Wakitua England huko kwingine watawaambia watu nini !

Thursday January 10 2019

 

LONDON,ENGLAND.ACHANA na Kylian Mbappe, Neymar na Lionel Messi hao ndio kabisa kama wakiamua kutua kwenye Ligi Kuu England basi itakuwa balaa.

Ligi Kuu England imekuwa na mvuto kwa watazamani wake kutokana na kuwa na kundi kubwa la wachezaji wenye viwango bora, tofauti na ilivyo kwenye ligi nyingine, ambazo wachezaji matata wenye mvuto mkubwa ni wachache.

Wakati Ligi Kuu England ikiwa na mvuto kwa sasa, bado kuna kundi kubwa la wachezaji wanaotajwa kwamba huenda wakajiunga na ligi hiyo kama sio sasa basi baadaye na hilo likitokea, basi Ligi Kuu England itakuwa balaa kwa kuwa na mvuto pengine kuliko ligi nyingine kubwa za Ulaya, La Liga, Bundesliga, Serie A na Ligue 1.

Kilichopo kwa sasa hata wachezaji wenyewe wamekuwa na hamu ya kwenda kucheza kwenye Ligi Kuu England ikiwamo mastaa kibao kama Ivan Perisic wa Inter Milan.

Adrien Rabiot (PSG)

Kiungo wa Kifaransa, Rabiot aliweka wazi mwezi uliopita kwamba hataongeza mkataba mwingine wa kuendelea kuitumikia timu yake ya Paris Saint-Germain baada ya huu wa sasa kufika kikomo.

Staa huyo yupo kwenye miezi yake michache ya mwisho ya kumaliza mkataba wake kwenye kikosi hicho na hakika amekuwa mmoja wa wachezaji wanaowindwa na klabu nyingi vigogo huko Ulaya. Kwenye Ligi Kuu England kuna timu kadhaa pia zinahaha kupata saini yake, ikiwamo Chelsea, Manchester United na Tottenham.

Kokote atakapoamua kwenda Rabiot moja kwa moja kutazidisha mvuto wa kuitazama Ligi Kuu England kutokana na uhodari wa mchezaji huyo ambaye ana mashabiki wake kibao wanaomfuatilia huko Ufaransa.

Ousmane Dembele (Barcelona)

Tangu alipotua Nou Camp, Dembele amekuwa si mchezaji mwenye uhakika sana wa kupata namba kwenye kikosi cha kwanza na jambo hilo linamfanya afikirie kuachana na timu hiyo na kutimkia kwingineko ambako atapata muda wa kucheza. Paris Saint-Germain inatajwa kuhitaji huduma yake, lakini kwenye mchakato huo vigogo wengine wa England wamekuwa wakihitaji saini yake, ikiwamo Arsenal ambao wanahitaji kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Hakuna ubishi, Dembele ni mchezaji mwenye mashabiki wake, hivyo akitua kwenye Ligi Kuu England ataleta mvuto mkubwa kwenye ligi hiyo na kuwavutia zaidi watazamaji wake kutoka katika pande zote za dunia.

Nicolas Pepe (Lille)

Kwenye Ligi Kuu Ufaransa, Nicolas Pepe ni mmoja wa wachezaji wanaotamba kwelikweli na kufanya vyema akiwa na kikosi cha Lille msimu huu. Kiwango chake bora kimemfanya staa huyo wa kimataifa wa Ivory Coast, mzaliwa wa Paris, Ufaransa kuzivutia klabu kadhaa zinazohitaji huduma yake hasa huko kwenye Ligi Kuu England ambapo mahasimu wawili wa London, Chelsea na Arsenal wameonyesha dhamira ya dhati kabisa ya kutaka huduma ya winga huyo.

Pepe ni mchezaji anayewindwa na timu nyingi na hakika kama ataondoka Ufaransa basi atakuwa amepunguza uhondo kwenye ligi na kuja kuuleta England, ambako mashabiki watazidi kupata burudani matata kutoka kwa wachezaji wa maana wanaotamba huko Ulaya.

Edinson Cavani (PSG)

Wanasema mambo ni moto huko kwenye Ligi Kuu England. Klabu vigogo kwenye ligi hiyo vinajaribu kuchuana kuleta wachezaji wa maana ili kuhakikisha mchakamchaka wa kuwania ubingwa unakuwa na utamu wake kila kona.

Kwenye majina ya mastaa matata kabisa yanayotajwa kwenye mpango huo moja wapo ni la Edinson Cavani, ambaye anadaiwa kuwa kwenye rada cha kocha Maurizio Sarri huko Stamford Bridge.

Sarri anataka kuongeza nguvu kwenye safu yake ya ushambuliaji, hivyo anaamini kuipata huduma ya mshambuliaji huyo wa Paris Saint-Germain itakuwa moja ya hatua kubwa sana katika kuifanya The Blues timu ya kuogopwa kwenye Ligi Kuu England.

