Wakishinda! Nyota Yanga kuvuna Sh17 milioni, Simba Sh15 milioni

Muktasari:

Mastaa wawili za zamani wa timu za Simba na Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ na Ally Mayay wamesema mechi hiyo haiamuliwi kwa rekodi.

TAMBO kibao, mbwembwe kibao lakini ubishi unamalizwa leo saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, timu za Simba na Yanga zitakapopambana kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA). Huko kwenye vibandaumiza wanasema “Mwana kulitaka mwana kulipata, mnalo hilo.”

Ni mechi ambayo itashuhudia mabadiliko makubwa ndani na nje ya uwanja. Ndani vikosi vimepanguliwa na kupangwa kimkakati zaidi, lakini nje sehemu kubwa ya majukwaa itakuwa wazi. Zile kelele za nyomi la watu hazitakuwepo.

Ni mechi ngumu ambayo lazima mshindi apatikane iwe ndani ya dakika 90 au kwenye matuta ili akacheze fainali ya FA.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael amesisitiza kwamba kwa jinsi alivyokisuka kikosi chake mashabiki wategemee matokeo ya kushangaza, huku Sven Vandebroeck wa Simba akisema mechi hiyo ni lazima washinde na itakuwa na burudani ya aina yake.

KAMBINI YANGA

Eymael alisema: “Tunaelewa ubora wa Simba kwenye kushambulia, lakini tunajua jinsi ya kuwadhibiti. Nimekaa sana na wachezaji wangu nikawajenga vizuri kiakili tayari kwa mchezo huu. alisema eyamel. “Tumeangalia mpaka video kujua ubora na udhaifu wao, ni timu nzuri kwenye kushambulia na inao wachezaji wazuri lakini tuna matokeo, kwa maelekezo ambayo nimewapatia (wachezaji wangu) tutawashangaza watu kwa matokeo kama ilivyokuwa katika mechi iliyopita.”

Alisema katika kikosi chake kutakuwa na mabadiliko makubwa kuanzia wachezaji wenyewe mpaka aina ya uchezaji ili kumaliza mchezo huo muhimu mapema kwa vile wanahitaji ushindi ili kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Yanga ambayo kwa msimu mzima imekuwa ikitumia Hoteli ya Regency Dar es Salaam kama sehemu ya kuweka kambi, baada ya kurejea kutoka Bukoba wachezaji walihamishiwa kwenye hoteli yenye hadhi ya nyota tano ya Western ili kujiweka sawa kisaikolojia kwa mchezo huo muhimu.

Kiuhalisia ni kwamba Yanga ndio wanahitaji zaidi ushindi katika mchezo huo katika kujihakikishia kutinga fainali ya Kombe la FA ambapo kiu yao kubwa ni kuhakikisha wanakata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa msimu ujao.

Lakini Simba wanataka kufuta gundu la kupoteza pointi mbele ya Yanga katika mechi mbili zilizopita. Yanga ambayo kwenye mchezo wa leo itamkosa winga Mapinduzi Balama ambaye amevunjika mfupa mdogo katika mguu wa kushoto na kuvishwa hogo, lakini nahodha Papy Tshishimbi atacheza dakika 45 tu kwa vile bado hajawa fiti.

Kocha Eymael amefichua kwamba kuna zaidi ya asilimia 50 za kiungo huyo pamoja na beki wake wa kulia, Juma Abdul kuwa sehemu ya mchezo huo.

Abdul na Haruna Niyonzima hawakutumika katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar ambao Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Benard Morrison.

Kuhusu kurejea kwa Morrison kikosini, Eymael alisema kumeongeza nguvu na ana imani kuwa makali yake ataendelea kuyaonyesha katika mchezo huo licha ya sakata lake na Yanga lililotokea siku chache zilizopita na kuzua gumzo kwa mashabiki wa timu hiyo. “Morrison ni mchezaji muhimu ambaye bado tunamhitaji, lakini ni lazima atambue kuwa hakuna mtu au mchezaji mkubwa kuliko klabu, ndio maana nilimuondoa kambini,” alisema Eymael huku Morrison akiwaambia mashabiki wafike kwa wingi Taifa kushangilia ushindi.

MILIONI 300 MEZANI

Bilionea anayeidhamini Yanga kupitia kampuni yake ya GSM, Ghalib Mohamed juzi alizungumza na wachezaji na kuwaambia kwamba atawapa Sh300 milioni kama watashinda mchezo huo.

Kwa hesabu nyepesi ni kwamba kila mchezaji atakayevaa jezi leo kama Yanga ikishinda atapata Sh17milioni ikiwa ni zawadi kutokana na mkwanja huo.

Habari za ndani zinasema kwamba alizungumza nao kwa njia ya video akiwa nje ya nchi na kuwaahidi kwamba: “Mkinifurahisha nitaongeza Sh100 milioni kwenye ile milioni 200 ya mechi iliyopita.” Kauli hiyo ilipokewa kwa shangwe na kuongeza mzuka miongoni mwa wachezaji hususan straika David Molinga ‘Falcao’ ambaye leo itakuwa dabi yake ya kwanza kuanza tangu ajiunge na Yanga.

