Wako wapi mastaa waliocheza na Kompany mechi ya kwanza Man City 2008

Thursday May 23 2019

 

LONDON,ENGLAND.BEKI wa kati, Vincent Kompany ameamua kuzifikisha mwisho zama zake za kuichezea Manchester City baada ya kudumu kwenye kikosi hicho kwa miaka 11.

Kompany ametangaza kuachana na Man City mwishoni mwa msimu huu na sasa anakwenda kuwa kocha mchezaji katika timu yake ya zamani ya RSC Anderlecht huko Ubelgiji.

Kapteni huyo wa Etihad, ameshinda mataji 10 makubwa kwa muda wake aliokuwa Man City na msimu huu ameondoka hapo akiwa amenyakua mataji matatu makubwa ya ndani huko England kwa maana ya ubingwa wa Kombe la Ligi, Kombe la FA na Ligi Kuu England.

Kompany mwenye umri wa miaka 33 kwa sasa, alinaswa na Man City mwaka 2008 kabla ya timu hiyo kununuliwa na bilionea wa Kiarabu, Sheikh Mansour na amekuwa moja ya msingi bora kabisa wa kuijenga timu hiyo ya Etihad.

Beki Kompany mechi yake ya kwanza kuichezea Man City ilikuwa kwenye ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya West Ham United, Agosti 2008 na hawa ndio wachezaji walianzishwa kwenye kikosi cha kwanza cha Man City katika mechi yake ya kwanza staa huyo wa Kibelgiji.

Hiki hapa kikosi cha Man City kilivyopangwa katika mechi ya kwanza ya Kompany katika timu hiyo mwaka 2008.

Advertisement

Joe Hart

Kocha Pep Guardiola hakufurahishwa na kipa namba moja wa Man City wakati anatua Etihad mwaka 2016 na haraka sana alimtoa kwa mkopo kwenda Torino. Kipindi hicho kipa alikuwa Joe Hart, ambaye ndiye aliyekuwa golini wakati Kompany anacheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha Man City. Hart baada ya kuondoka Torino alikwenda kujiunga na West Ham United kabla ya kunaswa na Burnley mwaka jana.

Kipa huyo mwenye umri wa miaka 32 amecheza mechi 21 kwenye kikosi cha Burnley msimu huu.

Vedran Corluka

Baada ya kutamba Ligi Kuu England kwa miaka mitano akianzia huko Man City kisha Tottenham Hotspur, Vedran Corluka aliondoka zake jumla mwaka 2012 na kwenda kujiunga na kikosi cha Lokomotiv Moscow huko Russia. Tangu kipindi hicho Corluka anacheza soka lake huko Russia akishinda makombe mawili ya ndani. Corluka mwenye umri wa miaka 33 kwa sasa naye alikuwamo kwenye kikosi cha Man City alizocheza Kompany kwa mara ya kwanza huko Etihad.

Micah Richards

Micah Richards alikuwa staa wa England wakati Kompany akitua Man City na mengi sana yalitarajiwa kuhusu Mwingereza huyo. Kipindi hicho, Richards alikuwa na umri wa miaka 20 tu na kulikuwa na imani beki huyo angekuja kuwa staa mkubwa sana baadaye.

Alishinda ubingwa wa Kombe la FA mwaka 2011 na alibeba taji la Ligi Kuu England mwaka uliofuatia. Lakini, baadaye, Richards alishindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha Man City na kutolewa kwa mkopo Fiorentina na baadaye akabebwa jumla na Aston Villa mwaka 2015.

Hakucheza mechi yoyote tangu Oktoba 2016 huku mkataba wake na Aston Villa ukifika tamati mwishoni mwa msimu huu.

Tal Ben-Haim

Ben-Haim alicheza mechi tisa tu za Ligi Kuu akiwa na kikosi cha Man City katika msimu pekee aliokuwa katika kikosi hicho. Lakini, alikuwa mmoja kati ya wachezaji walioanzishwa katika kikosi cha Man City wakati Kompany alipocheza mechi ya kwanza kwenye timu hiyo ambapo waliichapa West Ham United Bao Tatu. Kwa sasa akiwa na umri wa miaka 37 anachezea klabu ya Beitar Jerusalem, ikiwa ni timu yake ya 10 kucheza katika maisha yake ya kisoka. Ben-Haim alicheza mechi chache sana England, lakini bado jina lake limebaki kuwa juu kwenye ligi hiyo.

Michael Ball

Alisajiliwa kutoka PSV Eindhoven mwaka 2007. Michael Ball alicheza mechi 48 kwenye Ligi Kuu England akiwa na Man City kwa misimu yake miwili aliyodumu na timu hiyo kabla ya kuachwa aondoke.

