Wakili akwamisha ushahidi kesi ya kina Malinzi

Muktasari:

  • Wakili wa Serikali, Imani Nitume alidai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi

Kesi ya utakatishaji inayomkabili aliyekuwa Rais wa (TFF) Jamal Malinzi na wenzake imeshindwa kuendelea na ushahidi kutokana na wakili anayeendesha shauri hilo kutofika mahakamani.

 Wakili wa Serikali, Imani Nitume alidai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru),Leonard Swai anayeendesha shauri hilo amepata majukumu mengine. "Pia shahidi aliyeandaliwa kwa ajili ya kutoa ushahidi amepata udhuru hivyo tunaiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza ushahidi,"alidai Nitume. Wakili wa Utetezi,Kashinde Thabiti alidai kuwa siku ya kusikiliza shauri hilo upande wa mashtaka waandae mashahidi zaidi ya watatu na inapotokea wakili Swai anakuwa na majukumu mengine wawakilishwe na mawakili wa serikali wanaoendesha kesi hiyo. Hakimu Mkazi,Maira Kasonde aliwataka upande wa mashtaka kuhakikisha wanaleta mashahidi.Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 26,2019 kwa ajili ya uendelea na ushahidi. Katika kesi hiyo hadi sasa mashahidi 11 wameshatoa ushahidi hata hivyo mahakama hiyo ilikataa kupokea maelezo ya onyo ya washtakiwa Flora Rauya na Miriam Zayumba ambayo walihojiwa na ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( Takukuru ),Frank Mkilanya kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo. Mbali na washtakiwa hao, wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Malinzi, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine(46) na Mhasibu wa TFF,Nsiande Mwanga (27). Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa dola za Marekani 173,335. Summary Kesi ya utakatishaji inayomkabili aliyekuwa Rais wa (TFF) Jamal Malinzi na wenzake imeshindwa kuendelea na ushahidi kutokana na wakili anayeendesha shauri hilo kutofika mahakamani.