Wakali hawa wa Ligi Kuu England wameshuka daraja na utamu wao

Muktasari:

Mfano mzuri ni nyota hawa 8, wasiostahili kukosekana kwenye EPL msimu ujao.

MSIMU wa 2018/19 umemalizika. Kilichotokea kila mtu anafahamu. Pep Guardiola ametetea taji lake. Jurgen Klopp, anasubiri ubingwa wa UEFA. Sijui itakuaje, Juni Mosi ndio mwamuzi.

Hata hivyo, katika harakati hizo za ubingwa wa EPL, kuna wachezaji ambao, licha ya ubora wao, wamehukumiwa pamoja na timu zao mbovu.

Mfano mzuri ni nyota hawa 8, wasiostahili kukosekana kwenye EPL msimu ujao.

8. NEIL ETHERIDGE (CARDIFF)

Ndiye mchezaji bora wa mwaka wa klabu ya Cardiff City. Kipa huyu, raia wa Ufilipino, alikuwa mchezaji muhimu sana katika kikosi cha The Bluebirds. Alikuwa mmoja wa makipa walionesha uwezo mkubwa msimu huu, pengine kuliko hata David de Gea.

Kwa bahati mbaya, licha ya kuitandika Man United 2-0, kwenye mchezo wa mwisho, Neil Etheridge na timu yake, wameshuka daraja, baada ya kumaliza katika nafasi ya 18. Kuna tetesi kuwa, Bournemouth inamhitaji. EPL bado inahitaji uwezo wake wa kupangua Penalti.

7. AARON MOOY (HUDDERSFIELD)

Pamoja na ukweli hakufikia nusu ya kiwango alichokuwa nacho, akiwa Yorkshire, lakini kwa kuzingatia masahibu ya Huddersfield, ni sahihi kusema alichokifanya Aaron Mooy (28), si haba.

Uwezo wake wa kupiga pasi na kufunga mipira iliyokufa, ni ishara bado EPL inamhitaji.

6. VICTOR CAMARASA (CARDIFF)

Ni nadra kusikia Neil Warnock amesajili fundi wa mpira kutoka Hispania. Hata hivyo, hii imekuwa tofauti unapoizungumzia Cardiff City.

Kwa mara ya kwanza pengine, kocha huyo amepata zali ya kushuhudia ubora wa miguu ya Victor Camarasa, katika kikosi chake. Huyu alikuwa ni fundi aliyeonyesha uhodari, umahiri na uzoefu mkubwa.

Pamoja na ubovu wa Cardiff City, Camarasa bado aling’ara na kuzitambia klabu kubwa kama Man United, Chelsea na Leicester City.

Mhispania huyo aliyejiunga na Cardiff, kwa mkopo, akitokea Real Betis alifunga mabao matano na kutoka asisti nne, anahusishwa na Tottenham.

Ingekuwaje kama angekuwa katika kikosi makini kama cha Man City au Liverpool?

5. PHILIP BILLING (HUDDERSFIELD)

Miezi miwili imepita tangu Philip Billing alipoichezea Huddersfield mara ya mwisho msimu huu. Hakuwa chaguo la Jan Siewert, lakini kipenzi cha wachezaji wenzake, ambao walimpigia kura ya mchezaji bora wa mwaka wa klabu hapo.

Fundi wa kurusha mipira na kupiga mashuti. Msimu huu tu amegonga mwamba mara tatu na kufunga mabao mawili kwa mashuti. Umri umemtupa mkono, lakini bado ni aina ya mchezaji ambaye anaweza akafiti kwenye kikosi chochote kile cha EPL.

4. JEAN-MICHAEL SERI (FULHAM)

Labda huyu ndio mchezaji aliyeboronga zaidi msimu huu. Jean- Michael Seri, hakuwa na msaada wowote kwa Fulham. Kwa pamoja wakashuka daraja.

Huenda pia, aina ya wachezaji waliomzunguka pale Fulham wamechangia kiwango chake kuporomoka.

Hata hivyo, ingekuwaje kama mwaka 2017 Barcelona wangemsikiliza Xavi, alipowashauri kumsajili kama mrithi wake?

3. TERENCE KONGOLO (HUDDERSFIELD)

Miaka mitano imepita tangu Uholanzi ilipoamua kumwacha Virgil van Dijk katika kikosi chao, kilichoshiriki Kombe la Dunia mwaka 2014, kwa faida ya Terence Kongolo. Wakati huo Kongolo alikuwa bora zaidi ya Van Dijk, miaka mitano baadae, stori imebadilika.

Mmoja ameporomoka huku mwengine akipanda chati na kuwa mmoja wa mabeki bora wa kati duniani. Hadithi ya Waholanzi hawa inafurahisha na kuhuzunisha vilevile. Wakati Van Dijk anasubiri mechi ya fainali ya Uefa, Kongolo anasubiri msimu wa Ligi Daraja la Kwanza uanze.

2. ALEKSANDAR MITROVIC (FULHAM)

Licha ya ukame wa mabao uliomtembelea katika nusu ya pili ya msimu, Mitrovic bado aliweza kufunga mabao 11, bao moja zaidi ya Leroy Sane. Eti Romelu Lukaku kamzidi bao moja tu? Maajabu haya!

Maana yake, atakayemlaumu Mitrovic kutokana na masahibu ya Fulham atakuwa anakosea sana. Alifanya aliwezalo kuisaidia klabu yake. Unaanzaje kumlaumu mtu aliyetoa asisti nyingi zaidi ya Lukaku?

Mserbia huyu, hastahili kuwa nje ya EPL. Ligi Daraja la Kwanza sio hadhi yake kabisa. Kuna tetesi West Ham inahitaji huduma ya miguu yake. Hata Chelsea inamhitaji zaidi ya inavyowahitaji Gonzalo Higuain na Olivier Giroud.

1. RYAN SESSEGNON (FULHAM)

Huu haujawa msimu mzuri kwake. Licha ya kutoa asisti sita, ni dhahiri kiwango chake kimeporomoka sana. Ryan Sessegnon hata hivyo, anastahili kupewa nafasi nyingine. Msimu ujao anaweza akaja kivingine akipata timu ya maana kama Spurs.