Waliohamia Kirumba wazidi kutakata

Sunday October 04 2020
biashara utd pic

Achana na ushindi wa bao 1-0 walioupata Biashara United dhidi ya Mtibwa Sugar leo Jumapili Oktoba 4, 2020 ishu kubwa ilikuwa katika ndani ya uwanja kwa wachezaji walivyosakata kandanda safi na lenye ushindani.

Katika mchezo huo ambao umepigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, kila timu ilipambana kusaka pointi tatu na wenyeji Biashara United kuweza kujiongezea alama tatu muhimu.

Ikumbukwe kuwa Biashara United inatumia uwanja huo baada ya ule wa Karume Musoma kufungiwa na Bodi ya Ligi kwa madai ya kutokidhi vigezo.

Hata hivyo, CCM Kirumba imeonekana kuwa na neema kwa timu zilizochagua dimba hilo, kwani hata jana Gwambina ambao waliutumia kama wa nyumbani waliweza kuondoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ihefu.

Katika mchezo wa leo ilishuhudiwa kabumbu safi kutoka kwa timu zote, japokuwa Biashara United waliweza kushambulia haswa dakika za mwanzo na kufanikiwa kuandika bao kupitia kwa Kelvin Friday.

Mtibwa Sugar walitulia na kufanya mashambulizi lakini kipa Dan Mgore sambamba na mabeki wake wakiongozwa na Nahodha, Abdulmajid Mangalo waliweza kudhibiti hatari zote.

Advertisement

Biashara pamoja na kupata bao la mapema hawakutulia badala yake waliendeleza mashambulizi ya hapa na pale lakini Kipa wake Abdultwalib kufanya kazi nzuri ya kuokoa michomo.

Kwa matokeo hayo, Biashara United wanafikisha pointi 10 huku wapinzani wao wakibaki na alama zao tano baada ya timu zote kushuka dimbani mara tano katika Ligi Kuu.

Advertisement