Emiliano Sala (Nantes)

Ripoti ni kwamba Cardiff City wametenga kiasi cha Pauni 20 milioni kwa ajili ya kumnasa staa wa Nantes, Emiliano Sala. Wanafahamu kwamba kwa pesa hiyo itawashawishi Nantes kufanya biashara ya kumwachia mchezaji huyo.

Hakika Sala ni bonge la mshambuliaji ambapo suala la kufunga halijawahi kuwa tatizo kwa upande wake. Kwenye Ligi Kuu Ufaransa ameonyesha uwezo huo licha ya kucheza kwenye vikosi vya kawaida sana ambazo vimekuwa havina uwezo wa kupambana kushindania ubingwa.

Huduma yake inawindwa na klabu kadhaa za England ikiwamo Brighton, Crystal Palace, Cardiff, Fulham na Southampton.

Nabit Fekir (Lyon)

Ishu iliyopo ni kama Liverpool watarudi tena mezani kutaka huduma ya kiungo mshambuliaji wa Ufaransa, Nabil Fekir baada ya dili la kumnasa staa huyo wa Olympique Lyon kukwama mwaka jana kwenye dirisha la majira ya kiangazi.

Mchezaji huyo bado yupo kwenye rada za timu hiyo na nyinginezo kwenye Ligi Kuu England ambazo zimekuwa zikihitaji huduma yake. Rais wa Lyon, Jean-Michel Aulas alisema hakuna kinachoshindikana kwenye kumuuza mchezaji huyo kwani kinachotakiwa ni pesa tu. Chelsea wanamtaka staa huyo.

Mario Balotelli (Nice)

Kinachoelezwa ni hivi, Nice imekuwa na mpango wa kuachana na mshambuliaji, Mario Balotelli baada ya Mtaliano huyo kushindwa kufunga kwenye dakika 752 alizocheza kwenye Ligue 1 msimu huu.

Kocha Patrick Vieira huko Nice amekuwa hana uhusiano mzuri na mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kukipiga kwenye Ligi Kuu England. Balotelli anahusishwa na mpango wa kurudi England, huku Newcastle United na West Ham United zikitajwa kumtaka fowadi huyo.

Gonzalo Higuain (Milan)

Kilichopo ni kwamba Chelsea wanacheki uwezekano wa kuinasa huduma ya mshambuliaji wa Kiargentina, Gonzalo Higuin ili kuja kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Chelsea wamekuwa na shida kubwa kwenye ufungaji na kwamba Eden Hazard asipofanya hivyo tu basi imekuwa majanga maana Alvaro Morata na Olivier Giroud wote hawafungi, wamepoteza viati vyao vya kufungia. Kama usajili wa Higuian utakamilika basi Ligi Kuu England itakuwa imeshuhudia nyota mwingine matata kabisa katika ligi hiyo na hivyo kuzidi kuongeza mvuto wa ligi hiyo kutazamwa kila kona katika duniani hii.

Isco (Real Madrid)

Mengi yanasemwa kuhusu maisha ya kiungo fundi wa mpira wa Kihispaniola, Isco huko Real Madrid. Mambo ya staa huyo yamedaiwa kuwa katika wakati mgumu chini ya kocha Santiago Solari na ndio maana kwa sasa anachofikiria kwenye akili yake ni kuachana na wababe hao wa Bernabeu itakapofika mwishoni mwa msimu huu. Kilichopo ni kwamba kama Isco ataamua kuondoka zake Real Madrid, basi mahali ambako amelenga kwenda ni kwenye Ligi Kuu England, ambako kuna timu kadhaa zinahaha kupata huduma yake kama vile Liverpool, Arsenal na Tottenham Hotspur. Ni jambo la wazi kabisa, Isco akitua kwenye Ligi Kuu England, mvuto wa ligi hiyo utaongezeka zaidi.

Philippe Coutinho (Barcelona)

Kiungo wa Kibrazili, Philippe Coutinho ndio kwanza ana mwaka mmoja tu tangu alipojiunga na Barcelona Januari mwaka jana. Lakini, tayari staa huyo amekuwa akihusishwa na mpango wa kurudi kwenye Ligi Kuu England, huku safari hii Manchester United wakiripotiwa kutaka huduma yake. Coutinho alikuwa kwenye kikosi cha Liverpool wakati anaondoka kwenda Barcelona, hivyo kama ataamua kurudi kwenye Ligi Kuu England na kisha kujiunga na Man United basi jambo hilo litamfanya ajitengenezee uadui mkubwa na Liverpool kutokana na upinzani uliopo baina ya timu hizo mbili. Coutinho akirudi England, kisha akatua Old Trafford, Ligi Kuu England itakuwa balaa.

Advertisement