NYUMA YA PAZIA: Wako wapi wale mastaa wa zamani wa mikoani?

Tuesday May 19 2020

 

By EDO KUMWEMBE

NAKUMBUKA kumuona mshambuliaji aliyeitwa Idefonce Amlima akiwa katika ubora wake na timu ya Bandari - Mtwara mwanzoni mwa miaka ya 1990. Wakati huo nilikuwa Mtwara. Idefonce alikuwa staa hasa. Alikuwa staa ndani na nje ya uwanja.

Watoto wa Mtwara waliathirika na ustaa wa Amlima. Uwanjani walikuwa wakikimbia wakikunja mikono kama yeye. Nje ya uwanja walitamani kumgusa. Walikuwa wanatembea kama yeye. Kwa sababu Amlima alikuwa Mkatoliki na alipenda kuvaa rozari, kuna vijana walikuwa wanavaa rozari kumuiga.

Amlima alikuwa staa ndani ya uwanja. Alifunga karibu kila mechi. Simba ikiwa katika ubora wake iliwahi kulala mabao 3-2 uwanja wa Umoja (siku hizi Nangwanda Sijaona). Amlima alifunga mabao mawili. Ile ilikuwa Simba hasa.

Yanga ikiwa katika ubora wake iliwahi kushinda mabao 2-1. Lakini kwamba Amlima alitangulia kuifungia Bandari bao la kuongoza. Timu zote ambazo zilikuwa zinakwenda Mtwara zilikuwa zinamzunguzia Amlima. Alikuwa kioo cha Mtwara. Alama ya Mtwara. Alama ya timu ya Bandari.

Pindi ambapo mchezaji wa hadhi ya Amlima alikuwa akihama timu, basi mkoa mzima unazizima. Pengo lake linakuwa wazi ndani na nje ya uwanja. Timu inaanza kukosa ushawishi kwa sababu staa hayupo. Hata wakati anacheza halafu akapewa kadi nyekundu au kuumia basi ijayo uwanja unakuwa mpweke.

Zamani tulikuwa na wachezaji mastaa wa mikoani. Sijui siku hizi wamekwenda wapi. Ustaa kama huu wa Meddie Kagere kuna mchezaji alikuwa nao mkoani kwake. Si kwa bahati mbaya, bali kwa ufungaji wake mabao na ushawishi mkubwa katika timu.

Advertisement

Ukienda Morogoro unakutana na David Mihambo. Ukienda Dodoma unakutana na Mohamed Mbuguni. Ukirudi Mbeya unakutana na Jimmy Morerd na Tukuyu Stars yake. Kule Tanga kulikuwa na mastaa wengi hasa Coastal Union na African Sports.

Katika Coastal usingeweza kumtaja Juma Mgunda peke yake. kulikuwa na akina Razak Yusuph ‘Careca’, Hussein Mwakuruzo, Ally Maumba na wengineo. Hata hivyo Mgunda alikuwa mtu wa kuogopwa zaidi kwa sababu timu ilikuwa inamlisha zaidi yeye na hakuwaangusha.

Ukiniuliza sababu mojawapo ya mashabiki kutokwenda uwanjani hii inaweza kuwa sababu. Kuna kitu kimepotea katika timu za mikoani. Kuna moyo umepotea katika soka letu la mikoani. Timu zimeshuka hadhi lakini hata mastaa wa mikoani wameshuka hadhi.

Zamani ulikuwa unakwenda uwanjani sio tu kutazama mastaa wa Simba au Yanga. Hapana. Ungeweza kwenda uwanjani kwa ajili ya kutazama mastaa wa upande wa pili. Hata klabu za mikoani zingefika uwanjani kuna mashabiki walikuwa wanajitokeza kuwatazama mastaa wa mikoani.

Pamba ya Mwanza ingefika Dar es salaam basi mashabiki walikuwa na hamu wa kumtazama Fumo Felician. Walikuwa wana hamu ya kumtazama Kitwana Suleiman. Walikuwa ni mastaa ambao walikuwa wanawasikia pia wakiwa wanatesa katika viwanja vingine au mkoani kwao.

Nini kilisababisha haya? Mastaa walikuzwa na redio au? Walikuzwa na uwezo wao? Kwanini sasa hali hii haipo tena? Leo tunakwenda uwanjani hatujui ni mchezaji gani wa kuchungwa zaidi katika kikosi cha Ndanda.

Tunakwenda uwanjani kwa ajili ya kumtazama Benard Morrison lakini hatujui upande wa pili kuna mchezaji gani wa kuchungwa zaidi. Hatujui nani ni mchezaji wa kuchungwa zaidi katika kikosi cha Mwadui. Hili sio tatizo dogo sana kama tunavyofikiri.

Tukitazama kwa wenzetu wao bado wamebakiza hali hii. Ligi Kuu ya England kuna mastaa wa timu ambao ni vioo na ambao unajua wanaweza kufanya lolote, muda wowote, wakiwa nyumbani au ugenini.

Ukienda Leicester City unakumbana na Jimmy Vardy, ukienda Norwich unakumbana na Temu Pukki, ukienda Everton unakumbana na Richarlison. Wenzetu bado wanatengeneza mastaa wao kwa kiwango kile kile ambacho sisi tunatengeneza.

Na kwa kujua jinsi gani ambavyo mpira umeanguka, hawa mastaa wakati mwingine walikuwa wanashindwa kupata nafasi kwa sababu Simba na Yanga zilikuwa na wachezaji wakali katika nafasi zao. Haishangazi kuona Kitwana Suleiman aliishia Pamba, Jimmy Morerd aliishia Tukuyu.

Mastaa wa kileo wa timu za mikoani wanafunga mechi moja kubwa kisha wanapotea. Wakati mwingine wanasajiliwa na timu za mjini lakini wanashindwa kuonyesha makali yao. Turudi nyuma na kujiuliza kwanini timu za mikoani na wachezaji wa mikoani hawana hadhi kama zamani. Tumekosea wapi?

Mashabiki wa zamani walikuwa na imani na timu zao za mikoani. Walikuwa wanakwenda uwanjani wakitazamia ushindi dhidi ya timu yoyote ile. Lakini zaidi walikuwa wana matumaini makubwa na mastaa wao.

Mastaa wao pia walitengenezewa uadimu uliopitiliza. Mchezaji ni wa mkoani lakini ana hadhi kama ya Kagere. Siku hizi hali imekuwa tofauti kwa kiasi kikubwa na haishangazi kuona viwanja havijazi. Mvuto upo katika mechi kubwa tu kwa sababu mashabiki wanajua watamuona Kagere au Morrison.

Kama tukiulizana namna ya kurudi kule tulikotoka nadhani jibu linaweza kuwa moja tu. Klabu nyingine za Ligi Kuu ziongezewe uwezo wa kipesa. Tutafanyaje? Wengine wanaweza kutupa mwongozo. Timu za mikoani zinahitaji kuwa na mastaa wakubwa. Ama wa kuwanunua kutoka nje, au wale wa kuwatengeneza nyumbani na kisha wakafanikiwa kuwabakiza kwa miaka yote huku wakitamba.

Huwa najiuliza, ilikuwaje Coastal Union wakafanikiwa kumbakiza Juma Mgunda kwa miaka yote mpaka akastaafu soka akiwa na Coastal Union huku wote tukimkubali. Na zaidi ni kwamba Mgunda alikuwa pia mchezaji wa timu ya taifa. Kwa nini hali hiyo haitokei sasa hivi? Tujiulize.

Advertisement