naamini wenzangu watatuwakilisha vizuri dhidi ya wapinzani wetu ambao nao watakuwa wamejiandaa kuanza vyema msimu,” alisema Manula.

Naye Kapombe, alisema miongoni mwa mechi ambazo zinatazamwa kuwa na ushindani mkubwa hapa nchini zinapokutana, ni Simba na Azam, kwa maana hiyo kazi kubwa na maandalizi mazuri ambayo timu itafanya ndio itakuwa silaha kubwa ya ushindi.

Kapombe alisema ni timu yake ya zamani lakini kwa sasa yupo katika kikosi cha Simba kwa maana hiyo akili yake ni kuhakikisha wanafanya vizuri kwa maana ya kupata ushindi na kuondoka na kombe hilo la kwanza msimu huu.

Advertisement

“Naona nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo huu kama tukichukua ubingwa utaongeza morali yetu ya kwenda kufanya vizuri tena zaidi ya msimu uliopita, lakini tutakuwa na tahadhari kwani Azam nao wana timu nzuri na watakuja kwa kuhitaji ushindi,” alisema Kapombe ambaye msimu uliopita alikuwa majeruhi nusu msimu.

Beki wa kushoto, Gadiel Michael alisema, “tunakwenda kukutana na timu ngumu na bora kuanzia katika benchi la ufundi mpaka wachezaji wao.

“Mechi ni ngumu lakini tumejipanga kupata matokeo mazuri dhidi yao katika mchezo huu.”

Nyota kiraka wa Simba mkongwe, Nyoni alisema katika fainali mbili ambazo Azam wamekutana nao msimu huu katika Kombe la Kagame na Mapinduzi zote walipoteza hivyo wanataka kulipa kisasi.

“Ni kweli tunakwenda kucheza mchezo mgumu dhidi ya timu nzuri ambayo tunahitaji kupata matokeo mazuri dhidi yao na kwa maandalizi na timu yetu ilivyo msimu huu nina imani kubwa hilo linawezekana na tutaanza kukusanya kombe letu la kwanza msimu huu kesho (leo),” alisema Nyoni.

Wawa na Bocco kila mmoja walisema wanasubiri dakika 90 kuamua mchezo, lakini kiu yao ni kuona wanauanza msimu mpya kwa kubebea tena ngao kama walivyofanya misimu miwili iliyopita na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara mara mbili mfululizo.

Hata hivyo, nyota wa Azam nao wamesisitiza kazi itamalizwa Taifa kwa sababu hata wao wanataka taji hilo ambalo wamelitwaa mara moja tu katika mechi tano walizowahi kucheza kwa misimu tofauti.

Timu hiyo ya Azam juzi usiku walituma salamu Msimbazi kwa kuwafyatua Namungo FC iliyopanda Ligi Kuu kwa mabao 8-1 katika mechi ya kirafiki ya kujipima nguvu.

Advertisement