KAMBINI SIMBA

Nahodha wa Simba, John Bocco amesisitiza kwamba mechi hiyo ni muhimu kwa vile wao ni mabingwa wa nchi na wanataka kubeba makombe mawili ili kunogesha ubingwa wao.

Alisema kwamba wanatambua kiu ya mashabiki wao na hawatawaangusha kwani watakwenda uwanjani kusaka ushindi tu ili kucheza fainali.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alitamba akisema, “tunakwenda kushinda mchezo huu hakuna jingine, hatuwezi kufungwa mara mbili. Nimemwambia Clatous Chama kwamba tunahitaji ushindi, nimemtwisha mzigo kwa vile yeye ni mchezaji mkubwa na anaelewa umuhimu wa mchezo huu.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, bilionea kijana Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ yupo nje ya nchi kikazi, lakini juzi jioni aliwaagiza wajumbe watano kwenda kambini Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kuzungumza na wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

Vigogo hao wameweka mezani Sh230 milioni za ushindi na kama wachezaji watawafurahisha zaidi mkwanja utaongezeka ikiwa ni makubaliano yao kwa pamoja na Mo.

Kwa hesabu za vigogo hao wa Simba ni kwamba, kila mchezaji katika wale watakaovaa jezi atakuna Sh15milioni na ushee kutegemeana na jinsi watakavyowafurahisha mabosi kuanzia kwenye staili ya ushindi mpaka idadi ya mabao. Wale wa jukwaani watapozwa kishkaji.

Katika kikao hicho walikuwepo Mwenyekiti msaidizi wa bodi, Salim Abdallah ‘Try Again’, Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa, wajumbe wawili wa bodi Kassim Dewji na Mohammed Nassoro Kigoma pamoja na Katibu Dk Arnold Kashembe.

Kikao kilianza saa 2:00 usiku mara baada ya kupata chakula cha usiku na kumalizika saa 3:15, na kila mjumbe wa bodi alizungumza kuwajaza ‘upepo’ wachezaji kuipiga Yanga ili mji utulie.

Kocha Sven, Bocco na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kwa pamoja walikubali mbele ya kikao hicho kwa niaba ya wenzao kwamba yaliyopita si ndwele na kwamba wamehamasika Yanga ni lazima ifungwe Taifa.

REKODI ZAIBEBA SIMBA

Kama rekodi zitaongea au kujirudia Simba huenda wakamaliza mechi ya leo dhidi ya Yanga kirahisi, lakini mastaa wa zamani wamesema mechi hiyo itakuwa tofauti kabisa.

Tangu Chama tawala (CCM) kianzishwe mwaka 1977, mwanamieleka John Cena na mwanamuziki Kanye West wazaliwe, Simba imekuwa na rekodi za kutisha inapokutana na Yanga mwezi Julai. Rekodi zinaonyesha tangu 1977 ambayo ni miaka 43 iliyopita, Simba na Yanga zimekutana kwenye mashindano mbalimbali ndani ya mwezi Julai mara 10.

Katika mara hizo, Simba imeshinda michezo saba, sare mbili na kupoteza mechi moja ambazo ni sawa na pointi 23. Ni rekodi za kibabe ambazo zinawapa jeuri Simba, ingawa Yanga na wameonekana kupuuzia.

Yanga katika rekodi hizo za mwezi Julai tangu enzi hizo imeshinda mchezo mmoja tu, sare mbili na kuambulia pointi tano. Lakini hata hivyo, kwenye rekodi za jumla katika Ligi Kuu Bara pekee tangu 1965, timu hizo zimekutana mechi 104 na Yanga imeshinda 37, Simba 31 lakini Simba imepoteza 37 huku Yanga ikipoteza 31.

ITASAIDIA?

Mastaa wawili za zamani wa timu hizo, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ na Ally Mayay wamesema mechi hiyo haiamuliwi kwa rekodi.

Mayay alisema: “Mechi inayowakutanisha hawa jamaa wawili inakuwa na mambo mengi, lakini pia mipango ya mwalimu husika inaweza kuamua matokeo siku hiyo kwa upande wowote ule, tumeona licha ya ubora wa Simba lakini mechi ya raundi ya kwanza alitoka sare na raundi ya pili akafungwa.”

Mayay alisema hata sekunde moja inatosha kuamua mchezo huo na rekodi zikatupiliwa mbali.

Mmachinga alisema mchezo huo hauna cha historia wala nini kwa kuwa hautabiriki, akisema: “Unaweza ukawa bora na ukafungika na usiwe bora ukafunga, ni Mungu tu na dakika 90 zitaamua ila kimtazamo wengi wanaipa Simba nafasi kutokana na ubora wao ila mpira haueleweki hasa wanapokutana hawa.”

USHINDANI

Katika mechi iliyopita iliyoikutanisha miamba hii ya soka hapa nchini, Simba walifungwa na Yanga kutokana na udhaifu waliounyesha katika eneo la kiungo.

