Wakali walioanzia benchi Ligi Kuu England msimu huu

Muktasari:

  • Kwenye soka hawa wanaitwa super sub. Hawa hapa ndio super sub matata kabisa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu wakati ligi hiyo ikiwa imeshuhudia mechi 23 zilizopigwa.

LONDON, ENGLAND.KILA timu yenye kikosi matata cha kwanza kuna wachezaji hao wanaoanzia benchi, wanapoingia wanakuwa habari nyingine. Ukweli ni kwamba wachezaji hao si kama hawana uwezo ndio maana wanaanzia benchi, la viwango vyao ni vikubwa, sema kocha ni lazima awe na kikosi chake cha kwanza anachoanza nacho.

Kwenye Ligi Kuu England wapo wachezaji hao wanaoanzia benchi na kila wanapoingia uwanjani, basi wamekuwa wakifanya mambo makubwa kusaidia timu zao.

Kwenye soka hawa wanaitwa super sub. Hawa hapa ndio super sub matata kabisa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu wakati ligi hiyo ikiwa imeshuhudia mechi 23 zilizopigwa.

5. Romelu Lukaku

(Mechi 7, mabao 3)

Straika wa Manchester United, Romelu Lukaku amekuwa akipambana kuweka sawa kiwango chake cha soka kwa msimu huu baada ya mambo kuwa magumu upande wake. Kutokana na hilo, Lukaku amejikuta akiishia kwenye benchi mara kadhaa. Lakini, mara zote alizotokea benchi, Lukaku alijaribu kuonyesha yeye ni matata baada ya kuhusika kwenye mabao matatu.

Lukaku ametokea benchi mara saba, akifunga mabao mawili na kuasisti moja, hivyo kumfanya awe amehusika kwenye mabao matatu katika mechi saba alizotokea kwenye benchi.

4. Erik Lamela

(Mechi 7, mabao 4)

Winga wa Tottenham Hotspur, Erik Lamela, ameonyesha kama kuna kitu anachoweza kukifanya vizuri kwenye mchezo wa soka basi ni kuanzia benchi kisha kuingizwa baadaye akiwa ameshausoma mchezo wote.

Amekuwa na kiwango bora, lakini Kocha Mauricio Pochettino amekuwa akipendelea zaidi kumwaanzishia kwenye benchi. Kwenye Ligi Kuu England msimu huu ameanzishwa mara saba tu, huku mechi saba akitokea kwenye benchi na kuhusika katika mabao manne.

Katika mechi hizo saba alizotokea benchi, Lamela amefunga mabao mawili na kuasisti mengine mawili.

3. Xherdan Shaqiri

(Mechi 7, mabao 4)

Wakati anasajiliwa na Liverpool, Xherdan Shaqiri alionekana kama mzigo tu, lakini baada ya ligi hiyo kuchezwa kwa mechi 23, fowadi huyo wa kimataifa wa Uswisi amethibitisha ni mmoja kati ya usajili bora kabisa uliofanywa na Kocha Jurgen Klopp.

Fowadi huyo wa zamani wa Stoke City ameipa Liverpool wigo mpana wa uteuzi wake wa wachezaji kwenye safu ya ushambuliaji kwani anapoanzia benchi, akiingia basi timu hiyo inakuwa na nguvu mpya kama ilivyotokea kwenye mechi dhidi ya Manchester United, ambapo alitokea benchi na kufunga mabao mawili.

Kwa msimu huu, Shaqiri ametokea benchi kwenye mechi saba za Ligi Kuu England na kuhusika kwenye mabao manne, akifunga matatu na kuasisti mara moja.

2. Aubameyang

(Mechi 2, mabao 5)

Straika wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang panga pangua amekuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Unai Emery kwa msimu huu.

Fowadi huyo mara nyingi amekuwa akianzishwa na jambo hilo limemfanya alipe fadhila kwa kocha wake kutokana na kufunga mabao 14 katika ligi hiyo hadi sasa.

Lakini Aubameyang ameshawahi kutokea benchi kwenye mechi mbili za Ligi Kuu England msimu huu, dhidi ya Fulham na Leicester City. Kwenye mechi hizo, Aubameyang ameonyesha kuwa matata kwelikweli anapoanzia benchi, kwani mara mbili alizofanya hivyo amehusika kwenye mabao matano, akifunga manne na kuasisti moja.

1. Aaron Ramsey

(Mechi 11, mabao 6)

Kiungo Aaron Ramsey yupo kwenye miezi yake sita ya mwisho kwenye kikosi cha Arsenal. Msimu huu ukimalizika atatimkia zake Juventus kwenda kuanza maisha mapya. Ramsey kwa msimu huu amekuwa haanzishwi sana na Kocha Unai Emery kwenye kikosi kinachoanza, lakini hilo halijamfanya ashindwe kufanya mambo matamu na kuisaidia timu yake. Kwenye Ligi Kuu England kiungo huyo wa kimataifa wa Wales ameanzia benchi kwenye mechi 11 na kuhusika katika mabao sita. Kwenye mechi hizo alizoanzia benchi, Ramsey amefunga mabao mawili na kuasisti manne, hivyo awe amehusika kwenye jumla ya mabao sita katika kikosi hicho cha Washika Bunduki wa Emirates.