Serengeti Boys : Wala hatuwadai ubingwa, tunawadai maendeleo yenu

Muktasari:

  • Katika mchezo wao wa mwisho, kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2019) dhidi ya Afrika Kusini uliofanyika Novemba 17, 2018 kwenye dimba la Soccer City jijini Johannesburg, kulikuwa na wachezaji watatu tu, kati ya wale walioshinda Kombe la Dunia la 2007, 2013 na 2015.

NIGERIA ndio mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Dunia U17. Walianza kushinda kombe hilo mwaka 1985, wakiifunga Ujerumani Magharibi kwa mabao 2-0. Wakarudia tena 1993 wakiifunga Ghana mabao 2-1.

Mwaka 2007 wakaifunga Hispania kwa penalti 3-0 kufuatia sare ya bila kufungana baada ya dakika 120. Mwaka 2013 wakaifunga Mexico mabao 3-0 na mwaka 2015 wakaifunga Mali kwa mabao 3-0.

Katika miaka 10 iliyopita ya mashindano (2007 hadi 2017), Nigeria imefika fainali mara nne, ikishinda ubingwa mara tatu na kupoteza mara moja kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Uswisi mwaka 2009.

Hii ina maana kwamba, katika kipindi hicho, Nigeria ilitawala dunia katika ngazi ya soka la vijana. Ilitarajiwa kwamba katika kikosi cha sasa cha Nigeria, kungekuwa na rundo la wachezaji waliotoka kwenye mashindano haya…lakini sio hivyo.

Katika mchezo wao wa mwisho, kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2019) dhidi ya Afrika Kusini uliofanyika Novemba 17, 2018 kwenye dimba la Soccer City jijini Johannesburg, kulikuwa na wachezaji watatu tu, kati ya wale walioshinda Kombe la Dunia la 2007, 2013 na 2015.

Wachezaji hao ni Isaac Ajayi anayechezea Watford ya England, aliyekuwepo kwenye kikosi cha 2013 sambamba na mwenzake Kelechi Iheanacho anayekipiga na Leicester City, pamoja na Samuel Chukwueze wa Villareal, aliyekuwemo kwenye kikosi cha 2015.

Kikosi cha Kombe la Dunia U17 huwa na wachezaji 21. Hii ina maana kwamba, katika misimu mitatu ambayo Nigeria ilishinda ubingwa, kulikuwa na wachezaji 63 lakini ni watatu pekee ambao waliitwa kwenye timu ya taifa katika mchezo ule.

Ubingwa wa mwaka 2007, ulipatikana kwa kuifunga Hispania iliyokuwa na David De Gea ambaye sasa yuko Manchester United, Asier Illaramendi - Real Sociedad (akipita Real Madrid), Nacho - Real Madrid n.k. Hawa wote bado wanaendelea kuitumikia timu ya taifa ya Hispania, lakini Nigeria hayupo hata mmoja.

TATIZO LIKO WAPI?

Kinachoigharimu Nigeria ndicho kilichowatesa vijana wetu wa Serengeti Boys baada ya kipigo cha 5-0 kutoka kwa Uturuki kwenye mashindano ya UEFA ASSIST mjini Antalya. Shukrani kwa Azam TV kutuoneshea mbashara mechi za vijana wetu.

Katika mchezo wao wa mwisho, Serengeti Boys walifungwa 5-0 na Uturuki, siku iliyofuata vikaanza kutembea vipande vya video vya baadhi ya wachezaji wakijikebehi kutokana na kipigo hicho. Vijana hao ni kama walikuwa wakitafuta huruma kwamba wasilaumiwe kwa kipigo kile kwa sababu waliocheza nao walikuwa bora kuliko wao. Walijihisia wamewaangusha Watanzania hivyo wanataomba msamaha.

Ninyi watoto, UEFA Assist haikuwa na lengo la kutafuta bingwa bali kupima maendeleo yenu, mnaotarajiwa kushiriki au watakaoshiriki Kombe la Dunia la baadaye mwaka huu. Ndiyo maana hakukuwa na robo fainali, nusu fainali wala fainali…kila timu ilicheza mechi tatu na kurudi kwao.

Mashindano ya vijana, chini ya miaka 17, huwa hayana malengo ya ‘kupambana kwa namna yoyote na kushinda ubingwa’. Haya ni mashindano ya kutathmini maendeleo ya vijana katika kushika mafunzo ya walimu wao, kuelekea ukomavu wao. Tusidhani Brazil, Argentina, Ujerumani au Hispania hawawezi kupambana na kushinda ubingwa huu, hapana. Hayo sio malengo. Watoto wa chini ya miaka 17 wanatakiwa kucheza na kupimwa maendeleo yao namna wanavyoweza kufuata maelekezo ya walimu wao, bila kujali matokeo.

Kama itatokea wakashinda, ni dawa, wakishindwa, ni sawa…mwalimu aliye makini, atakerwa na vijana wake hata kama wameshinda lakini hawakufuata maelekezo yake. Na atafurahishwa na vijana wake, hata kama watashindwa lakini walicheza kwa kufuata maelekezo yake. Akili za vijana wetu wa Serengeti, bila shaka hata wanaowasimamia., ndizo zinazoigharimu Nigeria, na hata mataifa mengine yenye mitazamo hiyo. Wanapoenda kwenye mashindano kama haya, wanakwenda kupambana ili wawe mabingwa. Wakiukosa, ndio wanateseka sana.

Wenzetu wanapeleka vijana wao kuwapima maendeleo…baada ya miaka mitano, wanakuwa wamekomaa huku wakwetu walioenda kushindana, wanakuwa wameduamaa.

Tuwasaidie vijana wetu kwamba hatuwadai ubingwa, tunawadai maendeleo yao.