Katika mchezo huo, Simba ilianza na viungo wawili Jonas Mkude ambaye alikuwa anacheza katika eneo la ulinzi wakati Clatous Chama akicheza kama kiungo mshambuliaji.

katika mchezo huo Yanga walianza na viungo wanne - Feisal Salumu ‘Fei Toto’, Tshishimbi, Balama na Niyonzima ambao waliweza kutawala eneo la kiungo kwa muda mwingi na kutengeneza nafasi moja ambayo waliitumia kufunga bao.

Katika mechi hii benchi la ufundi la Simba limeliona tatizo hilo na kwa mujibu wa mazoezi ya mwisho inaonyesha wataanza na viungo watano ambao watakuwa Gerson Fraga, Mkude, Chama, Francis Kahata na Luis Jose.

VIKOSI

Mpaka jana jioni kwa hali ilivyokuwa kambini kwenye timu hizo vikosi huenda vikaanza hivi Simba: Aishi Manula, Haruna Shamte, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Kennedy Juma/Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Luis Jose, Gerson Fraga, John Bocco, Cletous Chama na Francis Kahata.

Yanga: Metacha Mnata, Juma Abdul, Adeyum Saleh, Said Makapu, Lamine Moro, Feisal Salum, Deus Kaseke, Haruna Niyonzima, David Molinga, Ditram Nchimbi na Bernard Morrison.

REFA NI KAYOKO

BODI ya Ligi na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) imetoa idadi ya waamuzi sita watakaochezesha nusu fainali hii, lakini Mwanaspoti linajua katikati atasimama Ramadhani Kayoko wa Dar es Salaam. Kwenye orodha ya TFF ilivyopangwa mwamuzi namba moja amewekwa Abubakar Mturo wa Mtwara kama atakayechezesha mchezo, ila Mwanaspoti limebaini kwamba ni zuga tu ili kuepuka usumbufu wa timu hizo.

Kati atasimama Ramadhan Kayoko (Dar) ambaye kwenye orodha klabu ilizopewa yuko namba nne. Kayoko atasaidiana na Mturo, Abdallah Mwinyimkuu (Singida), Nadeem Aloyce (Dar), Frank Komba (Dar) na Kassim Mpanga (Dar) huku kamishna wa mchezo huo akiwa Ally Katolila (Dar).

Kayoko alichezesha mchezo wa nusu fainali ya kombe la Azam ambao Simba walipata ushindi wa 2-0 na kuwatoa mashindanoni huku wakitawala sehemu kubwa ya mchezo. TFF wameamua kuchezesha kwa kutumia waamuzi sita ili kupunguza makosa madogo madogo ambayo mara nyingi huwa hayaonekani.

MASHABIKI 30,000 TU

Mkurugenzi wa Maendeleo ya mMichezo nchini, Yusuph Singo amesema mashabiki wanaoruhusiwa kuingia kwenye mechi hiyo ni 30,000 tu ambao ni nusu ya idadi halisi ya watu wanaoujaza uwanja huo.

Singo alisema ulinzi utakuwa mkali ili kuhakikisha suala hilo linafanyika kwa uangalizi mkubwa kuepuka maambukizi ya corona. “Tiketi zitakazotoka ni 30,000 kwa maana ya nusu ya uwanja, mchezo uliopita watazamaji waliingia 59,000 hivyo tumeona tupunguze kidogo ili tuweze kuendana na hali halisi ya kujilinda,” alisema. “Kwa wale ambao hawatapata tiketi huko zinapouzwa katika vituo, basi wasije kabisa uwanjani kwa sababu hazitauzwa kabisa katika maeneo ya uwanja.”

VIINGILIO

Mechi hiyo itapigwa saa 11:00 jioni na kuonyeshwa ‘live’ kwenye vibandaumiza na majumbani kupitia Azam Tv. Viingilio (VIP A) Sh30000, (VIP B) Sh25,000, (VIP C) Sh20,000 huku mzunguko ni Sh10,000. Kwa hesabu ya kawaida ni kwamba wakiingia mashabiki 30,000 kwa kiingilio cha Sh20,000 ni sawa na Sh1.1 bilioni.

COSTA: MSIDHARAU

BEKI wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Victor Costa amesema: “Mchezo uliopita Simba ilijiamini zaidi, ndio maana wakafungwa, wakibadilika watakuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi, lakini ikiwa watacheza kama mechi zilizopita sidhani kama watapata ushindi.”

“Kwenye mchezo uliopita waliocheza na Yanga, baadhi ya makosa yalikuwa ni ya kawaida na hiyo ndio ilitokana na kujiamini kwao, lakini walionekana kubadilika siku hadi siku mpaka wakafanikiwa kuchukua ubingwa.”

“Mimi nafikiri bado wapo vizuri, ila chakuwasihi ni kwamba wasijione bora zaidi, kwenye mpira unaweza ukawa na timu nzuri lakini ukafungwa pia.”

IMEANDIKWA NA KHATIMU NAHEKA, OLIVER ALBERT, MUSTAFA MTUPA NA THOBIAS SEBASTIAN