Wakongwe wafunguka rekodi kuvunjwa

Muktasari:

  • Nyota mwingine ambaye alitoa pasi kwa Peter Tino kwenye mchezo wa kufuzu Afcon mwaka 1980, Hussein Ngulungu alisema kilichopo sasa ni rekodi yao kusahaulika na kuangalia nini ambacho Stars inapaswa kufanya Afcon msimu huu.

BAADA ya juzi Jumapili Taifa Stars kuvunja rekodi ya miaka 39 kwa kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), nyota waliowahi kuiwakilisha nchi kwenye fainali hizo wamepongeza wachezaji hao kufuzu.

Kufuzu kwa timu hiyo kumepokewa kwa hisia tofauti na wachezaji wa zamani wa timu hiyo ambao waliiwakilisha Tanzania kwenye Afcon ya kwanza ya 1980.

Kwa nyakati tofauti jana Jumatatu na juzi Jumapili wachezaji hao walisema ushindi wa Stars umewapunguzia mzigo. “Miaka yote ilikuwa ikizungumzwa ushiriki wetu Afcon tunatajwa sisi, lakini sasa rekodi yetu imepita,” alisema Mtemi Ramadhan.

Alisema, alifurahi baada ya kuona Stars imevunja rekodi hiyo, lakini alishauri mikakati ya kuelekea kwenye mashindano ianze sasa.

“Yale mashindano ni magumu, nimefuatilia timu zilizofuzu, hakuna nyepesi hata moja, Stars wanapaswa kujipanga tunafahamu sawa kutwaa kombe hawawezi lakini wasitolewe mwanzoni, wapambane wafuzu japo kucheza robo fainali,” alisema Mtemi.

Nyota mwingine ambaye alitoa pasi kwa Peter Tino kwenye mchezo wa kufuzu Afcon mwaka 1980, Hussein Ngulungu alisema kilichopo sasa ni rekodi yao kusahaulika na kuangalia nini ambacho Stars inapaswa kufanya Afcon msimu huu.

Japo Ngulungu alieleza kutamani Rais Magufuli jana angewaalika wachezaji wote wa Stars walifuzu sasa na wale wa waliocheza Afcon ya 1980 alisisitiza, ushindi wa juzi dhidi ya Uganda umewapa faraja.

“Tulikaa muda mrefu bila kuonja ladha ya fainali hizo, sasa tuna tiketi mkononi, hiyo ni faraja kwetu, ingawa pia ningemuomba Rais kutufikiria wachezaji wote tuliocheza Afcon ya kwanza, atupe fursa ya kuzungumza na sisi,” alisema.

Kipa wa zamani wa timu hiyo, Iddi Pazi alisema; “TFF ilituchukua wachezaji wa zamani kwa ajili ya kuhamasisha ili tushinde, hivyo niwaombe katika harakati za kuelekea Misri wasitupe kisogo, tuendelee kushirikiana na ninaamini tutafanya vizuri pia huko,”

Alisema Stars ina uwezo wa kufika mbali kwenye mashindano hayo japo aliungana na Mtemi kusisitiza kuwa uwezekano wa kutwaa kombe hautokuwepo.

“Waende wakapambane, wasikubali kufunga mechi zote, hiyo itakuwa heshima kwao na kwa taifa pia, cha msingi waanze maandalizi sasa,” alisema.