Alikwenda kufanya majaribio huko Wigan Athletic na Blackpool kabla ya kwenda kucheza kwa miezi sita katika kikosi cha Leicester City. Maisha yake ya mpira yalikatishwa mapema kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti. Lakini, Ball alikuwamo uwanjani wakati Kompany alipocheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha Man City.

Stephen Ireland

Katika msimu wake wa kwanza Kompany huko Man City, kiungo Stephen Ireland ndiye aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka katika kikosi hicho. Ireland alicheza mechi 138 za ligi akiwa na Man City kabla ya kuondoka mwaka 2010 kwenda kujiunga na Aston Villa. Kisha alicheza kwa mkopo Newcastle na Stoke City kabla ya kujiunga na timu hiyo jumla. Staa huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Ireland alinaswa na Bolton msimu uliopita, lakini aliondoka bila ya kucheza mechi yoyote katika kikosi hicho.

Vincent Kompany

Kompany katika mechi yake ya kwanza Man City alicheza kwenye sehemu ya kiungo. Kipindi hicho kocha alikuwa Mark Hughes, ambaye baadaye alikuja kumbadilisha na kumtumia kwenye beki ya kati. Alipokuja Kocha Roberto Mancini aliendelea kumtumia Kompany kwenye beki ya kati kuanzia Desemba 2009. Mbelgiji huyo alishinda taji lake la kwanza kati ya 10 katika timu hiyo wakati alipobeba Kombe la FA mwaka 2011 na anaondoka kwenye kikosi hicho mwaka huu akiwa amekiongoza kupata mataji matatu makubwa, Kombe la Ligi, Kombe la FA na Ligi Kuu England. Kompany sasa anakwenda kuwa kocha mchezaji kwenye klabu yake ya zamani ya Anderlecht.

Michael Johnson

Michael Johnson, kama ilivyokuwa kwa Micah Richards, alikuwa kinda matata kabisa akitokea kwenye akademia ya timu hiyo, akiaminika angekuja kuwa mchezaji mkubwa sana katika kikosi cha Man City kwa siku za baadaye. Lakini, majeraha yalitibua maisha ya kiungo huyo ambapo aliishia kucheza mechi 37 tu za ligi katika kipindi cha miaka sita.

Mara yake ya mwisho alikuwa kwa mkopo huko Leicester City katika msimu wa 2011/12. Kwa sasa ana umri wa miaka 31 na hajawahi kupata timu nyingine ya kuchezea tangu wakati huo. Lakini, kipindi Kompany anacheza mechi yake ya kwanza Man City, Johnson alikuwa fundi wa mpira.

Martin Petrov

Matrin Petrov aliitumikia Man City kwa misimu mitatu kipindi hicho kuanzia ikiwa chini ya Kocha Mark Hughes na baadaye alipokuja Roberto Mancini mwanzoni mwa zama za matajiri wa Abu Dhabi. Staa huyo wa Bulgaria alikuwa bonge la mchezaji ndani ya uwanja, lakini ilipofika mwaka 2014 aliamua kutimisha maisha yake ya soka akiwa kwenye kikosi cha CSKA Sofia.

Wakati Kompany akicheza mechi yake ya kwanza, Petrov alikuwa kwenye winga akiwakimbiza mabeki wa West Ham United na kushinda mchezo huo.

Elano

Fundi wa mpira kutoka Brazili, Elano alifunga mara mbili katika mechi ya kwanza ya Kompany katika kikosi cha Man City. Kwenye kikosi hicho, Elano akitokea kwenye sehemu ya kiungo alifunga mabao 18 katika mechi 80 kabla ya kwenda kujiunga na Galatasaray mwishoni mwa msimu wa 2008-09. Baada ya hapo alikwenda kuichezea Santos (mara mbili), Gremio, Flamengo, na Chennaiyin FC huko India kabla ya kutangaza kustaafu soka mwaka 2017.

Elano alikuwa nyota wa mchezo wakati Kampany anacheza mechi yake ya kwanza huko Man City.

Daniel Sturridge

Straika Daniel Sturridge alifunga mara nne katika mechi 26 alizocheza msimu wa 2008/09 na alichaguliwa kuwa Kinda Bora wa Mwaka wa Man City kwa wakati huo kabla ya kwenda kujiunga na Chelsea mwishoni mwa msimu.

Kwenye kikosi cha Chelsea, Sturridge alicheza mechi 63 za ligi kwa kipindi cha miaka minne, huku mechi 12 akicheza kwa mkopo huko Bolton mwaka 2011.

Baada ya hapo alikwenda kujiunga na Liverpool ambako kwanza aliunda safu matata ya ushambuliaji sambamba na Luis Suarez.

Baadaye akatolewa kwa mkopo kwenda West Brom mwaka jana huku akitarajia kuondoka Anfield mwishoni mwa msimu huu.

Advertisement