Wakali wa pasi za mabao Ligi Kuu England hawa hapa

Thursday January 10 2019

 

LONDON, ENGLAND.MBIO za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England zimerudi upya kabisa. Kwa sasa timu zinakaba koo kinoma, ukizubaa tu umeachwa.

Liverpool, Manchester City na Tottenham Hotspur zimeachana pointi chache sana, lakini kuna timu nyingine kama Chelsea, Arsenal na Manchester United zipo kwenye mchakamchaka huo kuhakikisha vita inakuwa kali hadi filimbi ya mwisho ya kufunga pazia la msimu huu.

Kwa sasa zimeshachezwa mechi 21 kwenye ligi hiyo na kushuhudia wakali kibao ikiwamo hawa wanaoongoza kwa kupiga asisti nyingi msimu huu.

6.Paul Pogba- asisti 6

Kiungo wa Manchester United, Paul Pogba amekuwa kwenye kiwango bora kabisa tangu timu hiyo ilipoanza kuwa chini ya kocha wa muda Ole Gunnar Solkjaer. Hapo kabla, Pogba alikuwa kwenye wakati mgumu sana chini ya Kocha Jose Mourinho na kuwa na malumbano yasiyokwisha.

Kwa sasa anafunga na kuhusika kwenye mabao mengine. Msimu huu, hadi ligi ilipofikia kwa sasa, kiungo huyo Mfaransa amepiga asisti sita. Wachezaji wengine wenye asisti sita kwenye ligi msimu huu ni pamoja na Marcus Rashford, Aaron Ramsey na Bernado Silva.

5.Raheem Sterling- asisti 7

Ushindi wa Manchester City wa mabao 2-1 dhidi ya Liverpool umefanya mchakamchaka wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England kuanza tena upya kwani kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo, kuna tofauti ya pointi nne tu na wakati bado kuna mechi kibao za kuchezwa. Katika mechi hiyo, Raheem Sterling ndiye aliyepiga asisti ya bao la ushindi lililofungwa na winga wa Kijerumani, Leroy Sane. Jambo hilo lilimfanya Sterling awe amefikisha asisti saba kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Sane pia ana asisti saba.

4.Christian Eriksen- asisti 7

Tottenham Hotspur inakuwa matata uwanjani wakati supastaa wake, Christian Eriksen atapokuwa kwenye ubora wake. Kiungo huyo mchezeshaji ni fundi kwelikweli wa mpira na mabeki wamekuwa wakiteseka sana kwenye kumkaba. Eriksen ni fundi mkubwa wa kupiga pasi za mwisho na ndio maana hadi sasa kwenye Ligi Kuu England zikiwa zimechezwa mechi 21, amepiga asisti saba na hivyo kuwa kwenye orodha ya wakali waliopiga pasi nyingi za mabao kwenye mchakamchaka wa ligi hiyo yenye upinzani mkali kwenye kuwania ubingwa, Top Four na kukwepa kushuka daraja.

3.Mohamed Salah- asisti 7

Fundi wa kufunga wa Liverpool, Mohamed Salah ameendelea kuonyesha uwezo wake wa kupasia nyavu unapungua anapocheza dhidi ya timu za Top Six kwenye Ligi Kuu England. Staa huyo hivi karibuni amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika kwa mwaka 2018, amewafunga Arsenal tu tena kwa mkwaju wa penalti. Alhamisi iliyopita, Liverpool ilichapwa na Manchester City 2-1, huku bao la wababe hao wa Anfield likifungwa na Roberto Firmino. Lakini, hadi ligi ilipofikia kwa sasa, Mo Salah amefunga mabao 13 na kuasisti mara saba na kuwa kwenye orodha ya wachezaji waliopiga asisti nyingi kwenye Ligi Kuu England.

2.Ryan Frazer- asisti 9

Bournemouth imekuwa na msimu mzuri kwenye Ligi Kuu England hadi sasa. Siku za karibuni imekuwa ikikutana na wakati mgumu, lakini kitu kizuri kwao ni kwamba walianza vyema mwanzo wa msimu.

Kikosi hicho cha Kocha Eddie Howe kinashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi, ikikusanya pointi 27.

Kikosi hicho kinajivunia kuwa na huduma ya winga Ryan Frazer, ambaye ndiye aliyepiga asisti nyingi katika mechi 21 zilizochezwa hadi sasa kwenye ligi hiyo. Frazer amepiga asisti tisa.

1.Eden Hazard- asisti 9

Kevin De Bruyne alikuwa bingwa wa asisti kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, lakini msimu huu majeraha yamemtibulia na staa huyo wa Kibelgiji amepotea kabisa.

Eden Hazard kwa sasa ndiye anayefunika kwenye kitendo hicho cha kupiga asisti matata kabisa kwenye ligi hiyo akipiga asisti tisa hadi sasa. Huduma ya Hazard hakika ni bora kabisa na ndio maana Chelsea inapambana na hali yake kuhakikisha inambakiza Stamford Bridge kwamba asishawishike kwenye kokote kule.

Advertisement